Tuesday, February 5, 2013

RADI YAUA WATU WATANO MBEYA





WATU watano wamefariki dunia mkoani Mbeya kwa kupigwa radi katika matukio matatu tofauti likiwemo lililoua ndugu watatu wa familia moja. 
 
Wanandugu hao watatu wakazi wa kata ya Nyimbili Wilayani Mbozi wamefikwa na mauti leo majira ya saa saba mchana wakati mvua kubwa iliyoambatana na radi za mara kwa mara ikiendelea kunyesha wakiwa nyumbani. 

Afisa mtendaji wa kata ya Nyimbili Lingtone Nzowa amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Jerumana Halinga (35), David Halinga (5) na Kumi Halinga(3) na mtoto wa miezi tisa ambaye hakufahamika mara moja jina lake, alijeruhiwa katika ajali hiyo. 
 
 Tukio la pili limetokea katika kijiji cha Magurula kata ya Utengule Usangu Wilayani Mbarali ambapo radi iliyotokana na mvua kubwa imempiga Kasim Sagutangu na kusababisha kifo chake, Diwani wa kata hiyo Juntwa Mwalyaje amesema mvua hiyo imenyesha Februari 3 majira ya saa nane za mchana.
Tukio la tatu lilitokea Februari 3 katika kijiji cha Mbagala Kata ya Ilembo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mwanamke Kotanida Petro alifariki dunia baada ya kupigwa na radi akiwa shambani kwake.
 
 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa matukio hayo ya vifo vya watu watano vilivyotokana na radi.

No comments:

Post a Comment