Tuesday, March 27, 2012

MCHUNGAJI WA EAGT AJIINGIZA KWENYE BIFU JIPYA

MCHUNGAJI AYUBU  MWASIPOSYA


MCHUNGAJI wa kanisa la  EAGT lililopo katika eneo la TAZARA kwenye  mji  mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya,Ayub Mwasiposya amejiingiza kwenye malumbano mapya na vyombo vya habari  akidai kuwa vinatumiwa  na muumini wake  kumchafua .
Mwasiposya amejikuta akirudi kwenye mgogoro huo baada ya hapo awali   kusuguana kiimani na muumini wake aliyetambulika kwa jina la Benson Mwakilembe mgogoro ambao ulimfikisha mchungaji huyo mikononi mwa polisi akituhumiwa kumshika uchawi muumini huyo.
Mchungaji Mwasiposya katika mazungumzo na mwandishi wetu  aliviponda vyombo vya habari kwa maelezo kuwa vimekuwa vikitumiwa na Mwakilembe kwa kununuliwa ili kueneza habari chafu dhidi yake katika utumishi wa kazi ya mungu.
Mchungaji huyo aliyasema hayo mara baada ya kutakiwa  na mwandishi wa habari hizi kutoa ufafanuzi kuhusu habari zilizo kwenye mitandao zikimhusisha na mambo ya kishirikina ambapo alikiri kupata taarifa kuwa kuna habari hizo kwenye mitandao lakini akizitolea maelezo kuwa kuna kijana mmoja amekuwa akitapakaza habari hizo za uongo.
Alimtaja kijana huyo kwa jina moja la Gasper mkazi wa Mbalizi kuwa ndiye anaye shirikiana na Mwakilembe kumchafua kwenye vyombo vya habari tangu mwaka jana.
‘’Ndugu mwandishi ,mmenunuliwa ili kunichafua lakini mimi nasimamia kwenye neon basi.Hakuna kitakacho haribika kwakuwa naamini hizo ni habari za uzushi na ni pesa tu zinazomsumbua na amefanikiwa kunichafua kwenye vyombo mbali mbali vya habari’’.Alisema na kuongeza
‘’Siwezi kushindana na mwenye pesa bali namtegemea mungu pekee wala sipo tayari kumpigia magoti binadamu mwenza eti kwa sababu ya kipato,badilikeni msikubali kutumiwa kwani naamini taaluma yenu ni muhimu katika jamii .’’
Chanzo cha mgogoro huo ni kufuatia mchungaji huyo mwaka jana  kumtangaza Mwakilembe kwamba anapesa za kuzimu hivyo hawezi kupokea msaada wa mifuko ya saruji ambayo aliitoa muumini huyo kwaajili ya ujenzi wa kanisa.
Mwakilembe alisema kuwa mbali ya yeye kulihama kanisa la mchungaji Mwasiposya lakini aliamua kujitolea mchango wa ujenzi wa kanisa hilo kwa maana ya kumshukuru mungu pale alipofikia lakini cha ajabu Mwasiposya alimtangaza vibaya muumini huyo kwa kumkashfu kwamba mali zake ni za kuzimu.
Habari zaidi zinamsema  Mchungaji Mwasiposya kwamba idadi kubwa ya waumini wake kanisa limewatenga kwa maelezo kuwa mchungaji huyo amekuwa akiwatuhumu waumini wake kwamba ni washirikia.
Mbali ya mchungaji huyo kutuhumiwa  kuwatenga waumini hao kwa sababu hizo za kishirikina pia amekuwa akilalamikiwa kuendesha ibada zake usiku wa manane na kutuhumiwa kuwabughudhi wakazi waliojirani na kanisa hilo.
Hata hivyo,mchungaji huyo mbali ya kuvirushia madongo vyombo vya habari, masaa matano baadae Mwasiposya  alimpigia simu  mwandishi wa habari hizi na kuomba radhi kufuatia kauli zake za awali za kuviponda vyombo vya habari na kuvituhumu kutumiwa na Mwakilembe.

No comments:

Post a Comment