Wednesday, April 4, 2012

WALIMU MBEYA WASHINIKIZA KIONGOZI WAO ARUDISHWE MADARAKANI

 
ZAIDI ya walimu 50 wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya juzi waliandamana katika ofisi za Chama cha Walimu wilaya ya Mbeya(CWT) wakishinikiza kurejeshwa kazini kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho ambaye alisimamishwa na kamati tendaji ya wilaya hiyo.
 
Walimu hao wameliambia gazeti hili kuwa kamati hiyo haikumtendea haki mwenyekiti wao waliyemtaja kwa jina la Anthony Mwaselela ambaye aliandikiwa barua ya kusimamishwa na uongozi mnamo Januari 16, mwaka huu ambayo ilisainiwa na katibu wa CWT wilaya ya Mbeya Monica Haule.
 
Kwa mujibu wa barua hiyo( nakala zake tunazo), mwenyekiti huyo anatuhumiwa kushiriki vikao vya walimu waliojiendeleza kielimu ambao wanafahamika kama  Umoja wa maafisa Elimu Tanzania(UMET).
 
Awali walimu hao waliwahi kufunga ofisi za CWT Mkoa na ofisi ya  Mbeya vijijini kwa madai kwamba, katibu wa CWT Mkoa alishindwa kuwaandikia barua ya kuwaruhusu kwenda Ikulu  kumwona Rais kwa kusudi la kupinga waraka kandamizi uliokuwa umetolewa dhidi yao.
Aidha,katibu hyo pia anatuhumiwa  kutoshirikiana na viongozi wenzie  kwenda polisi kushughulikia kufunguliwa kwa ofisi za CWT  kitendo ambacho inadaiwa ni kukiuka  katiba ya chama hicho ibara ya 41(iv) na (v).

Ukiukwaji huo wanasema ulisababisha wanachama kukosa huduma za kiofisi,kushindwa kuangalia usalama wa mali za chama na kukosa mawasiliano kati ya wilaya moja hadi nyingine.
 

 
 Kwa mujibu wa barua walioandikiwa wawakilishi wa shule  wa halmashauri hiyo yenye kumbukumbu namba CWT/MBV/WAW/11/01 kutokana na makosa  ,kamati ya utendaji ya wilaya ilifikia maamuzi ya kumsimamisha uongozi mwenyekiti huyo hadi utakapofanyika mkutano mkuu ambao utakuwa na maamuzi ya kumuondoa au kumrudisha kwenye madaraka hayo.
 
Hata hivyo, walimu hao walidai kuwa hawakushirikishwa katika maamuzi hayo kitendo ambacho walisema ni cha kibabe kwani hata barua aliyoandikiwa Mwaselela iliwafikia wanachama wachache tena kwa siri.
 
Walifafanua kwamba, wenye maamuzi ya kumvua madaraka kiongozi wa kuchaguliwa ni wanachama wenyewe kupitia mkutano mkuu  kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na kudai kuwa kamati tendaji ilikiuka kanuni za chama hivyo walitaka mwenyekiti huyo arudishwe madarakani huku mkutano mkuu ukisubiliwa.
 
Maandamano ya walimu hao kwenye ofisi za CWT Wilaya ya Mbeya zilizopo uwanja wa Sokoine jijini hapa hayakufanikiwa kuwakuta viongozi wao hali iliyopelekea mwenyekiti wa CWT mkoa wa Mbeya Nelusigwe Kayuni na katibu wake Kasuku Bilago kulazimika kukaa kukaa na kujadili na walimu hao.
 
Kayuni alitumia muda mrefu kuwafafanulia walimu hao katiba ya chama na taratibu walizopaswa kuzifuata ingawa naye alikri kuwa kamati tendaji haikumtendea haki mwenyekiti huyo huku akieleza kuwa ofisi ya CWT mkoa hawana uwezo wa kutengua uamuzi huo bali walitakiwa wasubiri mkutano mkuu kwa ajili ya maamuzi.
 
Hali ilizidi kuwa tete baada ya mwenyekiti wa mkoa  kuwaambia kuwa mwaka huu hakutakuwa na mkutano mkuu wa chama hicho nchi nzima bali kwa dharula mkutano huo utakuwepo kwaajili ya tuhuma hizo pekee na kuwataka walimu hao kuwa wavumilivu.
 
Katika mkutano huo mvutano ulikuwa mkali kati ya uongozi wa CWT mkoa na walimu hao hali iliyowapelekea baadhi ya walimu kuanza kutawanyika mmoja baada ya mwingine kwa madai kuwa hawakuridhishwa na majibu ya viongozi hao na baadhi ya walimu hao walitishia kuzifunga tena ofisi hizo.

No comments:

Post a Comment