Monday, April 23, 2012



TUKIO la mwalimu wa shule ya msingi ya Juhudi ya jijini hapa  kufukuzwa shuleni hapo akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya ushikina mapema mwezi Aprili mwaka huu ,limechukua sura mpya baada ya kubainika baadhi ya wanafunzi pia kujihusisha na vitendo hivyo.

Hayo yalisemwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mnamo Aprili 19 mwaka huu mkutano ambao ulikusudia kuzungumzia mapato na matumizi ya shule hiyo baada ya kutokea mtafaruku kati ya wazazi na kamati ya shule.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa mtaa wa Mwambenja Bw.Lucas Mwakalonge alisema kuwa wanafunzi watatu walikamatwa na walinzi shuleni hapo wakiwa katika harakati za vitendo vya kishirikina.

Bw.Mwakalonge alisema kwamba baada ya wananchi kukusanyika na kujionea tukio hilo waliamuru watoto hao wafikishwe mikononi mwa Polisi ili wakatoe maelezo ambako waliachiwa kwa dhamana baada ya kutoa  maelezo.

Baada ya kugundua kwamba wanafunzi hao  walikuwa wakijihusisha na vitendo vya kishirikina baadhi ya wazazi waliamua kumuomba msamaha mwalimu aliyetajwa kwa jina moja la Kyando ambaye awali alituhumiwa kuhusika na vitendo hivyo kasha kumfukuza shuleni hapo.

Hata hivyo,baadhi ya wananchi bado walionesha dalili za kutokubaliana na suala la kumuomba radhi mwalimu huyo kwa kukosa imani naye.

Mwenyekiti huyo alisema matukio kama hayo si mageni katika mtaa huo kitendo ambacho kimekuwa kikieneza sifa mbaya ya mtaa wa Mwambenja,tukio hilo na lile lililo sababisha mwalimu Kyando kuondolewa shuleni hapo ni sawa na tukio lililo wahi kutokea miaka 15 iliyopita.

Mapema mwezi huu kando kando ya mto jirani na shule vilikutwa vitu vya ajabu ambavyo vilisadikika kuwa ni vitu vya kishirikina,vitu hivyo ni Vibuyu,vyungu viwili,fuvu la kichwa cha ng’ombe,pembe moja la ng’ombe na vitambaa viwili vyenye rangi nyeusi na nyekundu ambavyo vilifungwa kwenye miti miwili tofauti.

Mmoja wa wajumbe waliohudhuria mkutano huo aliyefahamika kwa jina la Frank Jacob,bila ya kufafanua  aliwataka walimu wote wa shule ya Juhudi pamoja na kamati ya shule wakae na kumaliza tofauti zao ambazo zimekuwa zikitapakaza sifa mbaya ndani ya jamii inayo wazunguka.


No comments:

Post a Comment