Monday, May 14, 2012

MWANAFUNZI AJIUA BAADA YA KUBAINI ANA MIMBA



Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Isange ,mkazi wa Isanu, Kata ya Isange, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya mnamo Mei 11 mwaka huu amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya kufungia ng'ombe muda mfupi baada ya kugundua alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu .

Afisa mtendaji wa Kata hiyo Bwana Anyambege Mwangomo amelitaja jina la marehemu kuwa ni Enitha Ndambo (15), ambaye alikuwa akiishi na bibi yake Bi Emelia Ndenga.

Marehemu alichukua hatua ya kujinyonga wakati mlezi wake akiwa katika kilabu cha pombe na kamba aliyotumia ilikuwa ndani ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi.

Polisi walifika  kwenye eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu  na kuupeleka katika Zahanati ya Isange kwa ajili ya kufanya upasuaji, ili kuthibitisha kama alikuwa na ujauzito na mara baada ya upasuaji waliwaruhusu wanakijiji kuzika mwili wa marehemu na kiumbe  kilichokuwa tumboni.

 Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari Kalinga kutoka katika Hospitali ya Serikali ya Makandana iliyopo wilayani humo, na zoezi la upimaji wa mimba wanafunzi ulifanywa na Daktari Anna Mwelevu wa Zahanati ya Isange..

Aidha katika uchunguzi uliofanywa umebaini aliyemsababishia ujauzito ni mwanafunzi wa shule hiyo  Alex Mwaitege, anayesoma kidato cha kwanza.


No comments:

Post a Comment