Bw. Elias Mwembe |
Mifugo ikiwa chini ya ulinzi wa mbwa |
![]() |
Mhariri wa JICHO LANGU BLOGU mtandao wa kijamii |
Vijana wakisindikiza mifugo kwenda malishoni |
Hili ni Josho la mifugo limekuwa msaada mkubwa |

![]() |
Steve Jonas, fikra pevu ! |
Na Steve Jonas,Mbeya
+255 (0)762 876 892
MFUGAJI Bw. Elias Mwembe mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chunya mkoani Mbeya ameanzisha mbinu mpya za kuwajengea watoto uwezo wa kwenda
shuleni ili kukuza elimu Wilayani humo.
Aliyazungumza hayo hivi karibuni mjini Chunya na kufafanua
kwamba idadi kubwa ya wazazi Wilayani humo wanashindwa kuwaandikisha
shuleni watoto wao kutokana na sababu zilizojigawa kwenye
makundi makubwa mawili aliyoyataja kuwa ni uchimbaji wa dhahabu na kuchunga
ng’ombe.
Bw. Mwembe ambaye pia ni mkulima, alisema baada ya kugundua
hayo aliamua yeye awe mfano wa kuigwa kwa wafugaji wengine ambapo amebuni mbinu
mpya ya Mbwa kuchunga ng’ombe badala ya binadamu kuendelea kufanya shughuli
hizo na kushindwa kufanya kazi zingine za kiuchumi.
Alisema yeye binafsi amefuga mbwa wasiopungua 100 ambao
amewagawa katika makundi matatu kulingana na makundi ya ng’ombe 1,000, kazi ya
mbwa hao ni kuwachunga ng’ombe kwenye maeneo ya malisho ambapo ana zaidi ya
miaka minne tangu mbinu hiyo ianze kutumika.
Alifafanua kwamba nguvu kazi ya binadamu inayotumika kwenye
mifugo hiyo kwa sasa ni ndogo kutokana na kwamba nguvu inayotumika ni kuiongoza
mifugo kwenda kwenye malisho majira ya saa moja asubuhi na ikifika saa tano
wanaifuata na kuirudisha nyumbani kwa ajili ya kukamua maziwa na lishe ya
ndama.
Mfugaji huyo alieleza kuwa baada ya kukamua mifugo hiyo
inaongozwa tena kwenda malisho kisha kuachwa ikilindwa na mbwa hadi saa 11 za
jioni muda wa kurejeshwa nyumbani.
Alisema wafugaji kama wataiga mbinu hiyo itatoa fursa kwa watoto
wa jamii hiyo kuhudhuria masomo badala ya kutumikishwa kwenye mifugo na kupoteza vipaji vyao vilivyofichama na
kudumazwa kwa tamaduni dume ambazo alizitaja kuwa kwa sasa zimepitwa na wakati.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya mpango huo alisema anahakikisha
mbwa wanapata chakula cha kutosha mara mbili kwa kila siku na hadi sasa wamesha
zoea muda wa chakula na majukumu yao wakiwa kwenye malisho.
‘’Chakula cha mbwa kinaandaliwa na wake zangu mara mbili kwa
siku, nashukuru Mungu kwamba mbwa wamekuwa wakifanya kazi vizuri kwa sababu
sijawahi kupata malalamiko kutoka kwa wakulima kwamba mifugo yangu imevamia
mazao, haijawahi kutokea na hilo ndilo linalonipa moyo kwamba kumbe
inawezekana’’. Alisema
Mfugaji huyo amejitolea kujenga josho la mifugo ambalo limekuwa
msaada kwa wafugaji wa maeneo mbalimbali hasa kwenye kanda ya Mlimanjiwa,
wafugaji hao wanachangia kiasi cha Shilingi 150 kwa kila ng’ombe mmoja gharama
ambazo ni ndogo ikilinganishwa na majosho mengine ambayo wafugaji hutozwa
Shilingi 500 kila ng’ombe mmoja.
‘Nimefanya hivyo ili kuwasaidia wafugaji wenzangu na
nilitaka kusiwe na gharama yoyote ila nimelazimika kwa ajili ya kuchangia
gharama za dawa’. Alisema
Bw. Mwembe alisema anaungana na Serikali kukemea vitendo vya
wazazi kuwaruhusu watoto kujihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini badala
ya kuthamini elimu ambayo ndiyo msingi wa maendeleo taifa.
‘’Kama ingewezekana natamani ningerudi utoto ili nisome kwa
bidii niweze kulitumikia taifa kikamilifu lakini bahati mbaya umri umenitupa
mkono hivyo sina budi kubuni mipango inayoweza kuinufaisha jamii na taifa kwa
ujumla’’. Bw. Mwembe alisema
Vilevile, aliwataka vijana kuzitumia fursa zao kwa shughuli
za kujiendeleza kielimu, ufugaji na kilimo ili kujikwamua kiuchumi badala ya
kubobea kwenye uchimbaji wa madini ambao kwa sasa ni ghari pia unahitaji kisomo
na vitendea kazi vya kisasa ili kulinda mazingira lakini pia kupata faida.