Wednesday, June 27, 2012
KIWANDA CHA KUOKA MIKATE MBEYA CHA FAMILY LOAF CHA TISHIA AFYA ZA WANANCHI
WANANCHI wa kata za Itiji na Mabatini katika Halmashauri ya jiji la Mbeya hivi karibu wamekitolea lawama kiwanda cha kuoka mikate cha Family Loaf kutokana na kitendo cha kiwanda hicho kutupa taka kwenye mto wa Mabatini ambao unatumiwa na wananchi hao.
Kwa mujibu wa wananchi wa kata hizo,kiwanda hicho kimekuwa kikitupa taka ndani ya mto huo ambao hutumika kwa shughuli za kibinadamu na mifugo hata kusababisha wananchi kupata hofu kwa maelezo kuwa taka hizo zinaweza kuwa na madhara kutokana na kemikali zilizomo ndani ya taka hizo.
Mmoja wa wananchi waliofanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti katika maeneo ya kata hizo,walisema kwamba wanaamini kuwa taka hizo ni lazima zitakuwa na kemikali zinazochanganywa katika maandalizi ya kuoka bidhaa hiyo.
Angel Davis mkazi wa Itiji alisema kuwa ,mbali ya kuwepo hofu ya hizo kemikali pia kitendo hicho ni cha uchafuzi mazingira na kukiuka haki za binadamu na viumbe vingine vinavyo tumia maji ya mto huo.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Omary Abdalah alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kiwandani hapo alikiri kuwa eneo la Mabatini ni eneo ambalo limekuwa likitumiwa na kiwanda kuhifadhi taka baada ya watu wa jiji kushindwa kusomba taka mbali ya kutozwa ushuru 50,000/= kwa mwezi wa idara ya afya.
Hata hivyo alisema kwamba hana uhakika kama taka hizo zinatupwa ndani ya mto kwa maelezo kuwa mtu anaye husika na utupaji taka aliagizwa kutupa kwenye Guba la taka lililopo Mabatini wala si vinginevyo.
Naye Isaya Amir ambaye anahusika na utupaji taka alikiri kutupa taka ndani ya mto huo huku akieleza kuwa hajui kama taka hizo zinaweza kuwa na madhara badala yake alisema anafanya hivyo ili maji kusomba taka na kuondokana na mlundikano wa taka kwenye eneo hilo.
Hata hivyo,Meneja uzalishaji alipoulizwa kuhusu ubora wa bidhaa ya kiwanda hicho alishindwa kutoa maelezo ya kina huku akisema mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) walifika kiwandani hapo kuchukua bidhaa inayozalishwa hapokiwandani kwa uchunguzi lakini hadi leo hawajapatiwa majibu lakini wakati huo mikate yake haina hata nembo ya TBS.
Mkurugenzi wa jiji la Mbeya Idd Jumanne alipoulizwa kuhusiana na
uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho ,alishindwa kukiona kwenye mtao wa Kompyuta hivyo kueleza kwamba kiwanda hicho kinaendesha shughuli kinyemela ambapo ni makosa kisheria.
Alisema kwamba,ili kubaini kinachoendelea kiwandani hapo aliahidi kupeleka wataalamu wake wa mamlaka ya chakula na dawa huku akisisitiza kuwa ana wasiwasi hata ushuru wa kusomba taka hatoi kwa maelezo kuwa jiji hupenya kwa wadau wote wa taka na kama gari halifiki ni wajibu wake kupiga simu ili kupatiwa huduma badala ya kuchafua mto
Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha mikate zaidi ya 300 kwa siku na kina zaidi ya miaka minne ,hivyo basi, kwa kipindi hicho chote kiwanda kimekuwa kikisambaza bidhaa hiyo na kuwalisha wananchi bila kuwa na leseni ya mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) wala leseni ya viwango bora vya (TBS) kwa mujibu wa sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment