KATIKA ziara za viongozi wa kitaifa mikoani, zinaonekana kuwa na
mapungufu ya kuikosesha jamii kile kinacho kusudiwa kuwafikia.
Nalazimika kuyasema haya kufuatia dosari zilizojitokeza hivi
karibuni katika ufunguzi wa mbio za Mwenge Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Waziri mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyefungua mbio
hizo, lakini awali ya yote siku moja kabla ya kuanza kwa mbio hizo mnamo Mei 10
kwenye Ikulu ndogo ya mkoa wa Mbeya, kulitokea mkanganyiko ambao unaweza kuwa
chanzo cha kuinyima jamii haki yao ya msingi ya kupata habari.
Wanahabari ni muhimili wa nne katika serikali yetu ikitanguliwa na serikali
kuu,sheria na Bunge.
Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba wanaifikishia jamii
taarifa ya serikali kwa mujibu wa kanuni na maadili ya tasnia yao. Lakini kile
kilicho jitokeza siku hiyo ni sehemu ya mapungufu ambayo hayastahili kurudiwa.
Naamini kwamba, bajeti ya mkoa katika shughuli zote
kuhusiana na mbio za mwenge ilizingatia umuhimu na heshima ya mbio hizo ambazo
imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa watanzania tangu enzi za uhai wa mwasisi wa mbio hizo, Baba wa
Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Katika bajeti hiyo waandishi hawakupewa umuhimu wa
juu kama muhimili wa nne katika Taifa kwa kushindwa kuwaandalia usafiri wa
kutosha ili kufika katika maeneo mbali mbali aliyopangiwa kiongozi wa
serikali,Mh.Pinda
Naamini kwamba si wananchi wote ambao walikuwa na fursa ya
kufika alikotembelea Waziri mkuu,kwa
maana hiyo msaada wao mkubwa ulikuwa ni kupata taarifa kwa upana kupitia vyombo
vya habari.
Lakini kwa sababu idadi kubwa ya waandishi wa habari
walishindwa kuambatana na msafara wa Waziri mkuu, kutokana na kukosa usafiri, naamini hata katika upashaji
wa habari kwa jamii haukukidhi mahitaji ya wananchi hasa ukizingatia kwamba
tukio hilo la mbio za mwenge lilikuwa tukio kubwa la kitaifa mkoani humo.
Nadhani jambo la kwanza la kuzingatia lilikuwa ni
kuhakikisha wananchi wanapata ujmbe wa mbio hizo na agizo la kiongozi wao
kupitia vyombo vya habari ,hivyo basi waandishi walitakiwa kuandaliwa mapema mazingira
ya kuweza kufanya kazi zao kwa maslahi ya jamii.
Najua zipo sababu ambazo zinaweza kutolewa za kushindwa
kuwaandalia waandishi usafiri wa kuongozana na msafara wa Mh.Pinda kabla ya
kuzindua mbio hizo za mwenge alipo kuwa akienda kukagua Kiwanda cha Tanganyika
Packers,kiwanda cha Marumaru na kituo cha utafiti wa kilimo Uyole.
Lakini sababu hizo nadiliki kusema kuwa zinaweza kuwa
hazitalingana na umuhimu wa wanahabari katika kuitumikia jamii,moja kwa moja,
nadhani sababu ambazo zinaweza kutajwa
labda inaweza kuwa ni ufinyu wa bajeti kuhusu ugeni huo kwa maana kuwa
waandaji walihofu namna ya kuwawezesha (posho) waandishi.
Afisa habari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya anapaswa kujua
mahitaji ya wananchi kupitia waandishi wa habari,hili ndilo jambo la
msingi. Posho ni jambo la ziada japo si kweli kwamba ofisi ingeshindwa kufanya
hivyo ,kwa sababu hawakupewa umuhimu ndio sababu zilizo sababisha kuwepo
usumbufu wa usafiri.
Katika hili pia ni vema nikiwa wazi kwamba si waandishi wote
ambao wanategemea kupewa posho ili waweze kumudu kazi zao,hapana.Nia ya
mwandishi ni kupata habari na kuitangazia jamii kile ambacho kinaonekana kuwa
na umuhimu.
Na kwa kuwa waandishi ni kama daraja la kuwaunganisha viongozi na wananchi ,waandishi wanaitumia fursa kama
hiyo ili kuzitumikia pande zote mbili bila kujali posho.Jambo la msingi
wasinyanyapaliwe kwenye vyombo vya usafiri kama ilivyo tokea katika gari moja
aina ya Land cruiser lenye namba za usajili DFP 5950.
Dereva wa gari hilo na afisa habari wa ofisi ya mkuu wa mkoa kwa pamoja
walitoa lugha ambazo ziliwafedhehesha waandishi wakati wakitaka waandishi
wapungue ndani ya gari hilo,si mara ya kwanza waandishi kufanyiwa vituko na watu hao.
Kwa lugha za nyodo afisa habari huyo bila kuzingatia taaluma ya wanahabari aliwataka waandishi
wajitegemee usafiri kwa madai kuwa gari lililokuwa limeandaliwa kwa ajili yao
lilikuwa na uwezo wa kubeba waandishi kumi tu,ndani ya gari hilo kulikuwa
waandishi 11 lakini kutokana na kauli hizo baadhi ya waandishi waliamua kutelemka na kutawanyika
.
Hali hiyo imesababisha idadi kubwa ya waandishi kususia mbio
za mwenge huku kukiwa na malalamiko kwamba afisa habari amekuwa akiwatumia
marafiki zake wanahabari katika ziara za viongozi mkoani hapa na kitendo hicho
kimekuwa kikijirudia mara kwa mara.
Afisa habari kama kweli ni mwanataaluma wa habari, anapaswa
kubadilika ili kazi za viongozi zitangazwe kwa mapana na viongozi pia katika
ziara zao wajulishwe kwa mapana kero za wananchi kupitia tasnia ya habari ndani
ya ziara zao.
No comments:
Post a Comment