MSHAURI wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)Mkoa wa Mbeya,Bw. Eddo Mwamalala
amemtupia kombora Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Mbeya mjini Bw.John
Mwambigija kuwa siasa zake majukwaani ni
za uchochezi ambao haupaswi kufumbiwa macho.
Aliyasema hayo juzi katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Mbeya Peack mjini
hapa huku lawama hizo pia akilitupia Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa maelezo
kuwa Polisi wamekuwa wakimfumbia macho Bw.Mwambigija.
Bw.Mwamalala ambaye pia ni
mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa alisema kuwa,Bw.Mwambigija amekuwa akiyatumia
majukwaa kwa kutoa lugha za matusi na vichekesho kitendo ambacho kinaweza
kuhatarisha amani ya watanzania.
Katika mkutano huo
Bw.Mwamalala aliwaambia waandishi kwamba ,anashangazwa pia na ukimya wa katibu
mkuu wa Chadema Bw.Wilbrod Slaa kuendelea kukaa kimya bila ya kukemea tabia
hiyo ya Mwenyekiti huyo.
“ Nalishangaa sana jeshi la
polisi kwa kuendelea kumwangalia huyu mtu kauli anazotoa akiwa jukwaani ni za
uchochezi kwani lugha nyingi ni za matusi lakini polisi wamekuwa wakimwangalia hata
katibu mkuu Dr.Slaa amekaa kimya bila ya kukemea vitendo hivyo.’’Alisema
Aidha,aliongeza kuwa kutokana
na lugha za matusi na vichekesho visivyo na tija katika jamii amekuwa akishangiliwa na wananchi na kupata kiburi akijigamba
na kusema yeye ndiye aliye mpa madaraka Mbuge Joseph Mbilinyi na madiwani
kupitia tiketi ya Chadema mkoani hapa.
Mshauri huyo aliendelea
kuponda akisema kwamba Bw.Mwambigija ni
tatizo ndani ya Chadema maana kazi yake ni kuchekesha watu majukwaani, kutukana
na kuendelea kutoa matamko yasiyo na tija kwa wanachama huku akiwarubuni baadhi
wa wanawake akiomba magari yao kwa ajili ya misafara isiyo rasmi kwa ushawishi
wa kuwateua kwenye ubunge wa viti
maalumu.
.
Bw.Mwamalala alisema kuwa
Viongozi wa Chadema kuendelea kulifumbia macho suala la Mwambigija ni kukibomoa
chama badala ya kukijenga.
Alisema kutokana na mambo
hayo tayari Bw.Mwambigija ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee wa upako mnamo
Juni 4 mwaka huu atapandishwa kizimbani kusomewa shitaka kwa mara ya kwanza.
Bw.Mwambigija katika
mahojiano mafupi na majira kwa njia ya simu alikiri kwamba siku hiyo atasomewa
shitaka baada ya kushitakiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya
Chunya Bw.George Ntasha Katabi akituhumiwa kumtolea lugha za kashfa katika moja
ya mkutano.
No comments:
Post a Comment