Wednesday, July 25, 2012

SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LA MAREKANI KUINUA KILIMO CHA MPUNGA MBEYA

Na Steve Jonas

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Marekani liitwalo Bill &Melinda Gates Foundation hivi karibuni limeonesha nia ya kuwasaidia wakulima katika sekta ya kilimo cha Mpunga  mkoani Mbeya hapa .


Hayo yamefahamika wakati wa majadiliano kati ya kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply na shirika hilo yaliyofanyika Wilayani Mbarali mkoani hapa wiki iliyopita ,majadiliano ambayo yalilenga namna shirika hilo litakavyofanya shughuli hiyo hapa nchini kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya Mtenda.


Wajumbe watatu wa shirika la Bill & Melinda Gates Foundation linalo milikiwa na tajiri mkubwa Duniani,Bill Gates waliofika mkoani hapa akiwemo Afisa mipango na masoko ambapo walijadiliana na kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply kuwepo ushirikiano wa kuinua wakulima wa chini ili waweze kunufaika na kilimo chao.


Akizungumza katika kikao hicho, Afisa mipango mkuu wa shirika la Bill & Melinda Gates Foundation, Richard Rogers alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo hivyo wameona ni vyema wakasaidia  sekta hiyo hasa kwa wakulima wa chini.


Rogers alisema kwamba,msaada huo kwa ushirikiano na  kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply watawapelwekea mbegu  wakulima pamoja na baadhi ya mahitaji yao yanayohusu kilimo kama ikiwa ni pamoja na kuwajengea maghara ya kuhifadhia mazao yao.


Aidha, alisema kuwa kilimo cha Mpunga ni muhimu katika mahitaji ya jamii hivyo awali wakulima wanapaswa kupewa elimu itakayowawezesha kujua kanuni za kilimo cha kisasa kitakachowanufaisha kwa kutumia mbegu za kisasa ambazo watakuwa wakipelekewa na mashirika hayo.

 Wajumbe hao walisema kuwa wameridhishwa na maelezo yakinifu yaliyotolewa na Mtenda hivyo waliahidi mpango huo utatekelezwa ndani ya miezi minne kuanzia sasa baada ya kufikisha katika bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo.


Mshauri wa kampuni ya Mtenda, Emele Malinza alisema kampuni ya Mtenda Kyela Rice imeshaanza kuwapelekea wakulima hao mbegu pamoja na mahitaji mengine katika Wilaya za Mbozi, Kyela na Wilaya ya Mbeya.


Malinza alisema licha ya kuwapelekea mbegu hizo  pia kampuni inatoa mafunzo kwa wakulima hao ili kuwawezesha kuwa na upeo mpana wa kilimo  cha mpunga na mahindi.


 Mkurugenzi wa Mtenda Kyela Rice Supply, George Mtenda alisema kupitia kampuni yake wakulima watanufaika na kuondokana na adha ya kuuza mazao yao kwani  kampuni yake ndiyo itakayokuwa jihusisha na ununuzi wa mazao hayo na kutafuta soko.


Mtenda alisema toka aanzishe kampuni hiyo zao la mpungalimejipatia  soko kubwa katika nchi jirani za Malawi , Zambia  na Kenya.


Alisema utafiti uliofanywa na mshauri wake katika nchi hizo umebaini kuwa mchele unaouzwa nchi hizo ni mbegu ambayo yeye kupitia kampuni yake ndiyo iliyozalisha katika maeneo ya Kyela, Mbozi na Mbeya vijijini.



DR.SHEIN AMWAPISHA WAZIRI MPYA WA MIUNDO MBINU BAADA YA MWINGINE KUJIUZURU HIVI KARIBUNI ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, akimuapisha Rashid Seif Suleiman, kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, wakati wa  hafla fupi iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar jana
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, akimuapisha Sheikh Daudi Khamis Salim,  kuwa Kadhi wa Rufaa Pemba, wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar jana.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akisalimiana na Viongozi waliohudhuria katika hafla ya kiapo cha Waziri Mpya wa Miundombinu,Rashid Seif Suleiman, katika Ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar Jana.Picha na Ramadhan Otrhman,Ikulu

TAKWIMU ZA MATUMIZI KATIKA MASUALA YA INTANETI

TAKWIMU za matumizi ya Intaneti zimeonyesha kuwa Bara la Asia linaongoza kwa matumizi ya Intaneti. Huku Afrika ikishika nafasi ya 5 katika Mabara 7  ulimwenguni. Takwimu hizo ni za mwaka 2011 kwa mujibu wa INTERNET WORLD STATS.

MKUU WA MKOA WA MBEYA AMPA SIKU MBILI DC WA CHUNYA KUTOA TAARIFA ZA NYARAKA


MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro

Mkuu wa wilaya ya Chunya Mheshimiwa Deodatus Kinawiro.


MKUU wa mkoa wa Mbeya ,Abbas Kandoro ametoa muda wa siku mbili kwa mkuu wa wilaya ya Chunya,Deodatus Kinawiro kutoa taarifa za  upotevu wa nyaraka za miradi ya kilimo

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo nyaraka hizo zinazoelezwa kupotea ni za miradi ya kilimo yenye thamani ya jumla ya shilingi Milioni 408,659,706.

Katika kikao maalumu cha baraza kilicholenga kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa fedha za serikali(CAG) mkuu wa mkoa amehoji ni kwa nini nyaraka hizo zipotee na hakuna hatua zilizochukuliwa.

Amesema upo uwezekano mkubwa wa kuwa fedha hizo hazikutumika ipasavyo na ndiyo maana zimefichwa ili ukweli usibainike.

“Kwa nini zipotee?Inaonekana kuna shughuli hazikufanyika lakioni fedha zilitumika.Nataka ndani ya wiki hii nipate maelezo juu ya upotevu huo na ilikuwaje.Mkuu wa wilaya hakikisha mpaka alhamisi ya wiki hii uwe umeniletea maelezo ofisini kwangu na hawa madiwani wapewe taarifa kamili” alisisitiza.

Amezidi kuitaja idara ya kilimo kuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wake kutokana na taarifa mbalimbali zinazobainisha kuwepo kwa kasoro.

Mkuu huyo wa mkoa amesema pia kuna miradi ya kilimo ya kiasi cha shilingi 496 milioni haijakamilika licha ya serikali kutoa fedha zote na kuhoji ni kwa nini lakini swali hilo halikupata majibu kutokana na afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya hiyo kutohudhuria kikao hicho.

Aliendelea kusema kuwa pia ipo miradi yenye thamani ya shilingi milioni 73 haijakamilika na kuhoji kuna nini katika idara ya kilimo mpaka kuwe na uozo wa namna hiyo.

Aliwataka madiwani kutokubali kuburuzwa na wakuu wa idara na kukubali kupitisha taarifa za miradi kwenye vikao vyao pasipo kujiridhisha iwapo zinaendana na uhalisia wa miradi husika.

Kandoro pia amezishushia rungu idara za Maji, na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF)akisema pia zinatuhumiwa kwa kuwa na uozo wa matumizi mabovu ya fedha kama ilivyo kwenye kilimo na kuhitaji maelezo ya kina ni kwa nini.

Amesema katika idara ya maji kuna kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 4.6  zimetumika pasipo maelezo ya matumizi yake huku pia kiasi cha zaidi ya milioni tano zikionekana kuwa malipo ya kughushi.

Kwa upande wa TASAF amesema kuna kiasi kikubwa cha fedha  kimetumika kununua mafuta lakini hakuna nyaraka zinazoelekea mafuta yalinunuliwaje na kutumika vipi.

Friday, July 20, 2012

RAIS KIKWETE KUWASILI KESHO MKOANI MBEYA KWA ZIARA YA SIKU MOJA



KWA mara ya kwanza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anatarajia kutua kesho katika uwanja mpya wa ndege  wa Kimataifa wa Songwe uliopo wilaya ya Mbeya vijijini mkoani Mbeya kwa ajili ziara yake ya siku moja mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amesema kuwa Rais Kikwete atatua katika uwanja huo majira ya saa kumi za jioni na kuwaomba wananchi wa eneo hilo kujitokeza kwa ajili ya kumpokea.

Kandoro amesema kuwa katika maandalizi ya ujio wa Rais Kikwete mkoani Mbeya, kuna ndege ambayo ingefika leo katika uwanja huo kisha kesho Rais kutua na kupokelewa na viongozi wa mkoa wa Mbeya pamoja na wananchi.

Amesema Rais Kikwete akiwa mkoani Mbeya atapokea taarifa ya mkoa kisha atapumzika na kesho kutwa (Jumapili) ataelekea katika eneo la uzinduzi wa mradi mkubwa wa Majisafi na taka uliojengwa eneo la Swaya Jijini Mbeya ambako atapata taarifa za mradi huo akiwa na viongozi wa Serikali za Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya.

Baada ya hapo Rais Kikwete kutembelea mtambo wa kusafisha Majisafi na kutibu maji na kupata maelezo kisha kuzindua mradi huo na kutoa nasaha zake, msafara wake utaondoka na kurejea ikulu ndogo kisha ataelekea uwanja wa ndege Songwe kwa ajili ya kuondoka mkoani Mbeya.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi Wizara ya Maji Mhandisi Mary Mbowe, amesema kuwa mradi utakaozinduliwa na Rais Kikwete ni kati ya miradi mitatu mikubwa iliyokuwa ikitekelezwa katika miji mitatu Tanzania.

Amesema Mradi huo ni kati ya miradi mitatu mikubwa inayojulikana kwa jina la Regional Centers Program ambayo imetekelezwa katika Jiji la Mwanza, mkoa wa Iringa na sasa Jijini Mbeya na kugharimu Kiasi cha Shilingi Bilioni 80.
 
Mradi huo ulianza katikati ya mwaka 2009 na msimamizi mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na taka Jiji la Mbeya na katika uzinduzi utakaofanywa wageni mbalimbali watahudhuria.

Mbowe amewataja wageni hao kuwa ni pamoja na Kamishina wa Maendeleo ya nchi za Ulaya, Balozi wa Ujerumani, viongozi wa Wizara ya Maji, wawakilishi wa Wizara ya fedha na wawakilishi wa baadhi ya Mamlaka za Maji katika Miji Tanzania.

Uwanja wa ndege wa Songwe atakaotua Rais Jakaya Kikwete umekamilika katika sehemu ya kutua na kurukia ndege lakini umekwama katika ujenzi wa jengo la Abiria kutokana na Serikali kudaiwa zaisi ya Sh. Bilioni 5 na Mkandarasi aliyejenga uwanja huo kampuni ya Kundan Singh Construction Ltd ya nchini Kenya.

Mbali na kukwama kwa ujenzi wa Jengo hilo la abiria, pia hakuna jengo la kurushia ndege na sababu imetajwa kuwa Serikali imekwama kumlipa mkandarasi wa jengo hilo kampuni ya Beijing Construction Ltd, ambapo imeelezwa kuwa kutokana na Serikali kuchelewesha malipo hayo inaweza kuburuzwa mahakamani kwa kukiuka mikataba waliyoingia na wakandarasi hao.

Tuesday, July 17, 2012

KIKAO CHA MAADILI CHA WANACHAMA WA HABARI MKOANI MBEYA



 Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya Mbeya Press club Ndugu Mwakipesile akimkaribisha Mwenyekiti wa Mbeya Press Club 
 Mwenyekiti wa Mbeya Press Club Ndugu Christopher Nyanyembe  akifungua kikao cha maadili 
 Mmoja wa waandishi akichukua tukio



 Waandishi wakifuatilia kwa umakini kikao 
Picha ya pamoja ya wana Mbeya Press club baada ya kikao

Friday, July 13, 2012

KANISA LA UINJILISTI MBALIZI LAPONGEZWA

BAADHI YA VIONGOZI WA KANSA LA UINJILISTI LA MBALIZI MKOANI MBEYA


KATIKATI NI MKUU WA WILAYA YA MBEYA DR, NORMAN SIGALLA AKIONESHA JINSI YA KUJIPANGA KUPIGA PICHA NA KUSHOTO NI KAMANDA MKUU WA KIKOSI KAZI CHA KALULUNGA blog.


 WAHITIMU WA CHUO CHA UUGUZI MBALIZI MBEYA WAKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA KWENYE MAHAFALI YA PILI KATIKA CHUO HICHO.


SERIKALI imelipongeza Kanisa la Uinjilisti Tanzania lenye makao yake makuu mjini Mbalizi wilaya ya Mbeya mkoani hapa kwa kuanzisha chuo cha uuguzi, ukunga na maabara.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Mbeya Dr. Norman Sigalla wakati wa maafali ya pili ya chuo cha kanisa hilo kilichopo eneo la Ifisi karibu na Hospitali teuele ya wilaya hiyo ambayo nayo inamilikiwa na Kanisa hilo.

Dr. Sigalla alisema kuwa kanisa hilo limekuwa mfano wa kuigwa wa taasisi zingine zisizokuwa za Serikali kwa kutoa taaluma kwa watanzania ambapo katika mahafali hayo wahitimu 117 walitunukiwa vyeti katika fani za uuguzi na maabara.

Aliwasihi wahitimu kutumia vema taaluma zao na viapo huku akisema kuwa wasijiingize katika migomo ya kuwakomoa wagonjwa kutokana na matatizo ya waajiri wao na kwamba migomo inadhihilisha upeo wa mwisho wa kufikiri kwa mwanataaluma na ni kinyume na dini zote zilizopo hapa nchini.

Sanjali na hayo aliziasa taasisi zote za binafsi zinazoanzisha vyuo vya taaluma mbalimbali katika wilaya yake kushirikiana na Serikali za wilaya wakiwemo wakuu wa wilaya ambao ni kiungo na wizara.

Naye Mkuu wa kikosi cha Hospitali ya Jeshi Mbalizi Mbeya Col. Dr. Janga alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho na kutoa wahitimu wa fani hizo ni ukombozi kwa taifa kutokana na Taifa kuwa na uhaba wa wataalam wa maabara.

‘’Kwanza kabisa nampongeza sana Mkurugenzi wa Maendeleo wa kanisa hili la Uinjilisti kwa kuanzisha chuo hiki hususani suala la wataalam wa maabara na hata Hospitali hii ya Mbalizi Ifisi ilisaidia sana kuwahudumia wagonjwa wakati wa mgomo wa Madaktari na huu ni mfano wa kuigwa kwa wazalendo’’ alisema Col. Dr, Janga.

Mkurugenzi wa Maendeleo wa kanisa hilo la Uinjilisti Tanzania Mchungaji Marcus Lehner alisema kuwa ataendelea kushirikiana na wapenda maendeleo wote kwa kusaidia hasa vijana kwa kuendeleza vyuo vya ufundi vinavyomilikiwa na kanisa hilo kwa ajili ya kuwaandaa vijana kujiajiri wenyewe pindi wanapohitimu.

‘’Tutaendeleza vyuo vya ufundi maana ni msingi wa ajira kwa vijana na mapungufu yaliyokuwepo kwa upande wa chuo cha uuguzi yote tumejipanga kuyatatua mara moja ikiwemo kuongeza vifaa vya mafunzo ikiwemo darubini, safe cabinete, thermometer, vitabu na walimu wa kudumu’’ alisema Mch. Lehner.

Kwa upande wa wahitimu wa mahafali hayo ya pili, kupitia risala yao iliyosomwa na Shukran Moses na Adolf Mtweve, walisema kuwa wamepata taaluma yao na kuelewa kutokana na chuo hicho kuwa na maabara ya kufanyia mazoezi kwa vitendo, Hospitali ambayo imewasaidia sana na kuwa moja ya darasa lao na kupata elimu ya Kompyuta.

Thursday, July 12, 2012

MAFUNZO YA HABARI ZA UCHOKONOZI YANAWEZA KULIKWAMUA TAIFA KATIKA VITENDO VYA UFISADI

MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI  KATKA MFULULIZO WA MAFUNZO YA HABARI ZA UCHOKONOZI KWENYE UKUMBI WA HOTEL YA MKURU AMBAPO MGENI KATTBU TAWALA MKOA WA MBEYA MARIAM MTUNGUJA AMEYAFUNGUA RASMI KWA KUWAPONGEZA WAANDISHI HAO KWA KUJIONGEZEA UWEZO ZAIDI KWA MAFUNZO HAYO

KATIKA HOTUBA HIYO AMEZUNGUMZIA MENGI IKIWEMO WATU KUTOPENDA KUAMBIWA UKWELI KWAKUA MTU HUPENDA KUJIANGALIA MBELE LAKINI NYUMA HAWAWEZI KIJIONA" NATAKA KUSEMA MWANDISHA WA HABARI NI KIOO CHA JAMII HIVYO NI VEMA KUWA NA WAANDISHI WENYE UWEZO NA UWELEWA" AMESEMA MTUNGUJA

PIA AMEWATAKA WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI KUAJIRI WAANDI WA HABARI WALIOSOMEA TASINIA HII ILI KUONDONGOKANA MIGONGANO YA INAYO SABABISHWA NA WAANDISHI WASIO NA TAALUMA HII

MWISHO AMETOA WITO WA KUSHIRIKIANA VEMA NA WAANDISHI PIA VYOMBO VYA HABARI ATATOA USHILIKIANO WA KUTOSHA KWAO.


MWENYEKITI WA MBEYA PRESS CLUB CHISTOPHA NYENYEMBE AKIMKARIBISHA MRATIBU WA (UTPC) VICTOR MALEKO AMKARIBISHE MGENI RASMI AZUNGUMZE  NA WAANDISHI WA HABARI

 MRATIBU WA UMOJA WA CLUB ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA (UTPC) VICTOR MALEKO AKIMUELEZA MACHACHE MGENI RASMI JUU YA MPANGO WA KUWAWEZESHA KITAALUMA WAANDISHI WA HABARI NA KISHA KUMKARIBISHA AZUNGUMZE NAO.

                                               MGENI RASMI MARIAM MTUNGUJA

KATIBU TAWALA MKOA WA MBEYA MARIAM MTUNGUJA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

                             WAANDISHI WA HABARI WAKISIKILIZA KWA MAKINI

  MKUFUNZI AKIMSHUKURU MGENI RASMI KWA HOTUBA YAKE KWA WAANDISHI

PICHA YA PAMOJA YA WAANDISHI WA HABARI WANAOHUDHURIA MAFUNZO HAYO

                      MGENI RASMI ANAAGANA NA WAANDISHI NA KUONDOKA.

WAANDISHI WA HABARI MBEYA WAKIWA KWENYE MAFUNZO YA HABARI ZA UCHUNGUZI

JUMLA YA WAANDISHI WA HABARI (20) MKOANI  MBEYA WAANZA KUPATIWA MFUNZO YA SIKU SITA YA UANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGU AMBAZO ZITAWAWEZESHA KUFANYA KAZI ZAO KWA UMAKINI NA KUIBUA MAMBO MBALIMBALI YALIOJIFICHA KATIKA JAMII

MAFUNZO HAYO YANAFANYIKA KATIKA HOTEL YA  MKURU ILIYOPO KATIKA ENEO LA SOWETO MJINI HAPA NA KUFADHILIWA  NA UMOJA CLUB ZA  WAANDISHI WA HABARI TANZANIA (UTPC)

MAFUNZO HAYO YANAFUNGULIWA MAY 15 MWAKA HUU NA KATIBU TAWALA MKOA WA MBEYA MARIAM MTUNGUJA.

BAADHI YA WAANDISHI WALIO HUDHURIA MAFUNZO HAYO WAKIMSIKILIZA KWA MAKINI MKUFUNZI WA MAFUNZO HAYO.

 MWENYEKITI WA MBEYA PRESS CLUB CHRISTOPHA NYENYEMBE AKIELEZEA JAMBO KABLA YA KUANZA MAFUNZO HAYO

NAYE MKUFUNZI WA MAFUNZO HAYO FILI KARASHANI KUTOKA DAR-ES-SALAM AKISISITIZA JAMBO KABLA YA KUANZA MAFUNZO HAYO.

BAADHI YA WANDISHI WAKIBADILISHANA MAWAZO KABLA YA KUANZA MAFUNZO KATIKA UKUMBI ULIOANDALIWA

                MKUFUNZI KARASHANI AKIENDELEA NA MAFUNZO KWA WAAMDISHI

WAANDISHI WAKIWA KATIKA KUTEKELEZA MOJA YA MAJUKUMU WALIYOPEWA NA MKUFUNZI

              HII NDIYO HOTEL SEHEMU AMBAYO YANAENDESHWA MAFUNZO HAYO

Tuesday, July 10, 2012

MACHIFU MBEYA KUHESHIMU MIPAKA YA UTAWALA WAO



MUUNGANO wa Jamii Tanzania (MJATA) hivi karibuni umewataka machifu mkoani hapa kuheshimu taratibu na mipaka ya utawala wao ili kujenga imani kwa jamii inayo wazunguka.

Hayo yalisemwa katika mkutano wa Machifu chini ya MJATA uliofanyika Julai 5 mwaka huu huko Igawilo jijini Mbeya.

Chifu aliye jitambulisha kwenye mkutano huo kwa jina la Julius Lyoto,alisema kuwa ili kujenga mahusiano mema na jamii machifu wanatakiwa kubadilika na kujenga misingi ya ushirikiano , kuheshimu taratibu na mipaka ya utawala.

Lyoto alitolea mfano wa machifu wa zamani akiwemo marehemu Chifu Adam Sapi kwamba walikuwa na utamaduni wa kutembeleana na kujadili maadili ya utamaduni,mila na desturi ili kuijenga jamii katika misingi hiyo.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa maadili ya Muungano wa Jamii Tanzania ambaye pia alijitambulisha kuwa ni katibu wa machifu Wilaya ya Mbarali,Ibrahim Mwalalila alisema kuwa kusudi la mkutano huo ni kujua kero za wanachama wa MJATA.

Alisema kwamba,muungano huo umekuwa ukipoteza wanachama wake kwa idadi kubwa na kuwepo mahudhurio finyu kwenye mikutano kinyume na mahudhurio ya awali hali ambayo imesababisha viulizo kwa viongozi.

Chifu Rocket Mwanshinga alipata fursa ya kuzungumza na kubainisha kero zinazo changia wanachama hao kujiondoa kwenye muungano huo kuwa ni uongozi mbaya uliopo madarakani,kutohusishwa kwenye maamuzi ya chama hali inayowafanya wajione wanaburuzwa.

Kero zingine alizo zitaja ni kutotekeleza ahadi za pesa ili kuendesha shughuli za utunzaji wa mazingira na kuhifadhi misitu majukumu ambayo ni miongoni mwa wajibu wa machifu hao.

Chifu Mwanshinga alisema kwamba , machifu pia wamekuwa wakidhalilishwa na uongozi uliopo madarakani kwa kitendo cha kupita maofisini kuomba misaada kwa visingizio kuwa ni agizo la machifu kitendo ambacho si cha kweli.

‘Machifu sio omba omba,wala hatuna tabia hiyo lakini tunashangazwa na tabia hiyo,mbaya zaidi hatusomewi hata hayo mapato badala yake tunmasomewa matumizi huku tukiendelea kuchangishwa pesa’.Alisema

Baada ya mkutano huo mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kumpata mwenyekiti wa MJATA ,Shayo Masoko Soja ambaye alitajwa kwenye mkutano kuwa anawaburuza machifu hao kwenye uongozi wake.

Muungano huo ulianzishwa na kusajiliwa mwaka 2009 ambao ulianzishwa kwa kusudi la kupambana na kuzuia maovu katika jamii yakiwemo ya upagaji wa nondo,mauaji ya maalbino na mengine mengi.


Wednesday, July 4, 2012

HALMASHAURI MBILI MBEYA ZAINGIA KWENYE BIFU LA ARDHI

Na Steve Jonas

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya zimeingia kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi baada ya Jiji kujiongezea eneo katika Mlima Iwambi bila ya makubaliano na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.


Habari zinasema kwamba,Halmashauri ya Jiji la Mbeya limekiuka taratibu za mipaka ya ardhi inayo zitenganisha Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na jiji kwa kupora eneo la ukubwa wa ekari 600 katika mlima maarufu kwa jina la Iwambi.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Anderson Kabenga ofisini kwake alisema kuwa jiji limepora ekari hizo ambazo ni ardhi ya wananchi wake bila ya ridhaa yao kwa maelezo kuwa hakuna kikao walicho keti na Halmashauri ya Jiji ili kumega eneo hilo kwaajili ya matumizi ya wananchi wa Halmashauri ya Jiji.


Alisema kuwa sababu zinazo elezwa na uongozi wa Jiji zinadai kwamba Jiji lilifanya hivyo kwa kusudi la kupanua Jiji kitendo ambacho Kabenga alikitolea ufafanuzi kuwa kama ni upanuzi wa Jiji siyo tatizo lakini zingefuatwa taratibu za kisheria kwa pande zote mbili kuketi pamoja na kukubaliana kuhusu suala hilo.


Kabenga alisema kwamba,Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya baada ya kubaini uporwaji wa ardhi hiyo kiliitishwa kikao maaluma cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambacho kiliamua kuwatuma wajumbe wanne kwa Waziri mwenye dhamana ili Waziri huyo afute tangazo Na237 la Desemba 12 mwaka 2005 lililotoka kwenye Gazeti la serikali.

Aidha ,alidokeza kuwa kusudi la Jiji kupora eneo hilo si katika kupanua ukubwa wa Jiji pekee bali lililenga pia kupora vyanzo vya Mapato kwa maelezo kuwa eneo hilo la ekari 600 lililopo katika mlima Iwambi lina madini hivyo Jiji lilitaka kujipatia mapato kupitia eneo hilo ambalo ni eneo halali la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya

Habari za uchunguzi na zinazo thibitisha kuwa eneo hilo lina madini ,zimebaini kuwa kuna kampuni moja inayojihusisha na uchimbaji wa Madini imewaandikia Barua wakazi wa eneo hilo inayo wataka wahame makazi yao lakini wananchi wameweka mgomo kwani hawana taarifa za serikali sambamba na kufidiwa.

Hata hivyo,ofisi ya mkurugenzi wa Jiji haina taarifa za wanachi kutakiwa wahame maeneo yao kwa maelezo kuwa hakuna mtu au kampuni inayo miliki ardhi hiyo ambayo ni mali ya serikali.

WANANCHI MBEYA WAITIKISA SERIKALI

Na Steve Jonas

WANANCHI wa kata ya Isongole katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya wiki iliyopita waliweka vizuizi kwenye barabara ya kutoka Uyole kwenda Tukuyu ili kuishinikiza serikali itatue kero zao .

Vizuizi hivyo vilivyokuwa vimetawala katika barabara hiyo ni pamoja na uchomaji wa magurudumu kati kati ya barabara,mawe , magogo na makundi ya watu wa rika mbalimbali hali  iliyosababisha kukwama kwa huduma za usafiri na huduma nyingine za kijamii.

Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, kwenye maeneo ya tukio hilo,wananchi walichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo vya kifisadi vinavyofanywa kwenye kizuizi cha kutoza ushuru wa mazao kilichopo eneo la Kijiji cha Namba Wani.

Daud Gabriel mkazi wa kijiji cha Ndaga alisema kuwa hatua ya wananchi kuzuia barabara hiyo ilitokana na kero za muda mrefu ambazo zimekuwa zikifanywa na watoza ushuru wa mazao ambao inadaiwa kwamba kuna ubaguzi unafanywa katika zoezi hilo.

Alisema kuwa kusudi la wananchi ni kutaka uwiano wa ushuru katika mazao yote kinyume na hivi sasa ambapo viazi hutozwa kiasi cha shilingi 120,000 kwa tani tano wakati ndizi na miwa hutozwa kiasi cha shilingi 30,000 kwa tani tano.

Naye Herman Ulaya alisema kwamba watoza ushuru hao wanatumia ubabe kwa kuwanyanyasa wananchi na kuwadhalilisha huku akitolea mfano kwake kuwa aliwahi kukamatwa akiwa na mzigo wa kuni kwaajili ya matumizi ya nyumbani.

Alisema alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Kiwira na baadae alitozwa shilingi 160,000 kwaajili ya usumbufu kwa watoza ushuru kitendo ambacho alikielezea kuwa hakikuwa cha halali.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ndaga,Paulos Said Zambi alizitaja kero za msingi kwa wananchi kuwa ni wananchi wanataka kutozwa ushuru kwa gharama zinazofanana bila kujali ni aina gani ya bidhaa.

Kero zingine ni kuitaka Halmashauri kuvipatia vijiji kiasi cha mapato yanayokusanywa,kulihamisha geti kwenda mpakani eneo la Isyonje na kuondoa ushuru wa mbegu zinazo pelekwa mashambani.

Zambi alisema kuwa wananchi wa vijiji nane vya kata ya Isongole wamekuwa wakitaabika kwa kipindi kirefu ambapo viongozi wamekuwa wakifumbia macho kilio chao hata kufikia hatua hiyo ya kuandamana na kufunga barabara ili viongozi waweze kujua umuhimu wa kilio hicho.

Wananchi hao waliandamana mnamo Julai 2 mwaka huu majira ya asubuhi na kusababisha vyombo vya usafiri kushindwa kufanya safari hali iliyosababisha msongamano wa magari hadi majira ya saa 11 jioni.

Askari wa jeshi la Polisi kutoka katika kituo cha kati jijini hapa walifika saa 8:40 wakiwa na silaha za moto na kufyatua hewani risasi mbili ambazo hazikufanikiwa kuwatawanya wananchi ambao walikuwa wakisikika wakisema ‘tunataka haki’.

Dakika 30 baadae mkuu wa mkoa wa Mbeya ,Abbas Kandoro akiongozana na kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya ,walifika katika kijiji cha Ndaga ambako Kandoro aliweza kutoa tamko la kuwataka wananchi hao wasitoe ushuru hadi hapo Halmashauri ya Wilaya itakapo kaa na kufika mwafaka.

Baada ya kauli hiyo ya mkuu wa mkoa iliyotamkwa majira ya saa 11jioni ,wananchi waliamua kuondoa vizuizi barabarani bila kushurutishwa na hali ilikuwa shwari mbali ya zoezi hilo kuwa kero kwa wasafiri ambao walilazimika kukwama wakati zoezi hilo likiendelea.