Wednesday, July 3, 2013

CHUTCU KINATARAJIA KUPATA MKOPO WA ZAIDI YA MIL.1O

Na Steve Jonas, Chunya

CHAMA   kinachosimamia zao la Tumbaku Wilayani Chunya (CHUTCU) kinatarajia kupata mkopo wa zaidi ya Dola 10 Mil. za kimarekani  kwa ajili ya kununua na kusambaza pembejeo katika msimu wa 2013/2014.

Hayo yalisomwa hivi karibuni kwenye Risala ya Chama hicho wakati wa sherehe za uzinduzi  soko la Tumbaku zilizofanyika Lupatingatinga  Wilayani humo katika mkoa wa Mbeya.

Risala hiyo ilisema CHUTCU katika msimu wa 2013/2014 kinategemea kupata mkopo wa dola 13,402,962.08 kutoka kwenye Benki CRDB wakati NMB itatoa dola 4,514,785.15 mikopo ambayo itatumika kujengea Mabani ya kisasa na majiko yake, kusogeza kuni, kuchambulia Tumbaku, ujenzi wa maghala mapya kwenye vyama  shiriki vilivyoomba.

Zilitajwa shughuli zingine kuwa ni ununuzi wa pembejeo na kusambaza kwenye vyama vya msingi vinavyounda CHUTCU ili kuwafikia wakulima kwa urahisi.

Ilielezwa kwamba zao hilo msimu huu litauzwa kwa wastani wa Dola 2.6 kwa kilo na bei ya juu itauzwa dola 3.299 kila kilo moja badala ya dola 1.91bei iliyotumika msimu uliopita.

 Taarifa hiyo ilisema mavuno ya tumbaku msimu wa 2012/2013 hayatafikia malengo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyojitokeza kwa mvua kunyesha chini ya kiwango na malengo yalikuwa  ni kupata kilo 12,500,000.

Ilifafanuliwa kuwa katika msimu wa 2013/2014 uzalishaji wa tumbaku utaongezeka hadi kufikia 13,055,000 kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kufuatia Serikali kuongeza mnunuzi mwingine kutoka Jamhuri ya watu wa China.

Uzalishaji wa tumbaku Wilayani humo msimu wa 2009/2010 ulifikia kilo 377,579, 2010/2011 kilo 628,606, 2011/2012 uzalishaji ulishuka hadi kilo 354,276 wakati  msimu wa 2012/2013 kwa mujibu wa tathimini ya zao (Crop Survey) zitavunwa kilo 578,989.

Kwa mujibu wa Risala hiyo iliyosomwa na Meneja Mkuu aliyefahamika kwa jina la Bw. Kassia, Chama hicho kimekuwa kikihimiza vyama vya msingi na wakulima ili misitu isiharibiwe kwa matumizi ya kilimo hicho ambapo hadi kufikia 2012/2013 jitihada hizo zimefanikiwa kupanda miti2,227,759 kwenye maeneo mbalimbali Wilayani humo.

Alisema mafanikio hayo yamechangiwa pia na Makampuni mawili ya Tanzania Leaf Tobaco Company Ltd ambayo ina Vyama vya msingi  nane na Premeium Active Tanzania Ltd ambayo ina vyama 13, Makampuni hayo ni wanunuzi wa zao hilo.

No comments:

Post a Comment