Na Steve Jonas
WANANCHI wa kata ya
Isongole katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya wiki iliyopita
waliweka vizuizi kwenye barabara ya kutoka Uyole kwenda Tukuyu ili kuishinikiza
serikali itatue kero zao .
Vizuizi hivyo
vilivyokuwa vimetawala katika barabara hiyo ni pamoja na uchomaji wa magurudumu
kati kati ya barabara,mawe , magogo na makundi ya watu wa rika mbalimbali
hali iliyosababisha kukwama kwa huduma
za usafiri na huduma nyingine za kijamii.
Kwa mujibu wa baadhi
ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, kwenye
maeneo ya tukio hilo,wananchi walichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na
vitendo vya kifisadi vinavyofanywa kwenye kizuizi cha kutoza ushuru wa mazao
kilichopo eneo la Kijiji cha Namba Wani.
Daud Gabriel mkazi wa
kijiji cha Ndaga alisema kuwa hatua ya wananchi kuzuia barabara hiyo ilitokana
na kero za muda mrefu ambazo zimekuwa zikifanywa na watoza ushuru wa mazao
ambao inadaiwa kwamba kuna ubaguzi unafanywa katika zoezi hilo.
Alisema kuwa kusudi
la wananchi ni kutaka uwiano wa ushuru katika mazao yote kinyume na hivi sasa
ambapo viazi hutozwa kiasi cha shilingi 120,000 kwa tani tano wakati ndizi na
miwa hutozwa kiasi cha shilingi 30,000 kwa tani tano.
Naye Herman Ulaya
alisema kwamba watoza ushuru hao wanatumia ubabe kwa kuwanyanyasa wananchi na
kuwadhalilisha huku akitolea mfano kwake kuwa aliwahi kukamatwa akiwa na mzigo
wa kuni kwaajili ya matumizi ya nyumbani.
Alisema alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Kiwira na baadae
alitozwa shilingi 160,000 kwaajili ya usumbufu kwa watoza ushuru kitendo
ambacho alikielezea kuwa hakikuwa cha halali.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ndaga,Paulos Said Zambi alizitaja kero za
msingi kwa wananchi kuwa ni wananchi wanataka kutozwa ushuru kwa gharama
zinazofanana bila kujali ni aina gani ya bidhaa.
Kero zingine ni kuitaka Halmashauri kuvipatia vijiji kiasi cha mapato
yanayokusanywa,kulihamisha geti kwenda mpakani eneo la Isyonje na kuondoa
ushuru wa mbegu zinazo pelekwa mashambani.
Zambi alisema kuwa wananchi wa vijiji nane vya kata ya Isongole
wamekuwa wakitaabika kwa kipindi kirefu ambapo viongozi wamekuwa wakifumbia
macho kilio chao hata kufikia hatua hiyo ya kuandamana na kufunga barabara ili
viongozi waweze kujua umuhimu wa kilio hicho.
Wananchi hao waliandamana mnamo Julai 2 mwaka huu majira ya asubuhi na
kusababisha vyombo vya usafiri kushindwa kufanya safari hali iliyosababisha
msongamano wa magari hadi majira ya saa 11 jioni.
Askari wa jeshi la Polisi kutoka katika kituo cha kati jijini hapa
walifika saa 8:40 wakiwa na silaha za moto na kufyatua hewani risasi mbili
ambazo hazikufanikiwa kuwatawanya wananchi ambao walikuwa wakisikika wakisema
‘tunataka haki’.
Dakika 30 baadae mkuu wa mkoa wa Mbeya ,Abbas Kandoro akiongozana na
kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya ,walifika katika kijiji cha Ndaga ambako
Kandoro aliweza kutoa tamko la kuwataka wananchi hao wasitoe ushuru hadi hapo
Halmashauri ya Wilaya itakapo kaa na kufika mwafaka.
Baada ya kauli hiyo ya mkuu wa mkoa iliyotamkwa majira ya saa 11jioni
,wananchi waliamua kuondoa vizuizi barabarani bila kushurutishwa na hali
ilikuwa shwari mbali ya zoezi hilo kuwa kero kwa wasafiri ambao walilazimika kukwama
wakati zoezi hilo likiendelea.
No comments:
Post a Comment