DIWANI wa kata ya Bonde la Songwe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kupitia CCM Bw. Amon Mwakapala na wenzake wanne hivi karibuni wametakiwa kuyahama makazi yao mara moja kufuatia tuhuma za mauaji yaliyotokea mwaka jana katika kijiji cha Lusungu mkoani hapa.
Maamuzi hayo yalitamkwa hivi karibuni na baraza la wazee wa vijiji vya Isambya,Lusungu na Malowe walioitisha mkutano wa hadhara ili kutoa tamko hilo hadharani kwa maelezo kuwa hawana imani na Mheshimiwa Diwani huyo pamoja na wenzake.
Chifu wa kijiji cha Isambya aliyefahamika kwa jina la Bw.Kayobile Mwaveya katika mkutano huo uliohudhuriwa na wananchi wa vijiji hivyo ,alisema kuwa imani imetoweka katika vijiji hivyo kufuatia mauaji ya mkazi mmoja wa kijiji cha Lusungu aliyetajwa kwa jina la Bw.Mwambunga yaliyotokea mwezi Novemba mwaka jana.
Chifu huyo alisema kuwa, katika mauaji hayo Diwani Mwakapala na wenzake waliotajwa katika mkutano huo kwa majina kuwa ni Bw.Edwin Mwangolelege,Baraka Mgula,Joseph Mbembela na mwingine ambaye alitajwa
kwa jina moja la Bw.Sailos wote kwa pamoja walituhumiwa kuhusika na mauaji ya Bw.Mwambunga.
Kufuatia tuhuma hizo,watuhumiwa walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa katika kituo cha kati mjini hapa na baadae kufikishwa mahakamani ambako walisomewa shitaka la mauaji.
Tuhuma hizo zimeibuka upya baada ya watuhumiwa hao kuachiwa huru mwaka huu kitendo ambacho wakazi wa vijiji hivyo hawakubaliani nacho kwa maelezo kwamba ,upo ushahidi wa wazi ambao unaonyesha watuhumiwa hao walihusika na mauaji hayo .
Wananchi hao walisema kuwa katika kesi hiyo hakuna haki iliyotendeka kwa madai kuwa kuna mkono wa mtu huku wakimtaja mheshimiwa Mbunge na mwenyekiti wa Halmshauri hiyo kupenyeza mkono wao ili kuhakikisha diwani huyo anaachiwa huru ,hivyo katika mazingira hayo uamuzi wao umefikia kikomo cha kuwataka watuhumiwa hao waondoke kwenye makazi yao.
Habari hizo zinaeleza kuwa ,awali marehemu aliwahi kutamka kwenye mkutano mbele ya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Mbeya Bw.Evance Balama kwamba maisha yake yalikuwa hatarini huku akimtaja diwani huyo kuwa ndiye anayetishia maisha yake lakini katika hali kutatanisha walisema hawaelewi ni kwa nini Bw.Balama alilifumbia macho suala hilo.
Sababu zilizotajwa za mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi ya kijiji cha Lusungu na Malowe lenye ukubwa wa ekari 480 ambazo marehemu alikabidhiwa na wananchi kwa kusudi la kusimamia baada ya kubainika mheshimiwa Diwani na serikali ya kijiji kuuza kinyemela ardhi hiyo na pesa kutunisha mifuko yao kwa manufaa yao binafsi.
Naye mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini Mheshimiwa Luckison Mwanjale alitajwa kumegewa ekari 14 kwenye eneo hilo la Umma ambalo walisema tayari ameweka mawe ya kumiliki wakati wananchi hawana taarifa za uzwaji wa eneo hilo .
Bw.Mwanjale ambaye yuko mjini Dodoma kwenye vikao vya Bunge, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alikiri kumiliki eneo la ekari 14 huko Malowe ambazo alizitolea maelezo kwamba eneo hilo alilinunua kabla ya yeye kuwa Mbunge.
Aidha,alikiri pia kuwa ni kweli Diwani Mwakapala na hao wenzake walikumbwa na tuhuma hizo huku akikataa katakata kumsaidia diwani huyo katika tuhuma hizo kama ambavyo wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakimtupia lawama Bw.Mwanjale.
‘’Natarajia kuja hivi karibuni na nitafanya mkutano hapo kijijini ili kuliweka bayana suala hilo,ni kweli ninatambua Mwakapala alikuwa na tuhuma hizo lakini sijawahi kuhangaika kwa lolote kumsaidia,nadhani wanahisi .’’Alisema
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Bw.Andason Mwakabenga alisema anazo taarifa zinazo husiana na mheshimiwa Diwani Bw.Mwakapala,taarifa ambazo zilikuwa zikimtuhumu kujihusisha na mauaji kisha kufikishwa mahakamani ambako aliachiwa huru naye pia alisema
hakuna msaada wake kwenye kesi hiyo.
Mheshimiwa Diwani Bw.Mwakapala alipotafutwa na mtandao huu ili kuzungumziasuala hili kwa kina alikiri kufikishwa ahakamani yeye na wenzakeambako alisema kuwa walisomewa shitaka la mauaji na kuthibitisha kwamba Mahakama iwaachia huru baada ya kukosa ushahidi wa wazi.
Alipoulizwa anampango gani juu ya tamko la baraza la wazee lililomtaka aachingie ngazi madaraka na kuyahama makazi yake ,alisema kuwa hana taarifa zozote kuhusiana na hilo.
No comments:
Post a Comment