Saturday, July 13, 2013

WAFANYABIASHARA WAILAUMU JIJI LA MBEYA



Na Anna Livifile, Mbeya

WAFANYABIASHARA wa Soko la Sido jijini hapa wamelitupia lawama uongozi wa jiji la Mbeya wakidai hawanufaiki na mapato ya soko kwa kufuatia mapungufu yaliyopo sokoni hapo.

Kwa mujibu wa katibu wa soko hilo Bw. Alanus Ngogo wafanyabiashara wanatozwa ushuru kila siku sh. 300 kwa kila mmoja kati ya wafanyabiashara 1114 lakini mbali ya Halmashauri ya jiji kukusanya kiasisi kikubwa cha fedha soko hilo limekuwa likikabiliwa na miundo mbinu finyu.

Bw. Ngogo aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyopo sokoni hapo kuwa ni kukosekana kwa umeme, taka kutozolewa kwa wakati, barabara za kuingia na kutoka kwa magari yanayopeleka mahitaji ya wafanyabiashara na mifereji ya kupitishia maji machafu.

Alisema tatizo lingine ambalo limekuwa kero kwa watumiaji wa soko hilo ni kukosekana kwa vyoo ambapo wanalazimika kutumia vyoo vya kulipia vinavyo milikiwa na watu binafsi kitendo ambacho kimeibua manung’uniko na kuhoji ni vipi jiji limeshindwa kuweka huduma hizo ikilinganishwa na ukusanyaji wa mapato.

Vilevile alishauri kuwa kuwepo na sehemu maalumu kwa ajili ya matangazo yatakayoonesha kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa zinazopatikana sokoni hapo kinyume na sasa ambapo hakuna utaratibu huo na kuwepo mkanganyiko kati ya wafanyabiashara na wanunuzi.

Katibu huyo alilitaka jiji lilitambulishe soko kwenye taasisi mbalimbali nchini ili wafanyabiashara waweze kupata mikopo itakayo kuza mitaji na kipato chao pia kuliwezesha jiji kuongeza vyanzo vya mapato

Katika hatua nyingine kiongozi huyo alisema kuwa wafanyabiashara wanataka kusikia kauli ya jiji itakayowatambulisha kuahamia soko jipya lililopo Mwanjelwa jijini hapa kwa maelezo kuwa wamesubiri kwa muda mrefu.

Soko hilo lipo katika hatua za mwisho za ujenzi tangu lilipoungua zaidi ya miaka mnne iliyopita hali iliyo sababisha wafanyabiashara hao kuhamia kwenye soko la Sido kwa muda ili kupiha shughuli za ujenzi wa soko jipya.

Mwisho………….


No comments:

Post a Comment