Tuesday, May 29, 2012
MSHAURI WA CHADEMA MBEYA AMTUPIA KOMBORA MWENYEKITI WAKE
MSHAURI wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)Mkoa wa Mbeya,Bw. Eddo Mwamalala
amemtupia kombora Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Mbeya mjini Bw.John
Mwambigija kuwa siasa zake majukwaani ni
za uchochezi ambao haupaswi kufumbiwa macho.
Aliyasema hayo juzi katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Mbeya Peack mjini
hapa huku lawama hizo pia akilitupia Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa maelezo
kuwa Polisi wamekuwa wakimfumbia macho Bw.Mwambigija.
Bw.Mwamalala ambaye pia ni
mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa alisema kuwa,Bw.Mwambigija amekuwa akiyatumia
majukwaa kwa kutoa lugha za matusi na vichekesho kitendo ambacho kinaweza
kuhatarisha amani ya watanzania.
Katika mkutano huo
Bw.Mwamalala aliwaambia waandishi kwamba ,anashangazwa pia na ukimya wa katibu
mkuu wa Chadema Bw.Wilbrod Slaa kuendelea kukaa kimya bila ya kukemea tabia
hiyo ya Mwenyekiti huyo.
“ Nalishangaa sana jeshi la
polisi kwa kuendelea kumwangalia huyu mtu kauli anazotoa akiwa jukwaani ni za
uchochezi kwani lugha nyingi ni za matusi lakini polisi wamekuwa wakimwangalia hata
katibu mkuu Dr.Slaa amekaa kimya bila ya kukemea vitendo hivyo.’’Alisema
Aidha,aliongeza kuwa kutokana
na lugha za matusi na vichekesho visivyo na tija katika jamii amekuwa akishangiliwa na wananchi na kupata kiburi akijigamba
na kusema yeye ndiye aliye mpa madaraka Mbuge Joseph Mbilinyi na madiwani
kupitia tiketi ya Chadema mkoani hapa.
Mshauri huyo aliendelea
kuponda akisema kwamba Bw.Mwambigija ni
tatizo ndani ya Chadema maana kazi yake ni kuchekesha watu majukwaani, kutukana
na kuendelea kutoa matamko yasiyo na tija kwa wanachama huku akiwarubuni baadhi
wa wanawake akiomba magari yao kwa ajili ya misafara isiyo rasmi kwa ushawishi
wa kuwateua kwenye ubunge wa viti
maalumu.
.
Bw.Mwamalala alisema kuwa
Viongozi wa Chadema kuendelea kulifumbia macho suala la Mwambigija ni kukibomoa
chama badala ya kukijenga.
Alisema kutokana na mambo
hayo tayari Bw.Mwambigija ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee wa upako mnamo
Juni 4 mwaka huu atapandishwa kizimbani kusomewa shitaka kwa mara ya kwanza.
Bw.Mwambigija katika
mahojiano mafupi na majira kwa njia ya simu alikiri kwamba siku hiyo atasomewa
shitaka baada ya kushitakiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya
Chunya Bw.George Ntasha Katabi akituhumiwa kumtolea lugha za kashfa katika moja
ya mkutano.
Monday, May 28, 2012
WAMACHINGA MBEYA KUHAMISHWA -IMEFAHAMIKA
TAARIFA
ambazo zimethibitishwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Juma Idd
zimeeleza kuwa kufikia Trehe 15 mwazi wa sita mwaka huu 2012, zoezi la
kuwahamisha wamachinga katikati ya Jiji la Mbeya litafanyika.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Mkurugenzi huyoamesema kuwa
mwisho wa wamchinga hao kuwepo katikati ya Jiji ni tarehe 30 mwezi huu
wa tano baada ya hapo zoezi la kuwahamishia wamachinga hao katika
maeneo yaliyotengwa litaanza aua kukamilika..
Monday, May 21, 2012
KANISA LA UINJILISTI NA MKAKATI WA MAENDELEO YA JAMII
Mchungaji Markus Lehner (kushoto) akiwa kwenye moja ya kazi za Kanisa la Uinjilist Mbalizi mkoani Mbeya |
Steve Jonas,Mbeya
Na
kila jambo linaumuhimu wake kwenye nafasi yake kulingana na mazingira husika
kwa mujibu wa jiografia ya eneo analoishi binadamu wa leo.
Zipo
changamoto nyingi anazokabiliana nazo mwanadamu katika maisha yake ya kila siku
,pia changamoto hizi zimebeba uzito mkubwa ambao ambao umekuwa kero katika
uboreshaji wa huduma za kijamii.
Ni
wazi kwamba jamii inahitaji kupata huduma zilizo bora kwa wakati muafaka ambapo
matokeo ya huduma bora ni kuwa na jamii
yenye ufahamu mzuri,uelewa wa mambo mbali mbali na ubunifu.
Matokeo
haya ni chanzo cha kuwa na taifa lenye watu makini katika kukuza kipato cha
kukidhi mahitaji yao ya kila siku na kupanua wigo wa pato la taifa.
Lakini
kikubwa zaidi katika hili ni kuunda msingi mzuri kwa kuiandaa jamii ili iweze kufika pale
panapokusudiwa,haijalishi ni mazingira gani bali mawazo endelevu na chanya
katika maarifa yanayoweza kuikwamua jamii kwenye hali ya umasikini.
Yapo
mambo mengi niniyoweza kuyaelezea kwa upana zaidi kuhusiana na kero zinazo
izunguka jamii ya kitanzania,lakini leo ni vyema nielekeze nguvu zangu kwa kile
kilichonisukuma kuandika makala haya.
Fikra
na uelewa wangu ni vitu viwili ambavyo vimezama ndani ya shughuli zinazo fanywa
na kanisa la Uinjilisti Tanzania lililopo Mbalizi katika Halmashauri ya Wilaya
ya Mbeya.
Kanisa
hilo limewekeza nguvu kubwa kuikwamua jamii kimaendeleo na kupunguza hali ngumu
ya maisha anayokabiliana nayo mtanzania wa kipato cha chini.
Mchango
wa kanisa hilo umejidhihirisha kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ni
Iringa,Mbeya,Njombe,Ruvuma,Rukwa na Katavi.
Mkurugenzi
wa kanisa hilo ,Mchungaji Markus Lehner ofisini
kwake jijini Mbeya alisema kuwa mbali ya kanisa kuhubiri neno la Mungu pia
linahudumia jamii kukuza elimu kwa
kusaidia ujenzi wa shule za msingi na sekondari.
Huduma zingine
ni za afya kwa ujenzi wa vituo vya
afya na hospitali teule ya Wilaya ya
Mbeya na kuwapatia ujuzivijana kwa kujenga vyuo vya ufundi katika mikoa hiyo ya
kanda ya nyanda za juu kusini.
Alisema
wananchi walikuwa wakitaabika kupata
huduma hizo na kulazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 10 ambapo tatizo
hilo kwa sasa limepungua baada ya kukamilika hospitali hiyo ambayo kwa mujibu wa mganga
mkuu hospitalini hapo,Bw.Msafiri Kimaro, ina uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa
wakati mmoja.
Hospitali
hiyo ilizinduliwa Oktoba 18 mwaka 2008 na Rais,Jakaya Kikwete ni tegemeo kwa wananchi mkoani humo na mikoa jirani huku ikipunguza msongamano wa
wagonjwa kwenye hospitali zingine kama ilivyokuwa hapo awali.
Bw.Lehner
alisema ili kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme kanisa lilifanikiwa
kupata wafadhiri kutika shirika lisilo la kiserikali kutoka Uswis na kuiwezesha
Hospitali kupata umeme wa jua
uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Alisema
umeme huo utatoa huduma za hospitali kama vile upasuaji na wadi ya uzalishaji
ambapo alithibitisha kuwa utadumu kwa muda wa zaidi ya miaka 30.
Hata
hivyo, mchungaji Lehner alisema zipo changamoto ambazo zinahitaji mkono wa
serikali ambazo ni maji na vyombo vya usafiri kwa watumishi wa hospitali.
Mchungaji
Lehner alishauri madhehebu kubuni mbinu kujipatia kipato kitakacho jenga uchumi
wa jamii badala ya kutegemea sadaka za waumini.
Pia
kanisa linashughulika na kuhifadhi mazingira, kituo cha kutolea elimu kuhusu
mazingira na utamaduni wa maisha ya watu wa kale na hifadhi ndogo ya wanyama
kama ishara ya urithi kutoka kwa watu wa kale.
Baadhi
ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wakazi wa vijiji jirani na
hospitali hiyo walisema kuwa ,tangu Tanzania ilipopata uhuru wake mwaka
1961 hawakuwahi kupata huduma ya maji ya bomba ambayo kwa sasa
wananufaika kupitia huduma za hospitali hiyo.
WAANDISHI WA HABARI WAPEWE FURSA KWENYE ZIARA ZA VIONGOZI MIKOANI
KATIKA ziara za viongozi wa kitaifa mikoani, zinaonekana kuwa na
mapungufu ya kuikosesha jamii kile kinacho kusudiwa kuwafikia.
Nalazimika kuyasema haya kufuatia dosari zilizojitokeza hivi
karibuni katika ufunguzi wa mbio za Mwenge Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Waziri mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyefungua mbio
hizo, lakini awali ya yote siku moja kabla ya kuanza kwa mbio hizo mnamo Mei 10
kwenye Ikulu ndogo ya mkoa wa Mbeya, kulitokea mkanganyiko ambao unaweza kuwa
chanzo cha kuinyima jamii haki yao ya msingi ya kupata habari.
Wanahabari ni muhimili wa nne katika serikali yetu ikitanguliwa na serikali
kuu,sheria na Bunge.
Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba wanaifikishia jamii
taarifa ya serikali kwa mujibu wa kanuni na maadili ya tasnia yao. Lakini kile
kilicho jitokeza siku hiyo ni sehemu ya mapungufu ambayo hayastahili kurudiwa.
Naamini kwamba, bajeti ya mkoa katika shughuli zote
kuhusiana na mbio za mwenge ilizingatia umuhimu na heshima ya mbio hizo ambazo
imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa watanzania tangu enzi za uhai wa mwasisi wa mbio hizo, Baba wa
Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Katika bajeti hiyo waandishi hawakupewa umuhimu wa
juu kama muhimili wa nne katika Taifa kwa kushindwa kuwaandalia usafiri wa
kutosha ili kufika katika maeneo mbali mbali aliyopangiwa kiongozi wa
serikali,Mh.Pinda
Naamini kwamba si wananchi wote ambao walikuwa na fursa ya
kufika alikotembelea Waziri mkuu,kwa
maana hiyo msaada wao mkubwa ulikuwa ni kupata taarifa kwa upana kupitia vyombo
vya habari.
Lakini kwa sababu idadi kubwa ya waandishi wa habari
walishindwa kuambatana na msafara wa Waziri mkuu, kutokana na kukosa usafiri, naamini hata katika upashaji
wa habari kwa jamii haukukidhi mahitaji ya wananchi hasa ukizingatia kwamba
tukio hilo la mbio za mwenge lilikuwa tukio kubwa la kitaifa mkoani humo.
Nadhani jambo la kwanza la kuzingatia lilikuwa ni
kuhakikisha wananchi wanapata ujmbe wa mbio hizo na agizo la kiongozi wao
kupitia vyombo vya habari ,hivyo basi waandishi walitakiwa kuandaliwa mapema mazingira
ya kuweza kufanya kazi zao kwa maslahi ya jamii.
Najua zipo sababu ambazo zinaweza kutolewa za kushindwa
kuwaandalia waandishi usafiri wa kuongozana na msafara wa Mh.Pinda kabla ya
kuzindua mbio hizo za mwenge alipo kuwa akienda kukagua Kiwanda cha Tanganyika
Packers,kiwanda cha Marumaru na kituo cha utafiti wa kilimo Uyole.
Lakini sababu hizo nadiliki kusema kuwa zinaweza kuwa
hazitalingana na umuhimu wa wanahabari katika kuitumikia jamii,moja kwa moja,
nadhani sababu ambazo zinaweza kutajwa
labda inaweza kuwa ni ufinyu wa bajeti kuhusu ugeni huo kwa maana kuwa
waandaji walihofu namna ya kuwawezesha (posho) waandishi.
Afisa habari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya anapaswa kujua
mahitaji ya wananchi kupitia waandishi wa habari,hili ndilo jambo la
msingi. Posho ni jambo la ziada japo si kweli kwamba ofisi ingeshindwa kufanya
hivyo ,kwa sababu hawakupewa umuhimu ndio sababu zilizo sababisha kuwepo
usumbufu wa usafiri.
Katika hili pia ni vema nikiwa wazi kwamba si waandishi wote
ambao wanategemea kupewa posho ili waweze kumudu kazi zao,hapana.Nia ya
mwandishi ni kupata habari na kuitangazia jamii kile ambacho kinaonekana kuwa
na umuhimu.
Na kwa kuwa waandishi ni kama daraja la kuwaunganisha viongozi na wananchi ,waandishi wanaitumia fursa kama
hiyo ili kuzitumikia pande zote mbili bila kujali posho.Jambo la msingi
wasinyanyapaliwe kwenye vyombo vya usafiri kama ilivyo tokea katika gari moja
aina ya Land cruiser lenye namba za usajili DFP 5950.
Dereva wa gari hilo na afisa habari wa ofisi ya mkuu wa mkoa kwa pamoja
walitoa lugha ambazo ziliwafedhehesha waandishi wakati wakitaka waandishi
wapungue ndani ya gari hilo,si mara ya kwanza waandishi kufanyiwa vituko na watu hao.
Kwa lugha za nyodo afisa habari huyo bila kuzingatia taaluma ya wanahabari aliwataka waandishi
wajitegemee usafiri kwa madai kuwa gari lililokuwa limeandaliwa kwa ajili yao
lilikuwa na uwezo wa kubeba waandishi kumi tu,ndani ya gari hilo kulikuwa
waandishi 11 lakini kutokana na kauli hizo baadhi ya waandishi waliamua kutelemka na kutawanyika
.
Hali hiyo imesababisha idadi kubwa ya waandishi kususia mbio
za mwenge huku kukiwa na malalamiko kwamba afisa habari amekuwa akiwatumia
marafiki zake wanahabari katika ziara za viongozi mkoani hapa na kitendo hicho
kimekuwa kikijirudia mara kwa mara.
Afisa habari kama kweli ni mwanataaluma wa habari, anapaswa
kubadilika ili kazi za viongozi zitangazwe kwa mapana na viongozi pia katika
ziara zao wajulishwe kwa mapana kero za wananchi kupitia tasnia ya habari ndani
ya ziara zao.
Thursday, May 17, 2012
PATRICK MAFISANGO NI PENGO KUBWA KWA SIMBA
KESHO WATAKUWA WAKIUAGA MWILI WA MAREHEMU KATIKA VIWANJA VYA
LEADERS CLUB JIJINI DAR ES SALAAM NA KUUSAFIRISHA KWENDA DRC KWANI YEYE
NI MRWANDA MWENYE ASILI YA KONGO.
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na
timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo alfajiri
(Mei 17 mwaka huu) kwa ajali ya gari Dar es Salaam.

Msiba
huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote
alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya
kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo
chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda
mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri
uwanjani.
Wakati
mauti inamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa Amavubi kwa ajili ya mechi za mchujo
za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi ujao.
TFF
inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu
aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina
Tuesday, May 15, 2012
WATUNISIA KUCHEZESHA MECHI YA TAIFA STARS HUKO ABIJAN
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua
waamuzi kutoka Tunisia na Misri kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia
hatua ya makundi kati ya Taifa Stars na Ivory Coast itakayochezwa Juni 2 mwaka
huu jijini Abidjan.
mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia. Mwamuzi
msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri. Mwamuzi wa akiba ni Youssef
Essrayri pia kutoka Tunisia.
Mtathmini wa waamuzi (referee
assessor) ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo
atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.
MBEYA BADO YATIKISWA NA MAMBO YA KISHIRIKINA
*Watatu wakiri hadharani na kukabithi mikoba yao.
*Wachanjwa chale hadharani na Mganga wa Jadi.
*Watozwa shilingi 400,000 kila mmoja kama adhabu.
WATUwatatu wanaoshukiwa kuwa ni
washirikina wamekiri hadharani katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Mataa wa Mwambenja, Kata ya Iganzo Jijini Mbeya, mbele ya Mganga
wa Jadi Nestory Vitus Kasonso kutoka , Sumbawanga Mkoani
Rukwa.
Tukio hilo limetokea Mei 14 mwaka huu
majira ya saa 8 mchana baada ya mganga huyo kufanya msako wa kuwabaini
wachawi katika mtaa huo baada ya kuombwa na wakati wa mtaa huo, kutokana
na kukithiri kwa vitendo vya kishirikina mtaani hapo.
Imedaiwa kuwa baadhi ya wakazi wa
mtaa huo wamekuwa hawana maendeleo kutokana na pesa kupotea katika
mazingira ya kutatanisha, mifugo kufa na watoto kuanguka mashuleni mara
kwa mara hali iliyowafanya kuitisha mkutano huo, ambapo awali aliletwa
Mganga wa Jadi kutoka Manienga Wilaya ya Mbarali, Bwana Mzungu Pondanga
(49), ambaye alifanya kazi kwa siku kadhaa baada ya kusitishwa mkataba
wake.
Sababu za kusitishwa kwa mkataba huo
ulitokana na sababu za wananchi zakutaka awabainishe hadharani wale wote
wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina, ambapo mganga huyo alikataa
kwa kile alichodai ni kuhofia uvunjifu wa amani mtaani hapo na wananchi
kuona kuwa hawajatendewa haki na hivyo kufanya kazi kwa simu moja tu
Aprili 29 mwaka huu ambapo matunguli kadhaa yaliteketezwa kwa moto.
Baadha ya hapo Kamati maalum
iliyochaguliwa na wananchi na kupata baraka kutoka kwa Chifu wa kabila
la Kisafwa Bwana Ndasya waliamua kumtafuta Mganga mwingine wa Jadi
ambaye walimtoa Laela Bwana Kasondo ambaye aliahidi kuwataha wachawi
wote na kwamba hakutakuwa na uvunjifu wa amani.
Aidha Bwana Kasonso baada ya kukagua
maeneo yote kwa makini kwa majuma mawili tangu Mei mosi ndipo aliitisha
mkutano wa hadhara jana na kuwabainisha watu watatu wawili wakiwa
wanaume na mmoja mwanamke.
Watu hao waliotanjwa hadharani ni
pamoja na Daud Mwakalobo, Inspector Mwanjabala na Bi Upendo Kapinga
ambaye ni Mke wa mwilu mmoja jijini hapa.
Katika makubaliano baina ya Kamati ya
mtaa na Mganga ilikubaliana yeyote atakaye toa kwa hiari yake matunguli
yake atatozwa shilingi 100,000 na ambaye atakutwa na mganga huyo
atatozwa shilingi 400,000 kama adhabu.
Kutokana na zoezi hilo wote watatu
walikutwa na mganga huyo na kukiri kujihusisha na vitendo vya
kishirikina na kwa kudhihirisha hilo walikutwa na pembe za ng'ombe na
mifupa ya ndege kama bundina dawa zilizochanganywa nyingine zilikutwa
chooni na vyumbani ambazo zililetwa hadharani na kuchomwa.
Baada ya kuchoma moto lilifuata zoezi
la kuchanjwa chale na mganga ambapo wote wawili (wanaume), walichanjwa
hadharani sehemu mbalimbali za miili yao kama kichwani (utosini) na paji
la uso miguuni, mikononi na maungoni huku mganga huyo akiwashindilia
dawa nyeusi iliyosagwa mithili ya unga laini na kupewa sharti la kutooga
kwa siku moja.
Aidha yalitokea mabishano makali
baada ya Inspector Mwanjabala kujaribu kukataa kuchanjwa chale ndipo
mkutano ulipiga yowe la kumtaka ahame mara moja ndipo alikubali na
kuchanjwa bila ubishi.
Bi. Upendo Kapinga alienda kuchanjwa
katika nyumba jirani ili kumstahi kutokana na makubaliano ili kutunza
utu wa mwanamke ingawa zogo lilitokea ikidaiwa naye achanjwe hadharani
ambapo wengine walikejeri ku wa mbona wengine humwaga hadharani huku
wakiwa utupu.
Baada ya zoezi hilo mganga aliwaasa
wananchi kutowachukia na kuwaogopa kwani hivi sasa atayejaribu kurudia
tabia ya ushirikina atafariki mara moja.
Hata hivyo zoezi hilo lilipata baraka
kutoka kamati ya Polisi jamii na ulinzi shirikishi na kutaka wakazi hao
wa Iganzo kufanya zoezi hilo kwa amani na kama kutatokea uvunjifu wa
amani utatokea viongozi watawajibika.
Monday, May 14, 2012
MASHINDANO YA DARTS YAPAMBA MOTO BLUE HOUSE MWANJELWA
WADAU WAKIFUATILIA KWA UMAKINI MASHINDANO HAYO MUDA HUU
MMOJA WA WASHIRIKI KATIKA SHINDANO HILI AKIRUSHA KISHALE MUDA MCHACHE ULIO PITA
WAKIENDELEA NA SHINDANO
MCHEZAJI BWANA JULIUS MUNISI AKIRUSHA KISHALE MUDA MCHACHE ULIO PITA
WADAU WAKIENDELEA KUFUATILIA TUKIO
ENDELEA KUFUATILIA TONE MEDIA LIVE GROUP TUPO ENEO LA TUKIO MOJA KWA MOJA
MTWANGA INJILI WA MIAKA 46 ABAKA KIBINTI CHA MIAKA 14
OBED Mwakilasa (46),
mkazi wa Kijiji cha Mwela, Kata ya Kandete wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya ametuhumiwa
kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na kumsababishia maumivu
makali katika mwili wake.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw.
Anania Mwalukasa amesema tukio hilo limetokea Mei 10 mwaka huu, ambapo
mtuhumiwa anadaiwa alimuita mtoto huyo kwenye shamba la michai kisha
kumfanyia ukatili huo.
Baada ya kukuta anakumbana na mkono
wa sheria Mwalikasa alienda kuomba msamaha kwa wazazi wa mtoto huyo ili
wamsamehe, ombi ambalo lilipokelewa na kusamehewa.
Aidha imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alifika kijijini hapo kwa mbinu ya kuhubiri neno la Mungu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Bwana
Mwalukasa ameonekana kukasirishwa na kitendo cha wazazi hao kusameheana
nyumbani na kudai kuwa tabia hiyo ikiendekezwa itasababisha kuendelea
kwa vitendo viovu kijijini hapo.
Madhara hayo yaliyosababishwa na
Bw. Mwakilasa kwa mtoto huyo hayajaweza kufahamika kutokana na wazazi
kutompeleka mtoto wao kufanyiwa uchunguzi katika Kituo chochote cha
huduma ya Afya(Zahanati/Kituo cha afya/Hospitali).
Hata hivyo vitendo hivyo vya ubakaji wilayani humo vimeota mizizi kutokana na baadhi ya wazazi kufumbia macho kwa kupewa pesa.
MWANAFUNZI AJIUA BAADA YA KUBAINI ANA MIMBA
Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika
Shule ya Sekondari Isange ,mkazi wa Isanu, Kata ya Isange, Wilaya ya
Rungwe Mkoani Mbeya mnamo Mei 11 mwaka huu amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya
kufungia ng'ombe muda mfupi baada ya kugundua alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu .
Afisa mtendaji wa Kata hiyo Bwana
Anyambege Mwangomo amelitaja jina la marehemu kuwa ni Enitha Ndambo
(15), ambaye alikuwa akiishi na bibi yake Bi Emelia Ndenga.
Marehemu alichukua hatua ya kujinyonga wakati mlezi wake akiwa katika kilabu cha pombe na kamba
aliyotumia ilikuwa ndani ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi.
Polisi walifika kwenye eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na
kuupeleka katika Zahanati ya Isange kwa ajili ya kufanya upasuaji, ili
kuthibitisha kama alikuwa na ujauzito na mara baada ya upasuaji
waliwaruhusu wanakijiji kuzika mwili wa marehemu na kiumbe
kilichokuwa tumboni.
Mwili
wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari Kalinga kutoka katika
Hospitali ya Serikali ya Makandana iliyopo wilayani humo, na zoezi la
upimaji wa mimba wanafunzi ulifanywa na Daktari Anna Mwelevu wa Zahanati ya
Isange..
Aidha katika uchunguzi uliofanywa
umebaini aliyemsababishia ujauzito ni mwanafunzi wa shule hiyo Alex
Mwaitege, anayesoma kidato cha kwanza.
KOCHA MPYA WA TAIFA STARS AITA 25 KIKOSINI
K
|
ocha Mkuu wa Taifa
Stars, Kim Poulsen leo (Mei 14 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 25
kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi Kanda ya Afrika
dhidi ya Ivory Coast.
Akitangaza
kikosi hicho ambacho kitaingia kambini kesho kutwa (Mei 16 mwaka huu, Kim
amesema uteuzi wake umezingatia uwezo wa mchezaji uwanjani, nafasi anayocheza
na ubora wake.
Wachezaji
walioitwa ni makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi
(Mtibwa Sugar). Mabeki ni Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam),
Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum
(Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo
ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Jonas
Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba- U20),
Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu- U20).
Washambuliaji
ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan
Singano (Simba-U20), Simon Msuva (Moro United- U20), Thomas Ulimwengu (TP
Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Haruna Moshi (Simba) na John Bocco
(Azam).
Stars
inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro
itacheza mechi ya kirafiki nyumbani Mei 26 mwaka huu dhidi ya Malawi kabla
kuivaa Ivory Coast ugenini Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan.
Subscribe to:
Posts (Atom)