KWA mara ya kwanza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anatarajia kutua kesho katika uwanja mpya
wa ndege wa Kimataifa wa Songwe uliopo wilaya ya Mbeya vijijini mkoani
Mbeya kwa ajili ziara yake ya siku moja mkoani hapa.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake leo, Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
amesema kuwa Rais Kikwete atatua katika uwanja huo majira ya saa kumi za jioni
na kuwaomba wananchi wa eneo hilo kujitokeza kwa ajili ya kumpokea.
Kandoro amesema
kuwa katika maandalizi ya ujio wa Rais Kikwete mkoani Mbeya, kuna ndege ambayo
ingefika leo katika uwanja huo kisha kesho Rais kutua na kupokelewa na viongozi
wa mkoa wa Mbeya pamoja na wananchi.
Amesema Rais
Kikwete akiwa mkoani Mbeya atapokea taarifa ya mkoa kisha atapumzika na kesho
kutwa (Jumapili) ataelekea katika eneo la uzinduzi wa mradi mkubwa wa Majisafi
na taka uliojengwa eneo la Swaya Jijini Mbeya ambako atapata taarifa za mradi
huo akiwa na viongozi wa Serikali za Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya.
Baada ya hapo Rais
Kikwete kutembelea mtambo wa kusafisha Majisafi na kutibu maji na kupata
maelezo kisha kuzindua mradi huo na kutoa nasaha zake, msafara wake utaondoka
na kurejea ikulu ndogo kisha ataelekea uwanja wa ndege Songwe kwa ajili ya
kuondoka mkoani Mbeya.
Kwa upande wake
Mkurugenzi msaidizi Wizara ya Maji Mhandisi Mary Mbowe, amesema kuwa mradi
utakaozinduliwa na Rais Kikwete ni kati ya miradi mitatu mikubwa iliyokuwa
ikitekelezwa katika miji mitatu Tanzania.
Amesema Mradi huo
ni kati ya miradi mitatu mikubwa inayojulikana kwa jina la Regional Centers
Program ambayo imetekelezwa katika Jiji la Mwanza, mkoa wa Iringa na sasa
Jijini Mbeya na kugharimu Kiasi cha Shilingi Bilioni 80.
Mradi huo ulianza
katikati ya mwaka 2009 na msimamizi mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji
safi na taka Jiji la Mbeya na katika uzinduzi utakaofanywa wageni mbalimbali
watahudhuria.
Mbowe amewataja
wageni hao kuwa ni pamoja na Kamishina wa Maendeleo ya nchi za Ulaya, Balozi wa
Ujerumani, viongozi wa Wizara ya Maji, wawakilishi wa Wizara ya fedha na
wawakilishi wa baadhi ya Mamlaka za Maji katika Miji Tanzania.
Uwanja wa ndege wa
Songwe atakaotua Rais Jakaya Kikwete umekamilika katika sehemu ya kutua na
kurukia ndege lakini umekwama katika ujenzi wa jengo la Abiria kutokana na
Serikali kudaiwa zaisi ya Sh. Bilioni 5 na Mkandarasi aliyejenga uwanja huo
kampuni ya Kundan Singh Construction Ltd ya nchini Kenya.
Mbali na kukwama
kwa ujenzi wa Jengo hilo la abiria, pia hakuna jengo la kurushia ndege na
sababu imetajwa kuwa Serikali imekwama kumlipa mkandarasi wa jengo hilo kampuni
ya Beijing Construction Ltd, ambapo imeelezwa kuwa kutokana na Serikali
kuchelewesha malipo hayo inaweza kuburuzwa mahakamani kwa kukiuka mikataba
waliyoingia na wakandarasi hao.
No comments:
Post a Comment