KITUO
cha daladala kilichopo eneo la kituo cha polisi Mbalizi kwenye Halmashauri ya Wilaya
ya Mbeya kimekuwa tishio kwa wasafiri wanaopandia
eneo hilo baada ya kugeuka kuwa genge la wezi wa mifukoni.
Genge hilo la wezi wa
mifukoni limeendelea kujiimarisha eneo hilo bila kuchukuliwa hatua
yeyote ambapo udhibiti wa awali ulikuwa ukifanywa na baadhi ya
makondakta na madereva kwa kuwakataza kupanda kwenye magari yao lakini
udhibiti huo umeshindikana.
Wezi hao wamebuni mbinu
mmbadala ya kufanikisha uhalifu huo kwa kushika madaftari makubwa huku
wakipanda gari ambazo abiria huwa wakisimama kisha kuanza kufanya kazi
zao za wizi wa simu za kiganjani na fedha kwa abiria.
Baada ya kufanikisha
wizi huo hushuka katika kituo kinachofuata kijulikanacho kwa jina la
Nsungwe au Stendi ya Tarafani kisha kurejea eneo la kituo cha Polisi.
Hali hiyo imedumu kwa
muda mrefu sasa kukiwa hakuna jitihada za kudhibiti
kundi hilo la uhalifu ambalo limekuwa likiogopa kuweka maskani yake
katika stendi ya Mbalizi kutokana na wapiga debe wa stendi hiyo kuwa na
umoja wao na kupiga vita vitendo vya wizi.
WANANCHI wa kata za Itiji na Mabatini katika Halmashauri ya jiji la Mbeya hivi karibu wamekitolea lawama kiwanda cha kuoka mikate cha Family Loaf kutokana na kitendo cha kiwanda hicho kutupa taka kwenye mto wa Mabatini ambao unatumiwa na wananchi hao.
Kwa mujibu wa wananchi wa kata hizo,kiwanda hicho kimekuwa kikitupa taka ndani ya mto huo ambao hutumika kwa shughuli za kibinadamu na mifugo hata kusababisha wananchi kupata hofu kwa maelezo kuwa taka hizo zinaweza kuwa na madhara kutokana na kemikali zilizomo ndani ya taka hizo.
Mmoja wa wananchi waliofanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti katika maeneo ya kata hizo,walisema kwamba wanaamini kuwa taka hizo ni lazima zitakuwa na kemikali zinazochanganywa katika maandalizi ya kuoka bidhaa hiyo.
Angel Davis mkazi wa Itiji alisema kuwa ,mbali ya kuwepo hofu ya hizo kemikali pia kitendo hicho ni cha uchafuzi mazingira na kukiuka haki za binadamu na viumbe vingine vinavyo tumia maji ya mto huo.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Omary Abdalah alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kiwandani hapo alikiri kuwa eneo la Mabatini ni eneo ambalo limekuwa likitumiwa na kiwanda kuhifadhi taka baada ya watu wa jiji kushindwa kusomba taka mbali ya kutozwa ushuru 50,000/= kwa mwezi wa idara ya afya.
Hata hivyo alisema kwamba hana uhakika kama taka hizo zinatupwa ndani ya mto kwa maelezo kuwa mtu anaye husika na utupaji taka aliagizwa kutupa kwenye Guba la taka lililopo Mabatini wala si vinginevyo.
Naye Isaya Amir ambaye anahusika na utupaji taka alikiri kutupa taka ndani ya mto huo huku akieleza kuwa hajui kama taka hizo zinaweza kuwa na madhara badala yake alisema anafanya hivyo ili maji kusomba taka na kuondokana na mlundikano wa taka kwenye eneo hilo.
Hata hivyo,Meneja uzalishaji alipoulizwa kuhusu ubora wa bidhaa ya kiwanda hicho alishindwa kutoa maelezo ya kina huku akisema mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) walifika kiwandani hapo kuchukua bidhaa inayozalishwa hapokiwandani kwa uchunguzi lakini hadi leo hawajapatiwa majibu lakini wakati huo mikate yake haina hata nembo ya TBS.
Mkurugenzi wa jiji la Mbeya Idd Jumanne alipoulizwa kuhusiana na
uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho ,alishindwa kukiona kwenye mtao wa Kompyuta hivyo kueleza kwamba kiwanda hicho kinaendesha shughuli kinyemela ambapo ni makosa kisheria.
Alisema kwamba,ili kubaini kinachoendelea kiwandani hapo aliahidi kupeleka wataalamu wake wa mamlaka ya chakula na dawa huku akisisitiza kuwa ana wasiwasi hata ushuru wa kusomba taka hatoi kwa maelezo kuwa jiji hupenya kwa wadau wote wa taka na kama gari halifiki ni wajibu wake kupiga simu ili kupatiwa huduma badala ya kuchafua mto
Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha mikate zaidi ya 300 kwa siku na kina zaidi ya miaka minne ,hivyo basi, kwa kipindi hicho chote kiwanda kimekuwa kikisambaza bidhaa hiyo na kuwalisha wananchi bila kuwa na leseni ya mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) wala leseni ya viwango bora vya (TBS) kwa mujibu wa sheria.
MWALIMU mstaafu wa
elimu ya msingi mkoani Mbeya Bw.Paul Lyambwa Mbamba (74) mkazi wa kijiji cha
Lusungu katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mbeya, hivi karibuni alikabidhiwa
kadi ya uanachama wa Chadema baada ya kurudisha kadi ya CCM chama alichokitumikia tangu mwaka 1977
Bw.Mbamba ameuambia mtandao wa www.mamboyakwetu.blogspot.commjini hapa hivi karibuni kuwa ameamua
kujiunga na CHADEMA baada ya kuchoshwa na CCM kwa vitendo vya unyanyasaji ambavyo amevivumilia kwa kipindi kirefu wakati
akikitumikia Chama hicho.
Katibu wa CHADEMA tawi la Lusungo Bw.Gabriel Songa alithibitisha kuwa ,Bw.Mbamba alirudisha kadi yenye Na.155861 ya CCM ambayo
alikuwa ameilipia ada kwa mara ya mwisho
mwezi Machi 25 mwaka 2010 kwenye tawi la Kasale kijiji cha Idiga kilichopo
kwenye kata ya Bonde la Songwe jimbo la Mbeya Vijijini.
Bw.Songa alisema kuwa,Bw.Mbamba ambaye ana
taaluma ya ualimu baada ya kukabidhi kadi hiyo ya CCM alikabidhiwa kadi ya
CHADEMA yenye Na.CDM 0443364 mnamo Mei 26 mwaka huu na kuthibitisha kwamba
Bw.Mbamba tayari amekuwa mwanachama hai wa Chadema
Katika mahojiano mafupi na Mtandao huu Mbamba alisema kuwa
ndani ya CCM kuna baadhi ya watu wanajifanya miungu watu ambapo wanataka
kunyenyekewa na kukiendesha chama katika misingi ya urafiki na undugu kitendo
ambacho kinasababisha wananchi kuongozwa na watu ambao si chaguo lao.
Mwalimu huyo alisema kwamba ,kwenye uanachama wake ndani ya
CCM aliwahi kugombea nafasi ya udiwani katika kata hiyo kwenye uchaguzi mkuu
uliopita ambapo alisema kuwa alifanyiwa kitu mbaya vikiwemo vitendo vya
kutishia uhai wake ambavyo vilikuwa vikifanywa na wanachama wa CCM hata kusababisha kutupwa katika uchaguzi huo.
Aliongeza kuwa ndani ya CCM hakuna Demokrasia ya kweli bali
imejaa unafiki na vitendo vya ubabe ambavyo havina tija katika shughuli za
maendeleo ya watanzania.
DIWANI wa kata ya Bonde la Songwe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kupitia CCM Bw. Amon Mwakapala na wenzake wanne hivi karibuni wametakiwa kuyahama makazi yao mara moja kufuatia tuhuma za mauaji yaliyotokea mwaka jana katika kijiji cha Lusungu mkoani hapa.
Maamuzi hayo yalitamkwa hivi karibuni na baraza la wazee wa vijiji vya Isambya,Lusungu na Malowe walioitisha mkutano wa hadhara ili kutoa tamko hilo hadharani kwa maelezo kuwa hawana imani na Mheshimiwa Diwani huyo pamoja na wenzake.
Chifu wa kijiji cha Isambya aliyefahamika kwa jina la Bw.Kayobile Mwaveya katika mkutano huo uliohudhuriwa na wananchi wa vijiji hivyo ,alisema kuwa imani imetoweka katika vijiji hivyo kufuatia mauaji ya mkazi mmoja wa kijiji cha Lusungu aliyetajwa kwa jina la Bw.Mwambunga yaliyotokea mwezi Novemba mwaka jana.
Chifu huyo alisema kuwa, katika mauaji hayo Diwani Mwakapala na wenzake waliotajwa katika mkutano huo kwa majina kuwa ni Bw.Edwin Mwangolelege,Baraka Mgula,Joseph Mbembela na mwingine ambaye alitajwa
kwa jina moja la Bw.Sailos wote kwa pamoja walituhumiwa kuhusika na mauaji ya Bw.Mwambunga.
Kufuatia tuhuma hizo,watuhumiwa walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa katika kituo cha kati mjini hapa na baadae kufikishwa mahakamani ambako walisomewa shitaka la mauaji.
Tuhuma hizo zimeibuka upya baada ya watuhumiwa hao kuachiwa huru mwaka huu kitendo ambacho wakazi wa vijiji hivyo hawakubaliani nacho kwa maelezo kwamba ,upo ushahidi wa wazi ambao unaonyesha watuhumiwa hao walihusika na mauaji hayo .
Wananchi hao walisema kuwa katika kesi hiyo hakuna haki iliyotendeka kwa madai kuwa kuna mkono wa mtu huku wakimtaja mheshimiwa Mbunge na mwenyekiti wa Halmshauri hiyo kupenyeza mkono wao ili kuhakikisha diwani huyo anaachiwa huru ,hivyo katika mazingira hayo uamuzi wao umefikia kikomo cha kuwataka watuhumiwa hao waondoke kwenye makazi yao.
Habari hizo zinaeleza kuwa ,awali marehemu aliwahi kutamka kwenye mkutano mbele ya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Mbeya Bw.Evance Balama kwamba maisha yake yalikuwa hatarini huku akimtaja diwani huyo kuwa ndiye anayetishia maisha yake lakini katika hali kutatanisha walisema hawaelewi ni kwa nini Bw.Balama alilifumbia macho suala hilo.
Sababu zilizotajwa za mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi ya kijiji cha Lusungu na Malowe lenye ukubwa wa ekari 480 ambazo marehemu alikabidhiwa na wananchi kwa kusudi la kusimamia baada ya kubainika mheshimiwa Diwani na serikali ya kijiji kuuza kinyemela ardhi hiyo na pesa kutunisha mifuko yao kwa manufaa yao binafsi.
Naye mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini Mheshimiwa Luckison Mwanjale alitajwa kumegewa ekari 14 kwenye eneo hilo la Umma ambalo walisema tayari ameweka mawe ya kumiliki wakati wananchi hawana taarifa za uzwaji wa eneo hilo .
Bw.Mwanjale ambaye yuko mjini Dodoma kwenye vikao vya Bunge, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alikiri kumiliki eneo la ekari 14 huko Malowe ambazo alizitolea maelezo kwamba eneo hilo alilinunua kabla ya yeye kuwa Mbunge.
Aidha,alikiri pia kuwa ni kweli Diwani Mwakapala na hao wenzake walikumbwa na tuhuma hizo huku akikataa katakata kumsaidia diwani huyo katika tuhuma hizo kama ambavyo wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakimtupia lawama Bw.Mwanjale.
‘’Natarajia kuja hivi karibuni na nitafanya mkutano hapo kijijini ili kuliweka bayana suala hilo,ni kweli ninatambua Mwakapala alikuwa na tuhuma hizo lakini sijawahi kuhangaika kwa lolote kumsaidia,nadhani wanahisi .’’Alisema
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Bw.Andason Mwakabenga alisema anazo taarifa zinazo husiana na mheshimiwa Diwani Bw.Mwakapala,taarifa ambazo zilikuwa zikimtuhumu kujihusisha na mauaji kisha kufikishwa mahakamani ambako aliachiwa huru naye pia alisema
hakuna msaada wake kwenye kesi hiyo.
Mheshimiwa Diwani Bw.Mwakapala alipotafutwa na mtandao huu ili kuzungumziasuala hili kwa kina alikiri kufikishwa ahakamani yeye na wenzakeambako alisema kuwa walisomewa shitaka la mauaji na kuthibitisha kwamba Mahakama iwaachia huru baada ya kukosa ushahidi wa wazi.
Alipoulizwa anampango gani juu ya tamko la baraza la wazee lililomtaka aachingie ngazi madaraka na kuyahama makazi yake ,alisema kuwa hana taarifa zozote kuhusiana na hilo.
Saturday, June 2, 2012
Binti wa
kazi za ndani aliyefahamika kwa jina moja la Zefa(8),mkazi wa Mtaa wa
Block Q - Makunguru,Kata ya Ruanda Jijini Mbeya amefariki dunia akiwa
chumbani kwa usiku wa manane Mei 30 mwaka huu.
Binti
huyo aliyefika siku nne zilizopita akitokea Kijiji cha Msangano, Wilaya
ya Mbozi alikuwa akifanya kazi kwa Bwana Veramundi Mtally mkazi wa mtaa
huo.
Tukio
hilo limetokea Mei 30 mwaka huu mara baada ya kumaliza kupika,binti huyo
aliongeza mkaa na kisha kulala na mtoto huyo wa mwajiri wake aitwaye
Goodluck Veramundi(7),ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya
Msingi Kambalage jijini hapa.
Mnamo
majira ya asubuhi saa 12:00 jioni Bwana Mtally aliingia chumba cha binti
huyo kwania ya kumwamsha ili amuandae mtoto kwa ajili ya shule ndipo
aligonga mlango bila kupata majibu na kisha kugonga dirisha pia
hakufanikiwa ndipo alipoamua kuuvunja mlango na kumkuta binti huyo akiwa
hajitambui pamoja na mtoto aliyekuwa naye chumbani.
Bwana
Mtally aliomba msaada kwa balozi wa mtaa huo kusaidia kutoa nje mwili wa
marehemu Zefa pamoja na mtoto Goodluck na kuwapeleka katika Hospitali
ya Rufaa jijini hapa na walipofika Daktari wa zamu alibainisha kuwa
binti huyo amefariki.
Aidha
mtoto huyo amenusurika kifo kutokana na kujifunika blanketi gubigubi
hivyo hewa yenye moshi haikuweza kumpata,licha ya kukutwa akiwa mchovu
na hajitambui.
Hata
hivyo Bwana Mtally alitoa taarifa Kiyuo cha polisi kati na kupewa PF3 na
hivyo kuruhusiwa kutibiwa na kulazwa mwanawe katika hospitali ya Rufaa.
Mwili wa marehemu Zefa umehifadhiwa Hospitalini hapo,ukisuburi ndugu zake kutoka Msangano kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Wakati
huohuo katika msimu huu wa baridi kali mkoani hapa wamekuwa wakitumia
nishati ya mkaa hali inayohatarisha maisha ya wakazi wengi ambao hutumia
mkaa kupikia na kuota ili kujisitili na baridi.
Jeshi
la polisi lilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi wa tukio
hilo la kusikitisha na kukuta mkaa ukiwa unawaka huku maji
yakichemka,madirisha yakitoa mvuke kutokana na joto kali lililokuwepo
katika chumba hicho.
MWENYEKITI WA WAFUGAJI BONDE LA SONGWE AKIZUNGUMZIA KADHIA WANAYOIPATA KUTOKA KWA WATENDAJI WA SERIKALI YA WILAYA YA CHUNYA
RISTI AMBAZO ZINATOLEWA
KAMA KAWA, NDUGU..........WANATOZWA MILIONI 6, STAKABADHI ZINAANDIKWA LAKI 6
WAFUGAJI WAKIUZA MIFUGI YAO MNADANI ..................BONDE LA SONGWE.......
STAKABADHI BADALA YA KUANDIKWA MIFUGO KUZIDI ZINAANDIKWA KULISHA MASHAMBA AMBAYO HAYAJULIKANI NI MASHAMBA YA NANI NA ENEO GANI!
·
BAADHI
ya watendaji wa Serikali wilayani Chunya wameamua kupimana nguvu na
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi Philip Mulugo ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Songwe kwa kuwakamata wafugaji wa Jimbo hilo na
kuwatoza faini zisizo na tija.
Hali hiyo imebainika baada ya kikosi cha waandishi wa habari kutembelea jimbo hilo
na kukutana na vilio vya wananchi hasa wafugaji ambao walisema kuwa
watendaji hao wanaongozwa na Afisa Mifugo wa wilaya hiyo Adam Mbale.
Mwenyekiti
wa wafugaji wahamiaji wa bonde la Songwe Julius Machia alisema tangu
zoezi la kukamata mifugo inayozidi 70 na kutozwa kwa kila mfugo
unaozidi shilingi 20,000 kumesababisha matatizo mengi kwa wafugaji
yakiwemo baadhi yao kuuwawa na askari kwa kupigwa risasi katika
operesheni ya kamata mifugo na wafugaji kudhulumiwa kwa kupigwa faini
kubwa hali ambayo inamlazimu mfugaji kuuza mifugo kwa bei ya hasara.
“Kwa
miaka 10 sasa zoezi la kukamata mifugo, limekuwa kama mvuta sigara
huvuta sigara anapojisikia kiu kwa kuwa watendaji wa serikali
wanaendesha zoezi hili bila mpangilio na limekuwa linafanyika mara kwa
mara tena kwa unyanyasaji mkubwa’’,anasisitiza Machia.
Wafugaji
hao walisema mbali na fedha wanazotozwa pia kuna vitendio vya
udhalilishaji na ambavyo havifuati haki za binadamu vikiwemo kutishiwa
risasi hewani ili wenye mifugo wajifiche na kuogopa kuuwawa,kupiga
nyumba risasi hadi kubomoa ambapo walitolewa mfano nyumba ya mfugaji
Jikolela Mihambo wa kijiji cha Swela nyumba yake iliteketea kwa moto
baada ya kupigwa kwa risasi.
Mfugaji
katika kijiji cha Chang’ombe Gamaya Bunga alisema utozwaji wa faini
unaonekana kufanyika kwa upendeleo kwa kuwa wakulima wanaovunja sheria
na kulima kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kama vile kwenye
vyanzo vya maji vya mto Songwe na ziwa Rukwa hawakamatwi.
Baadhi ya risiti ambazo MTANDAO WA kalulunga.blogspot.com imezipata
nakala zake zinaonesha kuwa mfugaji Materemki Lugola wa kijiji cha
Wanzani alilipa faini ya shilingi milioni 4,740,000 mwaka 2001 kwa
ajili ya mifugo 948 kula katika mashamba ya wakulima badala ya faini
ambazo zimetakiwa za kuwa na mifugo mingi.
Aliyetakiwa kupokea fedha hizo ni mkulima ambaye shamba lakelimeliwa
na mifugo kupitia ofisi za vijiji badala yake mpokeaji wa fedha hizo ni
Afisa mifugo,kilimo na ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
ambaye amesaini katika risiti kuwa amepokea kiasi hicho cha fedha.
Risiti
nyingine ya mwezi Mei mwaka 2011 inaonesha kuwa mfugaji Julius Machia
wa kijiji cha Chang’ombe alilipa faini ya shilingi milioni sita kwa
ajili ya kuzidi mifugo 300 ambapo kila mfugo uliozidi ulitozwa shilingi
20,000,hata hivyo risiti hiyo imeandikwa mfugaji huyo amelipa shilingi
laki sita badala ya milioni sita.
Wafugaji
wahamiaji wengine waliopigwa faini ya kuzidi kwa mifugo na kuandikiwa
risiti kuwa ni faini kwa ajili ya kulisha mifugo kwenye mashamba ni
Misa Njigula wa kijiji cha Totowe ambaye alipigwa faini ya shilingi
1,275,000 kwa ajili ya ng’ombe 255,Masale Gidai wa kijiji cha Magamba
alipigwa faini ya shilingi 770,000.
Masele
Julius wa kijiji cha Ifuko alipigwa faini ya shilingi 140,000,Mashala
Kwilasa wa kijiji cha Galula Sh. 115,000 na mfugaji John Kasema wa
Totowe Sh. milioni nane kwa ng’ombe 400.
Kwa
upande wake afisa mifugo,kilimo na ushirika katika Halmashauri ya
wilaya ya Chunya Adamu Mbale alisema kuwa Kutokana na uwepo wa mifugo
mingi serikali mwaka 2002 ilitoa sheria ya Halmashauri ya wilaya ya
Chunya kuhakikisha kila mfugaji katika bonde hilo awe na mifugo
isiyozidi 70 na kwamba mfugaji atakayezidisha kiwango hicho cha mifugo
anapigwa faini ya shilingi 20,000 kwa kila mfugo unaozidi.
“Kuna
watendaji wawili kutoka vijiji vya Bonde la Songwe ambao wamechunguzwa
na TAKUKURU baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwenye risiti za
malipo na kesi zao zipo mahakamani’’,anasema Mbale.
Beston
Mwambene mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ihovyo anasema“Wafugaji
wanaamini kuwa kutajirika kwao ni kuongeza mifugo na sio kupunguza
mifugo kwa kuwa hata wakulima wanakuwa na maisha bora kwa kuongeza
uzalishaji katika mashamba yao hapa kinachotakiwa waelimishwe zaidi kuwa na mifugo bora’’,anasema Mwambene.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo
Philip Mulugo ambaye ni Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi
alipoulizwa kwa njia ya simu alisema kuwa alikuwa jhana taarifa hivyo
aliahidi kulifuatilia jambo hilo ambapo watumishi hao wamefanya tena zoezi hilo Mei 16 mpaka Juni 1, mwaka huu huku wakitoza mpaka mbuzi Sh. 20,000.