

Historia hii fupi ya msanii huyo katika uhai wake ambaye kwa
hakika alikuwa mpiganaji wa Gheto ,inaandikwa
na Steve Jonas.

Alikuwa mtoto mpenzi wa Gheto,alipigana kwa kutumia sauti
yake na nyuzi za gitaa lake.Mikogo ya sauti yake ilivuma kote Duniani
akafurahisha,akaamsha ,akasuta na akahimiza.


Bob ambaye alikuwa akipigania Uhuru na haki katika staili ya
midundo ya Regae,baba yake alikuwa ni afisa wa Jeshi kikosi cha maji nchini
Uingereza ambaye alifariki wakati Bob angali tumboni mwa mama yake Bibi Cedella
Booker mwanamke wa kiafrika.
Mama yake Bob alikuwa mwimbaji mahiri wa kwaya kanisani Bob
aliupitisha udogo wake huko shamba kwenye mazingira ya wakulima wa ndizi na
minazi ,akinywa madafu,akiwakamua ng’ombe maziwa na mbuzi pia aliogelea kwenye
vijito na Bahari.
Bibi Cedella Booker hakutaka mwanaye aishie kutanga tanga na
kuzurura.Aliogopa mwanaye kuharibika kama ilivyo kwa watoto wa familia zingine
zenye tabaka la chini, alitamani sana mwanaye ajifunze kazi yoyote ya ufundi
ambayo ingeweza ingeweza kumudu maisha yake hapo baadae.




Desmond Dekker baada ya muda akatoa kibao chake cha muziki
kilichoitwa ‘Honour Thy Father and Thy Mother’ akimaanisha ‘waheshimu Baba na
Mama’wimbo huu ulipendwa sana na katika mafanikio hayo ilikuwa ni kijana huyo
kusaidiwa na studio za Beverleys.
Mambo yalipo mnyookea katika muziki,Desmond alimshawishi Bob
ajaribu kuupa wasaa zaidi muziki.Bob alikubaliana na ushauri wa Desmond na
walikwenda kwenye studio za Beverleys. Huko Bob akakutana na Jimmy Cliff mwana
muziki mashuhuri.
Cliff mbali ya umaarufu aliokuwa nao wa kimuziki hasa katika
sinema ya ‘The Harder They Come’,alikuwa na moyo wa huruma na kupenda kusaidia
akamsaidia Bobo kwa vifaa na ushauri mpaka hapo Bob alipofanikiwa kuipua wa
kwanza wa ‘Judge Not’.
Wakati huo Robert Nesta Marley alikuwa na umri wa miaka 15 tu,wakati
huo huo mama yake tayari alikwisha hamia Marekani(U.S) alimwacha Bob akijifunza
‘welding’.
Baadae Bob alipokuwa akiishi Gheto huko Trench Town kwenye
nyumba ya baba yake Bonny Livingstone ikiwa ni muda mfupi tu tangu alipounda
urafiki na Bonny,kijana mmoja mwembamba mrefu,mcheshi mwenye maneno mengi,Peter
Tosh alionekana akipitapita mitaani akiwa na Gitaa lake.
Alikuwa akipiga na kuimba,akicheka na kutania,akitukana na
kuchokoza na ubishi kama jadi yake.Watu hawa watatu ndio walioanzisha kundi zima
la The Wailers.Waanzilishi hao ni BonnyLivingstone,Bob Marley na Peter
Tosh.Mwanzoni walijiita The Wailing Wailers.
Baada ya vigogo hao kupatana vyema huko Kingstone katika
Gheto la Trench Town,ndipo mwimbaji mwingine alijiunga aliyeitwa Junior Braith Waite
lakini hakuweza kukaa sana kutokana na wazazi wake kuhamia Marekani ambako
ilibidi aongozane nao.
Kulikuwepo pia wasichana wawili ambao ni Rita ambaye baadae
alikuja kuolewa na Bob Marley na Beverley Kelso.Lakini akina dada hawa
hawakudumu sana japo walikuwa waimbaji wazuri sana,huko mbele Rita akiwa The I
Threes alikuja kuendelea kuimba na Marley.
Huku wakidhaminiwa na Beverleys Records.Bob,Bonny na Tosh
wakayapanda majukwaa ya Kingstone wakiimba nyimbo zenye mtazamo wa kibiblia
pamoja na nyimbo za mapenzi kama vile wimbo wa ‘Do It Twice’waliimba nyimbo za
kuchangamsha na kuliwaza vijana wa Gheto.
Waliwaliwaza vijana wa Gheto kwa sababu ya kukosa kazi huku
wakizongwa na Polisi,pia waliimba nyimbo za kuulaani utumwa ambao mtu mweusi
alikabiliwa nao kwa muda mrefu sana hali ambayo ilionyesha kama vile mtu mweusi
hana haki yake hapa Duniani.
Kujulikana kwa vijana hawa kuliongezeka zaidi hasa pale
walipo chukuliwa na ‘Studio one’ ya jamaa aliyeitwa Coxsone Dodd,huyu jamaa alikuwa maarufu sana
hasa katika utengenezaji wa Santuri,lakini mambo hayakuwa mazuri kwa wapiganaji
hao kuhusiana na kipato.
Coxsone Dodd hakuwa na nia ya kupanua vipaji vya Bob ,Tosh
na Bonny kwani alitaka wamtumikie ,awanyonye, awakamue kasha wabaki hohehahe
kimuziki au kwa namna nyingine wasingeweza kupigania haki za wengine huku wao
wenyewe wakinyimwa haki zao kimuziki.
Mnamo mwaka 1966,Wailers waliipua kibao kama vile Put It
On,Rude Boy, I’m still waiting na Rule them Rudie ambazo zilimwingizia kipato
kikubwa Coxsone Dodd,ilfika sikukuu ya Krismasi ambapo vijana hao walidai haki
yao ili wakafurahi na wenzi wao Trench Town,Gheto.
Dodd akawapa Paund 60,Bob hakuweza kuvumilia akazichukua
pesa hizo na kumtupia usoni Dodd kasha akaanza safari ya kumfuata mama
yake Marekani huko akaendelea kutunga
nyimbo kama vile wimbo uitwao ‘Bend Down Low’.
Akiwa huko Marekani Bob akapata kibarua katika kiwanda cha
kutengeneza magari aina ya Cryster kilichopo mjini Delaware,lakini huko Amerika
hakukaa sana aliamua kuondoka nchini humo baada ya kupata barua .
Barua aliyoipata Bob ilimtaka akapigane vita huko
Vietnam,wazo hilo Bob hakuafikiana nalo huku akijiuliza ni kwa nini aende
kupigana vita au kushiriki katika suala la mauaji ya watu wasio na makosa
,akarudi Jamaica.
Ulimwengu wa kibepari bado uliendelea kumtupa huku na kule
,aligundua kuwa kila mahali wanataka kumtumia au kukitumia kipaji chake cha
muziki ili wajitajirishe wao au kumtumia kama kibarua mchomeaji kasha kumlipa
ujira mdogo ama kutumia ujana wake katika vita huko Vietnam kwa manufaa ya
mabeberu.
Watu hawa wanajifanya ni marafiki kumbe wanataka kumtumia tu
kama ilivyokuwa kwa Coxsone Dodd ambaye alijifanya rafiki kipenzi wa Bob hata
kufikia hatua ya kumsaidia Bob chumba cha kulala nyuma ya Studio One lakini Bob
alipodai haki yake alipewa paund 60 tu ambazo Dodd alitupiwa usoni kwa hasira.
‘Watoto,
Mwanadamu anamdhurumu mwanadamu mwenzie,
Mpaka unashindwa kujua yupi umwamini,
Adui yako mkubwa anaweza kuwa rafikio mkubwa ,
Na rafikio mkubwa anaweza kuwa adui yako mkubwa,
Wengine watakula na kunywa nawe,
Kumbe nyuma yako wanakuhujumu,
Ni rafiki tu ajuae siri yako,
Hivyo ni yeye tu awezaye kuitoa ,
Mwache aivae kofia Yule ambaye inamtosha,
Maneno hayo yanaonyesha hali halisi Bob alivyo itambua jamii
ya Kibepari na ndipo alipoamua kuifikishia ujumbe huu Dunia nzima kupitia kibao
chake cha ‘Who The Cape Fit’katika Santuri ya Rastaman Vibration.
Basi,Bob mambo yake yaliendelea kusua sua huko Jamaica kwa
sababu hakuwa na pesa wala mtaji kwani walio kuwa na uwezo huo walikuwa Chui
ndani ya ngozi ya Kondoo,wanafiki na makupe.
Wailers wakaendelea na Regae katika hali ya nguvu na
kushindana na umasikini na unyonyaji,mwaka 1969 Lee Perry Scratch ambaye zamani
alikuwa akimfanyia kazi Coxsone Dodd,akawa ameeanzisha Studio yake mwenyewe
iliyoitwa Upsetter .
Upsetter ikishirikiana na kampuni ya Trojan Records ya
Uingereza na kutoa Albam za Wailers Rasta Revolution Herbsman.Wailers wakawa
wamewasha moto na kuushitua Ulimwengu,sasa masikio yakawa yameelekezwa huko
Jamaica na Regae ikaanza kuingia kwenye damu za watu wa nje ya Jamaica.
Wailers wakiwa na studio ya Lee Perry Scratch (Upsetter),Bob
,Peter na Bonny wakakutana na ndugu wawili ,hao walikuwa watoto wa mzee Barett
ambao ni Carlton Barett(Carly) na Aston Barett (Family Man),Carly alikuwa mpiga
ngoma (Drums) na Family Man alikuwa akipiga Gitaa zito.
Katika nguvu hiyo mpya Bob ,Peter na Bonny waliandika nyimbo
za kuziimba ,Carly na Aston wakakamata vyombo vyao kwa hakika wote walikuwa na
uwezo wa kuimba na wote walikuwa na uwezo wa kupiga vyombo,siku za harakati
hizo zikaendelea .
Baade Bob Marley alipokutana na Chris Black Well,ambaye
alikuwa mtengenezaji Santuri,Black Well alikuwa mzungu aliyetokea kwenye
familia ya kitajiri tena ya kikoloni nay a kibaguzi,alijichanganya na wafanya
kazi weusi huko Uingereza akajifunza Lugha na tabia zao akawazoea na wakamzoea.
Kampuni yake ya kutengeneza Santuri hakuianzisha kifahari na
kitajiri katika vitongoji vya Mabepari bali alianzisha kwenye kitongoji chenye
makazi ya watu weusi.
Chris aliyatazama macho maangavu ya Bob,akautazama mwili
wake mdogo ulio shupaa, akaisikiliza sauti yake iliyo jaa hisia ,hamasa na
azma…’Bob anatetea kitu chenye uzito mkubwa ‘.Alisema Chris Black Well. ‘Na The Wailers ni kundi kubwa kisanaa
,naamini ni watu wanaostahili kupata msaada ,muziki wao unauzito kuliko wa
Rock’.Alisema Chris.
Hayakuwa maneno matupu ,Chris aliwapatia The Wailers vifaa
vipya tena vya kisasa ambavyo hapakuwa na Bend yoyote ya Jamaica ambayo iliwahi
kumiliki au kuvitumia vyombo vya aina ile.Wakaamua kutengeneza Albam za Stereo.
Uuzaji na usambazaji wa Black Well ulikuwa mzuri sana
.Wailers wakapiga Regae nzuri ,na Island Records yaani kampuni ya Black Well
ikarekodi na kuuza Albam vema ingawa yeye Chris hakuwa mwanamuziki (mpigaji).
Hakika alitoa mchango mkubwa kuuza na kuusambaza muziki wa
Regae Duniani kote hata kuwepo kwa gumzo kubwa kuhusiana na kundi zima la The
Wailers,pia hatuwezi kuzungumzia The
Wailers bila kumtaja Chris Black Well.Aliwapa kila kifaa walichokitaka hata
studio aliwaachia .
Studio hiyo waliitumia walivyo taka ,wakati
wowote,akawatengenezea Santuri za stereo,akazisambaza vizuri kote .Albam ya
‘Catch a Fire’ ilitolewa mwaka 1973 ikiwa ni moja ya kazi za Island Records na
kila mpenda Regae aliifurahia Albam hiyo.
Mnamo mwishoni mwa mwaka 1973,baada ya ziara ya The Wailers
kutoka London ,Bunny Wailer alionyesha wazi kuwa hakuwa tayari kuendelea na The
W ailers.Naye Yule kijana mrefu ,mbishi,aliyejiamini sana Peter Tosh asiye
kubali kudhalilishwa pia alionyesha nia kama ya Bunny.
Redio,Matangazo,Magazeti ya Kibepari hayakutaka kabisa
kukubali mafanikio ya The Wailers kwamba yalitokana na bidii za pamoja za
wahusika wote,bali vyombo vyote hivyo viliamini kwamba kila kitu kilifanyika na
Bob Marley na hao wengine walifanywa kama vijana wake tu kitendo ambacho
kiliwaudhi Bunny na Tosh,hizo zilikuwa hisia ,mbinu za mabepari ili kuhakikisha
wanawatenganisha.
Hata kama Bob alikuwa kiongozi ,wenzie pia walikuwa na
umuhimu mkubwa na walifanya kazi kubwa .Bunny na Tosh walikuwa si waimbaji
wazuri tu bali pia walikuwa watunzi wazuri wa nyimbo na upigaji wa kama Carly
na Aston haikustahili kudhalilishwa .
Bunny akaamua kuwa mkulima ,akashika shamba katika sehemu iitwayo Bull Bay,akiwa na ndoto moja
,kuzalisha chakula kingi iwezekanavyo,ikiwezekana cha kuweza kuilisha Jamaica
nzima.Lakini hakuacha muziki,baada ya muda akaipua albam ya Black Heart Man.
Katika wimbo huo ,Bunny kuna maneno anayasema akidai kwamba
‘walimuua Lumumba kwa kupigania haki zake ,lakini hawawezi kumzuia Rasta’.Naye
Peter hakuacha muziki wala hakufa kimuziki kama baadhi ya magazeti ya kibepari
yalivyo tabiri.
Yalidai kuwa kiburi cha Tosh baada ya kujitenga kilimfanya
amuonee wivu Robert Nesta Marley.Ili kukata ngebe hizo za wanafiki,Tosh
alipakua Albam ya Legalise It na Equal Rights.Wakaanza kusema Tosh si
mwanamuziki ila ni mvuta Bangi aliye changanyikiwa anaye pigania haki za Ganja
(Ndumu).
Upuuzi huo haukufika popote kwani watu walizipokea vizuri tu
hizo Albam zake na zikapendwa sana .Adui zake hawakufurahi sana walipo msikia
akiimba na kutukuza Rasta,kutetea wakandamizwaji,kutetea Afrika ya kusini na
kupinga ubaguzi wa rangi .
Baada ya Peter na Bunny kuondoka 1974,Bob alianza kutafuta
wanamuziki wengine,akampata Al Andason Rasta ambaye alikaa sana Marekani(New
York),akampata Junior Marvin (Rasta bitoz),mtanashati na maridadi lakini mwenye
bidii na moyo usio kata tama.
Tena akapatikana Tyrone Downie kijana ambaye kwa muda mrefu
alikuwa anawahusudu sana The Wailers,wakajiunga pia wale I Threes,wanawake
weusi watatu waliokuwa na sauti nzuri ambao ni Rita Marley,Juddy Mowatt na
Marcia Griffiths walimsaidia Marly katika uimbaji.Juddy alitoa Albam ya Black
Woman.
Naye Rita Marley alionyesha umahiri wake kwa kuipua albam
iliyoitwa ‘Who Feels It Knows It’.Vilevile mwanadada Marcia alithibitisha
dhahiri kwamba yeye ni mwimbaji bora huenda kuwazidi hao wenzie Juddy na Rita,
alishirikiana vyema na Bob katika santuri yake iitwayo ‘Young Giftted and
Black’.
Kwa hakika walijituma sana katika kuboresha muziki wa Regae
na ndilo lililo kuwa kundi jipya lililounda nguvu ya The Wailers ambalo lilitoa
albam iliyowatia moyo ma-Rasta iliyoitwa ‘Natty Dread’ ambayo iliwajaza hamasa
vijana weusi wa Ulaya na Duniani kote.
Katika albam hiyo hakika kuna ujumbe uliokomaa
kimuziki,muziki ulionyooka,muziki wenye kilio na azma,muziki ulioonyesha
kujiamini na majivuno ya mtu ya mtu anaye jua afanyalo.unaonesha matatizo
kadhaa ya Rasta huko Jamaica ambako sheria kadhaa ziliwapiga vita.
Ukaonyesha shida na raha za maisha ya njini,akawataka watu
weusi wajiulize walikotoka na asili yao ya kitamaduni.Ulizungumzia mahaba,
mapinduzi umasikini,kutaharuki na kuazimia,uchungu na hasira.Itegee sikio kama
nyimbo ya No Woman No Cry,Natty Dread na Talking Blues’.
Ilifika wakati Fulani Bob na Wailers walivamiwa na
kushambuliwa kwa risasi,kila watu wengi walihisi kuwa walishambuliwa kwa sababu
ya mawazo yao hasa yaliyotokana na albam yao ya Natty Dread.
Jamaica ilikuwa ni nchi yenye upinzani mkali wa
kisiasa.Vyama viwili vikubwa vya kisiasa nchini humo wakati huo vilikuwa ni
Jamaica Labour Part(JPL) kilichoongozwa na Edward Seaga na chama cha
Peoples’National Part kilichoongozwa na Michael Manley.Ghasia za kisiasa
zilitokea mara kwa mara na C.I.A kama kawaida yake haikosi kuingilia kwa
maficho.
Mnamo mwaka 1976, The Wailers walifikiria wafanye onyesho
ambalo mada yake kubwa ingekuwa kuwaunganisha watu wa Jamaica,kuwasihi waache
uhasama na ghasia ,wafungue macho.Serikali ya Michael Manley ambayo ndiyo
ilikuwa madarakani ikakubali.Bob alihitaji kufanya onyesho la AMANI.
Jioni moja siku tatu kabla ya onyesho hilo,watu wenye
bunduki waliwashambulia The Wailers ambao walikuwa wanafanya mazoezi ya muziki
,ghafla wakasikia milio ya bunduki mlango ukafunguliwa huku mitutu ikitangulia
na kutoa milipuko kadhaa.Bob Marley na Rita Marley walijeruhiwa.

Claudie Massop ambaye alikuwa mfanya biashara mweusi ambaye
alikuwa mtu mashuhuri jijini Kingston alimsihi Bob arudi Jamaica.Massop
aliheshimiwa sana kwenye magheto na alichukuliwa na watu weusi kama kiongozi wa
magheto,kilichomuuma sana Claudie Massop ni kuona jinsi vijana walivyokuwa
wakipigana hovyo.
Walipigana na kuuana kwenye ushabiki wa vyama vya siasa
ambavyo vilikuwa havijawez kutatua matatizo yao.Massop aliona vijana hao
wanamalizana bure huku wanao faidi wakiwa ni wanasiasa.Massop alikutana na
wanamuziki wengi na kuongea nao.
Alikuwa na lengo kla Bob la kufanya onyesho kubwa jioni
ambalo kusudi lake lilikuwa kupinga uhasama uliokuwa umeenea katika
jamii.Massop alimchukulia Bob kama mdogo wake hata Bob alimchukulia Massop kama
kaka yake hivyo Bob asingeweza kukosa kwenye maonyesho yaliyoandaliwa na
Massop,walipendana sana na kuheshimiana.
Wanamuziki wa Jamaica kama vile Jacob Miller na Peter Tosh
walikuwepo.Lakini Bunny hakuhudhuria ,yalikuwa maonyesho makubwa yaliyofanikiwa
sana, yakaumeza moyo wa kila mtu.Ilikuwa ni vita ya wanmziki wa Gheto dhidi ya
uhasama wa siasa na hujuma za C.I.A.
Kilele cha sherehe hizo kilikuwa pale Bob aliposhikanishwa
mikono na Edward Seaga pamoja na Michael Manley ambao walikuwa ni viongozi wa
vyama vya siasa nchini Jamaica,vyama vya JPL na PNP.Wiki chache baadae baada ya
maonyesho hayo Massop akapigwa risasi na kufariki.
Hakuwa na kosa ,hakuwa na silaha ,polisi iliwachukua siku
nyingi sana kumpata muuaji aliyekuwa miongoni mwao wenyewe na jambo hilo
halikuwafurahisha watu wa Jamaica hata kidogo.Jitihada za Claudie zilikuwa
zimekubaliwa na kuheshimiwa na kila mtu,kuuawa kwake kuliwastua wajamaica
wengi.
Walijiuliza sana ni polisi gani aliye muua Brother Massop na
alikuwa ana mtumikia nani? Lakini yawezekana huyo askari ndiye aliye wajeruhi
Bob na Rita Marley walipokuwa wakifanya mazoezi na wenzao wa kundi la The
Wailers.
Kiundani zaidi Robert Nesta Marley alikuwa na kipaji pia
alipendwa na wengi ,si mashabiki tu bali kwa baadhi ya wanamziki wenzie ambao
ni mashuhuri katika ulimwengu wa muziki,walimkubali na kumheshimu kama vile
Jimmy Cliff.
Mnamo mwaka 1972 John Nash alipiga na hata kurekodi nyimbo
za Bob Marley ambazo ni Stir It UP,Guava Jelly na Nice Time,vile vile alimfanyia
mpango wa kurekodi regae on bload way katika studio za CBS.1974 mwanamziki
mashuhuri wa mtindo wa rock Eric Clatton,alipiga wimbo wa Marley ‘I’Shot The
Sherriff’.
Naye mwana mziki asiye ona Stevie Wonder katika uwanja wa
Taifa wa Kingston,walijumuika na Bob kutumbuiza .Mnamo mwaka 1980 Stevie
alirekodi ‘Master blaster’ iliyojulikana na kupendwa sana, msingi wa ‘Master
blaster’ ulikuwa wimbo wa Bob,Jamming Commoderes huko Madson Square Gardens,New
York.

Baadhi ya vijana kuwa Rasta ni ile hali ya kutokunyoa nywele
na badala yake kuzisuka na kuzisokota tu ili ziwe ndefu.Lakini Rasta haishii
hapo,Rasta ni utamaduni unaokumbatia mila ,desturi,din,itikadi na siasa.Kwa
ujumla wake utamaduni wa Rastafari ni ni utamaduni wa uasi.
Ni utamaduni uliochipuka katika jamii ya watu weusi na
machotara ambao daima walijikuta wakinyanyaswa na kudharauliwa.Hususani huko
Carriabean walianza kujiuliza wao ni akina nani hasa,asili yao ni wapi,
walitoka au walitokea wapi, kwa vipi, sasa wana hali gani na wafanye nini ili
maisha yao yawe bora na ya neema zaidi.
Katika imani za kirasta kuna vipengele vinavyo osha hamu ya
mtu mweusi (aliye nje ya Afrika) kurudi Afrika ikiwa mtu unanyanyaswa daima
mahala ulipo,ikiwa kila uendapo na kila upitapo unadhulumiwa,unatukanwa na
kubaguliwa,ikiwa watawala wanakufanya ujihisi hutakiwi,wazo la “wapi ulikotoka”
linajengeka kirahisi na kushika mizizi.
Unatamani ulikotoka kwa sababu unajenga hali Fulani ya uasi
na jeuri,unaitukuza asili yako.Hivyo ndivyo cheche ilivyojenga mawazo ya “going
back to my root”inachipuka katika jamii ya watu weusi wala si jamii ya weupe
huko Marekani.Mweupe hana anachokikosa.
Kweli,hana anachokikosa cha kumfanya atamani Ulaya alikotoka,amekuta
kuna ustawi huku kuliko huko kwenye asili yake.Alilie nini basi? Na ndio maana
hujawahi kumsikia kaburu akililia “Roots”(asili) yake.
Kimila na kidini,biblia ina nafasi kubwa katika maisha ya
Rasta kwa sheria ,Rasta anapaswa kusoma walau sura moja ya biblia kila
siku,wanaamini kuwa biblia inaupinga mfumo wa sasa duniani ambao ni wa
kinyonyaji,wanaouita mfumo wa BABY LONE.
Wanaamini kuwa yeyote anayefuata Biblia lazima awe mpigania
haki za mtu mweusi mpigania haki,usawa na uhuru na mpinga unyonyaji anaye
wakubali Rasta.Na ndio maana imani ya Rastafariani inamshambulia sana
Papa,kiongozi wa madhehebu ya Kikatoliki kwa kumwita mwongo ,mnafiki na ni nguzo ya mfumo wa Babylone.
Rasta wanaamini kuwa chimbuko lao na asili yao ni Afrika
hususa huko Sheshamane nchini Ethiopia,Rasta huwa na hamu kubwa sana ya kukanyaga
ardhi ya Sheshamane katika Bara la Afrika .Bob Marley alitembelea Sheshamane
mnamo mwaka 1978 ambako alikutana na Rasta wenzake.
Baada ya hapo alirudi wa sherehe za Uhuru wa
Zimbabwe.Vilevile Rasta wanacho chakula maalumu ambacho kinaitwa ITAL .Ni chakula
kitokanacho na mimea sio wanyama (vegetarian) na hakiungwi chumvi.
Rasta hatakiwi kukata nywele na akina mama hutakiwa
kuzifunika ili zisionekana hadharani,wanazo sheria na kanuni kali kuhusu
wanawake.Matharani mwanamke alie katika siku za hedhi hatakiwi kuguswa na
wanaume wala hatakiwi kupika chakula .
Imani ya Rastafara inaruhusu ,inaendekeza na kutukuza
uvutaji wa Bangi (Ganja).Rasta wanaamini kuwa ganja au bangi inasaidia
kusafisha akili,kutafakari na kuchambua mambo.Rasta hawaamini kama kuna kifo
,wanaamini kuwa mtu hafi bali anahama tu. ‘Mungu hawezi kukunyang’anya zawadi
kubwa ya uhai aliyokupa yeye mwenyewe’.Wanasema Rasta.
Katika imani ya Rastafara ,hayati mfalme Haile Selassie wa E
thiopia alikuwa Jah Rastafara ambaye kwa tofasiri ya moja kwa moja ni ‘Umbo’ la
Mungu Duniani (Picha ya Mungu Duniani).
Kijadi Rasta walikuwa ni watu wanaotengwa tengwa sana katika
jamii ya Jamaica.Hii inatokana na sheria zao ngumu,imani zao za kidini zilizo
wasuta wanafiki,mtazamo wao wa kisiasa ulio wapinga watawala wanasiasa na
mabepari pia wakoloni na tabia yao ya kuvuta Bangi waliitukuza mno.
Walipigania sana Ganja ihalalishwe,wamekuwa wakiitwa ‘wachafu’ ,watu wenye nyoyo nyeusi nk.Lakini
hapana anaye ukataa ukweli kuwa umeupanua na kuudumisha utamaduni wa waliowengi
nchini Jamaica.Wala hapana ukweli .
Sanaa hiyo ambayo bila shaka huko Caribean pia wanajivunia
na hakika wameifanya Jamaica ijulikane kote kote.Wameibeba Regae na kuisambaza
Dunia nzima .Na muhimu kuliko yote hapana anaye pinga ,awe adui au rafiki kuwa
Rasta wamekuwa wakipigania haki na uhuru pasipo kuchoka.
Pia alikuwepo Marcus Garvey ambaye ni mmoja wa Rastafari
waliokuza sana urasta na ndiye aliyependekeza sare inayotumika kwa
marastafari,yeye kuliko Rasta yeyote,ndiye aliye endeleza imani na hamu yao ya
kuirudia asili yao ama kimwili au kinadharia .
Marcus Garvey,mjamaica aliyezaliwa huko St.Ann’s ambako Bob
alizaliwa pia,alikuwa mtetezi mkubwa wa haki na usawa Duniani.Aliona kuwa mtu
mweusi anadharauliwa na kuonewa ,ananyanyaswa na kudhurumiwa ,Garvey
alimpigania sana mtu wa hali hiyo.
Aliuchukia ukoloni na alipigana kwa kila hali aliyoweza kuupinga
.Imani yake ilikuwa kwamba siku mojakama ingebidi, mtu mweusi angechukua silaha
na kujikomboa. Mwaka 1922 wakati wakoloni
wa kiingereza walipo wachinja ovyo waafrika huko Kenya.
Marcus garvey alimpelekea simu waziri mkuu wa uingereza simu
hiyo inakumbukwa sana.Katika simu hiyo ya tarehe 20 March 1922 Garvey,kwa niaba
ya watu weusi milioni mia nne.Garvey alikuwa kiongozi katika Universal Negro Improvement
Association.
Alimweleza waziri mkuu wa uingereza aliyeitwa David Lloyd
George kuwa serikali yake ilikuwa ikifanya vitendo vya kinyama huko Kenya
ambavyo kila mnegro alivilaani,wazalendo wa Kenya walikuwa wakiuawa hovyo
katika nchi yao wenyewe baada ya kudai haki zao kama binadamu.
‘Ni siasa gain hiyo? Alihoji Marcus Garvey katika simu hiyo.
‘Inazidi kuongeza lundo la dhuruma za kihistoria ambazo mtu mweusi ametendewa
naye siku moja atamka kikweli si kwa fimbo,rungu na mawe tu bali kwa silaha bora
za kileo’.Alieleza kwenye simu hiyo.
Haya.Mambo hayo! Ebu turudi tena upande wa Bob Marley. Japo
Bob alichukizwa na siasa nchini mwake na kuwalaani wanasiasa hasa kutokana na
matendo hayo,yeye mwenyewe alikuwa mwanasiasa mkubwa .Uchambuzi unaonyesha kuwa
alichokilaani Bob kilikuwa mfumo wa maisha ya uonevu.
Mfumo huo huo ulitawala si Jamaica tu,bali sehemu nyingi
duniani alisema anawachukia wanasiasa kwa sababu aliwaona wanapanda majukwaani
huku wakiwaongopea wananchi .Aliuchukia unyonyaji aliouchukia ukandamizaji wa
kiuchumi na kiutamaduni.
Bob aliuchukia sana ulaghai na ndio sababu ambazo zilimfanya
akorofishane na mameneja wengi wa studio kadhaa kwa sababu walitaka
kujinufaisha kupitia mgongo wa Bob hali ambayo ilimfanya atoe kibaop cha BAD
CARD kilichomsuta Coxsone Dodd na Don Taylon.
‘Don alikuwa mjanja sana …mi sipendi watu lagjhai,kwa nini
asiambiwe ukweli kuwa anataka vitu fulani kwangu’.Alisema Bob alipohojiwa
Bob hakuwa mpenda makuu ,alijali sana upatikanaji wa
maakuli,malazi,mavazi na usafiri.Bob,baada ya kupata hayo ambayo aliyaona ni ya
msingi,bila kutamba wala kujitangaza kitamaduni bila kumkomboa kiuchumi ni
kupiga ngoma msituni.
Sawa na kwamba ikiwa ni sehemu kubwa ya jamii ya kike
itaendelea kuwa chini ukilinganisha na wanaume,nafasi nyingi zaidi za kazi na
kujiendeleza kimaisha zitaendelea kuwatendea wanaume,ikiwa mfumo wa maisha
utaendelea kuwa ule wa mama ‘kuhudumiwa’ na baba.
Na baba ‘kuhudumia’, ni uwongo kusema usawa utapatikana na
hata kama kila mwanamke Duniani atahitimu shahada ya juu ya upigaji
kelele.Ukombozi wa mwanamke ,kimsingi ni suala la kiuchumi na sio hisia au mila
.Mfano ni huko Bara la Hindi mila za huko zinaruhusu wasichana ‘kuoa’.
Yaani wasichana wa huko ndio wanao paswa kughalamia shughuli
za harusi na ndiye anayetoa mahali, lakini kwa kuwa kiuchumi huyo mama anakuwa
chini ya mumewe na aghalabu kumtegemea mumewe, huko ‘kuoa’ kunaisha siku hiyo
hiyo.
Baada ya hapo mwanamke anaanza maisha ya wasi wasi kutokana
na kuendeshwa na bwana na wakweze.Kesi za wanawake walio na wanaume kujiua huko
ni nyingi kuliko sehemu yoyote duniani.
Na wala ukombozi haumanishi kuwa bwana ni mchimbaji mgodi na
bibi mpiga mashine wabadilishane haumaanishi kuwa mwanamke awe na msuli kama
mwanaume au mwanaume awe laini kama mwanamke, kama baadhi ya ‘watetezi’
wanavyodai bila kujijua.
Marley aliwapenda wanawake ,na hasa wanawake wa tabaka la
chini ,la wakulima na wafanya kazi wa kipato cha chini ,wanawake wa tabaka hili
aliwafahamu yeye zaidi,walikuwa hasa wanawake weusi.Ndio maana katika wimbo
wake wa No Woman No Cry tunaona wazi msimamo wa kisiasa wa Marley .Haimbi tu
kuhusu mwanamke yeyote,anaimbia mwanamke wa tabaka lake,mwanamke mweusi.Basi
anazungumzia habari za kuni,habari za ugali …hivi ni vitu anavyojua mama wa
tabaka la chini.

Ana wajaza hamasa na kuwaonyesha utamu wa maisha na
uhai.Anaonyesha mapenzi na heshima zake kwao,katika wimbo wa ‘No Woman No Cry’
na ‘John was a good man’zinaonyesha
heshima na mapenzi makubwa kwa wanawake.
Sihayo tu ambayo Bob aliiyafanya wakati wa uhai ,wake
alikuwa anajihusiha pia na michezo kama vile mpira miguu walipokuwa ziara ya
ulaya ,Bob alikuwa na Bendeji mguuni lakini hakuonyesha wasiwasi tokana na
jeraha alilolipata siku alipocheza mpira wa miguu.
Marley alipokuwa jukwaani alirukaruka jukwaani huku na huko
kama mtu asiye na jeraha mwilini pake alifanya mazoezi ya viungo kama kawaida
alikimbia kutoka studio na kuingia uwanjani kusakata kabumbu na mara kadhaa
alionekana akikimbia mchaka mchaka.
Uvumi wa kutisha
ukazuka kwamba mguu wa Bob Marley ulikuwa ukioza na ingebidi ukatwe.Baadae wakathibitisha
kuwa wasingehitaji kuukata ,Marley angeendelea kuwa yule yule mwenye mwili
mkakamavu,mcheshi ,mchangamfu,mchezaji ,mwanamuziki aliyeyumba na kutamba na
kurukaruka jukwaa zima kama kawaida yake siku zote.
Lakini ku8mbe kulikuwa na ukweli wa kutisha mno,kansa ya
Melanoma ambayo iliendelea kumla ikiyaharibu maini na mapafu yake hadi
alipoanguka wakati akikimbia mchaka mchaka (jogging) katika Central Park ,baada
ya kupiga katika The Comodores katika midson Sqare Gardens New York.
Bob Marley akalazwa katika hospitali iliyoitwa Sloan
Carttering Hospital ya jijini New York.Uchunguzi mkubwa ukafanywa na matokeo ya
uchunguzi huo yalithibitisha ukweli wa kusikitisha kuhusu afya ya Bob Marley.
Baada ya hapo Bob ‘akatoweka’.Uvumi ukaenea kuwa amekwenda zake
huko SHESHAMANE nchini Ethiopia,huko Sheshame ni sehemu maalumu kwaajili ya
wenye imani zqa Kirasta.Bado tunakumbuka kuwa Marley aliwahi kwenda huko mnamo mwaka 1978.
Lakini Marley hakuwa Ethiopia .Alikuwa amekwenda huko Bad
Wiese,Ujerumani Magharibi ambako alilazwa kwaajili ya matibabu katika hospitali
mashuhuri kwa magonjwa ya Kansa (Sun shine House Cancer Clinic) .Hapo alikuwapo
daktari mashuhuri wa maradhi kama ya Bob.
Daktari huyo alikuwa anaitwa Josef Issels ambaye alikuwa
akimpa matibabu ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na kumpatia mgonjwa vyakula
maalumu na matibabu ya mionzi.
Kwanza ,Bob alipofika hospitalini hapo tayari alikuwa na
uvimbe katika ubongo na alikuwa hawezi kutembea,alikuwa hoi bin taabani.Lakini
wiki chache tu baadae ,alikuwa anaweza si kusimama tu bali hata kutembea tembea
na kuonana na watu.
Lakini kansa ilimjia vibaya .Siku zilipita bila kupona
.Nafuu aliyowahi kuipata haikuwa ya kupona,wala haikuwa njia ya kuelekea kwenye
afya njema.
Hali ikazidi kuzorota,ukafikia wakati ambao yeye mwenyewe na
daktari wake wakatambua kuwa alikuwa mtu wa kutoka.Alipotambua kuwa mauti yake
yamekaribia ,Bob akaamua kufunga safari ya kurejea Jamaica ili akafie huko.
Maskini ,kinyume na alivyopanga Bob,ili afike Jamaica akiwa
hai ,badala yake alifika huko akiwa ni marehemu kwani alifariki akiwa katika
hospitali moja ya Florida tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1981.
Itakumbukwa kwamba katika uhai wake Bob,viongozi wa mfumo wa
Babylone daima walipingana na Marley.Walimpiga vita na kuinunia Regae.Wakati akiwa
taabani kitandani walimtambua,ni wakati
huu ukweli ulipoibuka na kushinda.
Wakamtambua rasmi ,wakampatia nishani ya heshima ya Order of
Merit .Hii ilikuwa kabla ya kifo chake,ilikuwa mwezi machi 1981.Kabla ya
kufariki Marley alikuwa amekubaliwa katika kanisa Orthodox Church la
Ethiopia-The Ethiopian Orthodeox Church kasha akapewa jina la Berhane Sellasie.
Mwili wa Bob Marley ukapelekwa Kingstone kwa ndege kutoka
Miami.Ibada ya kumuaga ilfanyika katika lugha nne ambazo ni lugha ya taifa ya
Ethiopia iitwayo Amharic na Geez ambayo ni lugha ya zamani ya kidini huko
Ethiopia.
Zingine zilikuwa ni lugha za kiafrika na kiingereza,viongozi
wa kisiasa akiwemo waziri mkuu wa Jamaica Edward Seaga walitoa heshima zao
.Wanasiasa ni watu ambao Bob katika uhai wake alikuwa amewakemea na kuwasuta
mara nyingi sana.
Marehemu akapelekwa katika medani ya taifa (National Arena)
sehemu kubwa ambayo awali iljengwa kwaajili ya michezo ya Common Wealth,hapo
maelfu ya watu walikusanyika kumuaga shujaa wao,polisi walijaa tele wenye mfumo
wa ki-babylone ambao hawakupata kuwa marafiki wa Bob Marley.
Agharabu polisi hao waliwatawanya vijana waliojawa hisia na
uchungu kwa gesi ya machozi.Haikuwa rahisi kupata utulivu na nidhamu waliotaka
polisi,nao kama kawaida ya askari wa mfumo huo wakatumia nguvu.
Muziki wa Bob ukasikika kwenye kanda huku watu wakipita
pembeni mwa jeneza lililohifadhi mwili wa marehemu Bob wakitoa heshima zao za
mwisho kwa mwanamuziki huyo mpiganaji wa ghetto.Halafu The Wailers wakapiga
muziki wa kidini na Microphone ilishikwa na Bibi Cedeller Booker.
Bibi huyo ndiye mama mzazi wa Bob aliimba kwa sauti
iliyotetemeka iliyopanda na kushuka .Ziggy na Steve ambao ni watoto wa Bob
wakaamka jukwaani,wakaimba nyimbo walizo kuwa wamefunzwa na baba yao, ‘1 Threes
walikuwapo pia ,waliimba kwa simanzi.
Halafu safari ikaanza kuelekea Nine Miles kijijini aliko
zaliwa Marley katika jimbo la Ann’s.Peter Tosh na Bunny Wailer hawakuhudhuria
,Bunny ni mtu asiye amini sherehe za mazishi na ukweli ni kwamba rasta
hawakichukulii kifo kama ilivyo jamii isiyo ya kirasta.
Bunny ni mtu anaye ping asana maombolezo ya msiba ,haileweki
kwa nini Peter hakuhudhuria lakini Don Taylor ambaye alikuwa meneja wa The
Wailers hatimaye kukorofishana nao alihudhuria na alifanya kazi kubwa ya
kuifariji jamii ya marehemu tena akatoa na msaada aliouweza.
Rita Marley walipofika huko Nine Miles alisema ‘hapa ndipo
mahali nilipopitishia miaka sita nikiwa na Bob na hapa ndipo nilipo zaa mtoo
wetu wa kwanza aitwaye Ziggy.
Barabara kuu itokayo mjini Kngstone ilikuwa ikiitwa
Washington Boulevard ndiyo iliyotumika kuusafirisha mwili wa hayati Robert
Nesta Marley,ilikuwa haipitiki,watu walisongamana,msululu wa magari ulikuwa na
urefu wa kilomita kadhaa.
Safari ikaenda taratibu huku vipaza sauti vilivyokuwa kwenye
magari vikitoa sauti za muziki wa Bob Marley.Barabara hiyo sasa imepewa rasmi
jina la Bob Marley Boulevard badala ya Washington Boulevard.
Huko kijijini kwao alikozikwa , kaburi lilipewa nafasi nzuri
na mahali pa pekee ambapo katika uhai wake Marley alipendelea kuketi na Rita
huku wakijadili mambo mbali mbali usiku huku wakisikiliza muziki na kuangazwa
na mbaramwezi au wakizitazama nyota.
Takribani mita mia moja kutoka eneo hilo,ndipo alipozaliwa Bibi
Cedeller Booker.Shujaa Robert Nesta Marley(Barhane Sellesie) mwasisi wa
soul,The Trench Town Experience,mwana wa Ragae vilevile mpiganaji kutoka Gheto
akapumzishwa.
MWISHO. Historia hii pia inapatikana kwenye mtandao wa www.mamboyakwetu.blogspot.com
(JICHO LANGU BLOGU) . Kwa mawasiliano zaidi 0762 876 892, E-mail:
sjonasm@yahoo.com
No comments:
Post a Comment