Wednesday, March 28, 2012

MTUHUMIWA ALIYETOROKA MIKONONI MWA POLISI AKAMATWA





Pichani ni kituo cha Polisi Kati  Jijini Mbeya.
*******

MANENO  Wiwa  Kalinga ni mmoja wa mahabusu waliotoroka wiki iliyopita katika Kituo cha Polisi cha  Kati Mkoani Mbeya Tanzania alikamatwa akiwa mafichoni Wilayani Mbozi mkoani humo.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa majira ya saa 10 alfajiri katika kijiji cha Ruanda wilayani humo.

Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na msako mkali uliofanywa na Jeshi la polisi  mkoani hapa, mara baada ya kutoroka ndani ya kituo cha polisi alikokuwa akishikiliwa na watuhumiwa wengine .

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi, amethibitisha kukamatwa kwa mahabusu huyo na kufanya jumla ya waliokamatwa kufikia wawili, huku mwenzake aitwaye  Fadhili Mwaitebele (27) mkazi wa Ilomba jijini Mbeya alikamatwa muda mfupi baada ya kutoroka.

Hata hivyo Kamanda Nyombi ametoa wito kwa wananchi kuwa popote watakapo waona wahalifu hao watoe taarifa kituo chochote cha Polisi kwani watu hao ni hatari katika jamii ,watuhumiwa hao walitoroka kituoni hapo baada ya kufanikiwa kuchonga tundu lililotokeza nje ya ukuta kisha wakatoweka huku askari waliokuwepo doria wakiendelea kuuchapa usingizi kituoni hapo.

No comments:

Post a Comment