Wednesday, July 25, 2012

SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LA MAREKANI KUINUA KILIMO CHA MPUNGA MBEYA

Na Steve Jonas

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Marekani liitwalo Bill &Melinda Gates Foundation hivi karibuni limeonesha nia ya kuwasaidia wakulima katika sekta ya kilimo cha Mpunga  mkoani Mbeya hapa .


Hayo yamefahamika wakati wa majadiliano kati ya kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply na shirika hilo yaliyofanyika Wilayani Mbarali mkoani hapa wiki iliyopita ,majadiliano ambayo yalilenga namna shirika hilo litakavyofanya shughuli hiyo hapa nchini kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya Mtenda.


Wajumbe watatu wa shirika la Bill & Melinda Gates Foundation linalo milikiwa na tajiri mkubwa Duniani,Bill Gates waliofika mkoani hapa akiwemo Afisa mipango na masoko ambapo walijadiliana na kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply kuwepo ushirikiano wa kuinua wakulima wa chini ili waweze kunufaika na kilimo chao.


Akizungumza katika kikao hicho, Afisa mipango mkuu wa shirika la Bill & Melinda Gates Foundation, Richard Rogers alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo hivyo wameona ni vyema wakasaidia  sekta hiyo hasa kwa wakulima wa chini.


Rogers alisema kwamba,msaada huo kwa ushirikiano na  kampuni ya Mtenda Kyela Rice Supply watawapelwekea mbegu  wakulima pamoja na baadhi ya mahitaji yao yanayohusu kilimo kama ikiwa ni pamoja na kuwajengea maghara ya kuhifadhia mazao yao.


Aidha, alisema kuwa kilimo cha Mpunga ni muhimu katika mahitaji ya jamii hivyo awali wakulima wanapaswa kupewa elimu itakayowawezesha kujua kanuni za kilimo cha kisasa kitakachowanufaisha kwa kutumia mbegu za kisasa ambazo watakuwa wakipelekewa na mashirika hayo.

 Wajumbe hao walisema kuwa wameridhishwa na maelezo yakinifu yaliyotolewa na Mtenda hivyo waliahidi mpango huo utatekelezwa ndani ya miezi minne kuanzia sasa baada ya kufikisha katika bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo.


Mshauri wa kampuni ya Mtenda, Emele Malinza alisema kampuni ya Mtenda Kyela Rice imeshaanza kuwapelekea wakulima hao mbegu pamoja na mahitaji mengine katika Wilaya za Mbozi, Kyela na Wilaya ya Mbeya.


Malinza alisema licha ya kuwapelekea mbegu hizo  pia kampuni inatoa mafunzo kwa wakulima hao ili kuwawezesha kuwa na upeo mpana wa kilimo  cha mpunga na mahindi.


 Mkurugenzi wa Mtenda Kyela Rice Supply, George Mtenda alisema kupitia kampuni yake wakulima watanufaika na kuondokana na adha ya kuuza mazao yao kwani  kampuni yake ndiyo itakayokuwa jihusisha na ununuzi wa mazao hayo na kutafuta soko.


Mtenda alisema toka aanzishe kampuni hiyo zao la mpungalimejipatia  soko kubwa katika nchi jirani za Malawi , Zambia  na Kenya.


Alisema utafiti uliofanywa na mshauri wake katika nchi hizo umebaini kuwa mchele unaouzwa nchi hizo ni mbegu ambayo yeye kupitia kampuni yake ndiyo iliyozalisha katika maeneo ya Kyela, Mbozi na Mbeya vijijini.



No comments:

Post a Comment