KITUO cha daladala kilichopo eneo la kituo cha polisi Mbalizi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kimekuwa tishio kwa wasafiri wanaopandia eneo hilo baada ya kugeuka kuwa genge la wezi wa mifukoni.
Genge hilo la wezi wa mifukoni limeendelea kujiimarisha eneo hilo bila kuchukuliwa hatua yeyote ambapo udhibiti wa awali ulikuwa ukifanywa na baadhi ya makondakta na madereva kwa kuwakataza kupanda kwenye magari yao lakini udhibiti huo umeshindikana.
Wezi hao wamebuni mbinu mmbadala ya kufanikisha uhalifu huo kwa kushika madaftari makubwa huku wakipanda gari ambazo abiria huwa wakisimama kisha kuanza kufanya kazi zao za wizi wa simu za kiganjani na fedha kwa abiria.
Baada ya kufanikisha wizi huo hushuka katika kituo kinachofuata kijulikanacho kwa jina la Nsungwe au Stendi ya Tarafani kisha kurejea eneo la kituo cha Polisi.
Hali hiyo imedumu kwa muda mrefu sasa kukiwa hakuna jitihada za kudhibiti kundi hilo la uhalifu ambalo limekuwa likiogopa kuweka maskani yake katika stendi ya Mbalizi kutokana na wapiga debe wa stendi hiyo kuwa na umoja wao na kupiga vita vitendo vya wizi.
No comments:
Post a Comment