Na Anna Livifile, Mbeya
WAFANYABIASHARA wa Soko la Sido jijini hapa wamelitupia
lawama uongozi wa jiji la Mbeya wakidai hawanufaiki na mapato ya soko kwa
kufuatia mapungufu yaliyopo sokoni hapo.
Kwa mujibu wa katibu wa soko hilo Bw. Alanus Ngogo wafanyabiashara
wanatozwa ushuru kila siku sh. 300 kwa kila mmoja kati ya wafanyabiashara 1114
lakini mbali ya Halmashauri ya jiji kukusanya kiasisi kikubwa cha fedha soko
hilo limekuwa likikabiliwa na miundo mbinu finyu.
Bw. Ngogo aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyopo sokoni hapo
kuwa ni kukosekana kwa umeme, taka kutozolewa kwa wakati, barabara za kuingia
na kutoka kwa magari yanayopeleka mahitaji ya wafanyabiashara na mifereji ya
kupitishia maji machafu.
Alisema tatizo lingine ambalo limekuwa kero kwa watumiaji wa
soko hilo ni kukosekana kwa vyoo ambapo wanalazimika kutumia vyoo vya kulipia
vinavyo milikiwa na watu binafsi kitendo ambacho kimeibua manung’uniko na
kuhoji ni vipi jiji limeshindwa kuweka huduma hizo ikilinganishwa na ukusanyaji
wa mapato.
Vilevile alishauri kuwa kuwepo na sehemu maalumu kwa ajili
ya matangazo yatakayoonesha kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa zinazopatikana
sokoni hapo kinyume na sasa ambapo hakuna utaratibu huo na kuwepo mkanganyiko
kati ya wafanyabiashara na wanunuzi.
Katibu huyo alilitaka jiji lilitambulishe soko kwenye
taasisi mbalimbali nchini ili wafanyabiashara waweze kupata mikopo itakayo kuza
mitaji na kipato chao pia kuliwezesha jiji kuongeza vyanzo vya mapato
Katika hatua nyingine kiongozi huyo alisema kuwa wafanyabiashara
wanataka kusikia kauli ya jiji itakayowatambulisha kuahamia soko jipya lililopo
Mwanjelwa jijini hapa kwa maelezo kuwa wamesubiri kwa muda mrefu.
Soko hilo
lipo katika hatua za mwisho za ujenzi tangu lilipoungua zaidi ya miaka mnne
iliyopita hali iliyo sababisha wafanyabiashara hao kuhamia kwenye soko la Sido
kwa muda ili kupiha shughuli za ujenzi wa soko jipya.
Mwisho………….