Wednesday, September 12, 2012

WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA WATOA TAMKO KUHUSU KIFO CHA MWANDISHI MWANGOSI


NaSteve Jonas, Mbeya

WAANDISHI wa Habari Mkoani Mbeya wamemtaka Rais wa Jamuhuri ya Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kusitisha mpango wa kuunda tume ya uchunguzi wa kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chaneli ten Daudi Mwangosi (40).


Akitoa tamko la wanahabari wa mkoa wa Mbeya mara baada ya mandamano ya amani yaliyofanyika jijini hapa leo,  Mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari Mkoani hapa (MPC) Christopher Nyenyembe  amesema kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo ni upotevu wa fedha za walipa kodi.


Nyenyembe amesema tukio la mauaji ya Daudi Mwangosi yanaeleweka na hayana haja ya kuunda tume kwa kuwa ushahidi wa picha za tukio lote zinaonyesha ukweli wa nani aliyehusika na mauaji hayo hivyo amemtaka Rais Kikwete kuachana na mpango wa kuunda tume ya uchunguzi.


Amesema watanzania wanahitaji huduma nyingi za maendeleo lakini fedha nyingi zimekuwa zikitumika kwa masuala yasiyo na tija kwa wanannchi kama ilivyo hivi sasa ambapo serikali inaunda tume ya kuchunguza mauaji ya mwandishi.


Mwanyekiti huyo amesema kuwa, tamko la waandishi wa mkoa wa Mbeya ni kuungana na waandishi wengine nchini kote kutofanya kazi za  jeshi la Polisi hadi pale watakapopata taarifa za ukweli juu ya mauaji ya marehemu Mwangosi.


Aidha, tamko hilo lilimewataka Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dr. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa jeshi la Polisi nchini( IGP) Said na Mkuu wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda wajiuzuru nafasi zao.


Nyenyembe alisema kwamba viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao kwa   raia wao ambapo mauaji hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwa raia wasio huku matukio hayo yakiendelea kufumbiwa macho bila kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika jambo ambalo  limekuwa likitia shaka kwa wananchi.

Naye mwandishi ambaye hakutaka kutaja jina lake ambaye pia ni mjumbe wa chama cha wandishi wa mkoa wa mbeya, alisema tatizo lililopo katika jeshi la polisi ni kuwepo kwa vijana wasio na maadili hasa wale ambao ni watoto na wengine wanaopita njia za panya kupitia viongozi wa jeshi hilo.

Mjumbe huyo amesema kuwa, nidhamu ya jeshi la polisi imeshuka kupita kiasi kutokana na kuingizwa kwa ndugu wengu ndani ya jeshi hilo, hivyo kulifanya jeshi hilo kama ni la kifamilia ambapo hivi sasa linashindwa kuwawajibisha wanaofanya vitendo vya kikatiri.

Amesema wananchi wengi wamekuwa wakikimbilia kwa wanahabari kusaidiwa badala ya kukimbilia kwa jeshi la polisi kutokana na kukatishwa tamaa na vitendo vya kikatiri toka kwa baadhi ya askali polisi kwa Raia hao ambao kwa kawaida ni usalama wa raia na mali zake jambo ambalo kwa sasa ni kinyume.

Mwangosi aliuawa na Polisi kwa bomu la machozi mnamo siku ya Jumapili alasiri, Septemba 2 mwaka huu akiwa kwenye majukumu yake ya kazi katika mkutano wa chama cha kisiasa (CHADEMA) uliofanyika siku hiyo kwenye kijiji cha Nyololo mkoani Iringa na kuzikwa kijijini kwao Busoke ,Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Mwangosi katika uhai wake alilitumikia Taifa na jamii kwa ujumla kupitia vyombo mbali mbali vya habari hadi mauti yanamfika alikuwa mfanyakazi wa kituo cha Televisheni cha Chanel Ten akikiwakilisha kituo hicho kutoka mkoani Iringa.






No comments:

Post a Comment