NaSteve Jonas, Mbeya
WAANDISHI wa Habari Mkoani Mbeya
wamemtaka Rais wa Jamuhuri ya Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kusitisha mpango
wa kuunda tume ya uchunguzi wa kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa
kituo cha Chaneli ten Daudi Mwangosi (40).
Akitoa tamko la wanahabari wa
mkoa wa Mbeya mara baada ya mandamano ya amani yaliyofanyika jijini hapa leo, Mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari
Mkoani hapa (MPC) Christopher Nyenyembe
amesema kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo ni upotevu wa fedha za
walipa kodi.
Nyenyembe amesema tukio la mauaji
ya Daudi Mwangosi yanaeleweka na hayana haja ya kuunda tume kwa kuwa ushahidi
wa picha za tukio lote zinaonyesha ukweli wa nani aliyehusika na mauaji hayo
hivyo amemtaka Rais Kikwete kuachana na mpango wa kuunda tume ya uchunguzi.
Amesema watanzania wanahitaji
huduma nyingi za maendeleo lakini fedha nyingi zimekuwa zikitumika kwa masuala
yasiyo na tija kwa wanannchi kama ilivyo hivi sasa ambapo serikali inaunda tume
ya kuchunguza mauaji ya mwandishi.
Mwanyekiti huyo amesema kuwa,
tamko la waandishi wa mkoa wa Mbeya ni kuungana na waandishi wengine nchini
kote kutofanya kazi za jeshi la Polisi
hadi pale watakapopata taarifa za ukweli juu ya mauaji ya marehemu Mwangosi.
Aidha, tamko hilo lilimewataka Waziri
wa mambo ya ndani ya nchi Dr. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa jeshi la Polisi nchini(
IGP) Said na Mkuu wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda wajiuzuru nafasi
zao.
Nyenyembe alisema kwamba viongozi
hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao kwa raia
wao ambapo mauaji hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwa raia wasio huku
matukio hayo yakiendelea kufumbiwa macho bila kuchukuliwa hatua za kisheria kwa
wahusika jambo ambalo limekuwa likitia
shaka kwa wananchi.
Naye mwandishi ambaye hakutaka
kutaja jina lake ambaye pia ni mjumbe wa chama cha wandishi wa mkoa wa mbeya, alisema
tatizo lililopo katika jeshi la polisi ni kuwepo kwa vijana wasio na maadili
hasa wale ambao ni watoto na wengine wanaopita njia za panya kupitia viongozi
wa jeshi hilo.
Mjumbe huyo amesema kuwa, nidhamu
ya jeshi la polisi imeshuka kupita kiasi kutokana na kuingizwa kwa ndugu wengu
ndani ya jeshi hilo, hivyo kulifanya jeshi hilo kama ni la kifamilia ambapo
hivi sasa linashindwa kuwawajibisha wanaofanya vitendo vya kikatiri.
Amesema wananchi wengi wamekuwa
wakikimbilia kwa wanahabari kusaidiwa badala ya kukimbilia kwa jeshi la polisi
kutokana na kukatishwa tamaa na vitendo vya kikatiri toka kwa baadhi ya askali
polisi kwa Raia hao ambao kwa kawaida ni usalama wa raia na mali zake jambo
ambalo kwa sasa ni kinyume.
Mwangosi aliuawa na Polisi kwa
bomu la machozi mnamo siku ya Jumapili alasiri, Septemba 2 mwaka huu akiwa
kwenye majukumu yake ya kazi katika mkutano wa chama cha kisiasa (CHADEMA)
uliofanyika siku hiyo kwenye kijiji cha Nyololo mkoani Iringa na kuzikwa
kijijini kwao Busoke ,Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Mwangosi katika uhai wake
alilitumikia Taifa na jamii kwa ujumla kupitia vyombo mbali mbali vya habari
hadi mauti yanamfika alikuwa mfanyakazi wa kituo cha Televisheni cha Chanel Ten
akikiwakilisha kituo hicho kutoka mkoani Iringa.