Wednesday, July 4, 2012

HALMASHAURI MBILI MBEYA ZAINGIA KWENYE BIFU LA ARDHI

Na Steve Jonas

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya zimeingia kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi baada ya Jiji kujiongezea eneo katika Mlima Iwambi bila ya makubaliano na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.


Habari zinasema kwamba,Halmashauri ya Jiji la Mbeya limekiuka taratibu za mipaka ya ardhi inayo zitenganisha Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na jiji kwa kupora eneo la ukubwa wa ekari 600 katika mlima maarufu kwa jina la Iwambi.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Anderson Kabenga ofisini kwake alisema kuwa jiji limepora ekari hizo ambazo ni ardhi ya wananchi wake bila ya ridhaa yao kwa maelezo kuwa hakuna kikao walicho keti na Halmashauri ya Jiji ili kumega eneo hilo kwaajili ya matumizi ya wananchi wa Halmashauri ya Jiji.


Alisema kuwa sababu zinazo elezwa na uongozi wa Jiji zinadai kwamba Jiji lilifanya hivyo kwa kusudi la kupanua Jiji kitendo ambacho Kabenga alikitolea ufafanuzi kuwa kama ni upanuzi wa Jiji siyo tatizo lakini zingefuatwa taratibu za kisheria kwa pande zote mbili kuketi pamoja na kukubaliana kuhusu suala hilo.


Kabenga alisema kwamba,Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya baada ya kubaini uporwaji wa ardhi hiyo kiliitishwa kikao maaluma cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambacho kiliamua kuwatuma wajumbe wanne kwa Waziri mwenye dhamana ili Waziri huyo afute tangazo Na237 la Desemba 12 mwaka 2005 lililotoka kwenye Gazeti la serikali.

Aidha ,alidokeza kuwa kusudi la Jiji kupora eneo hilo si katika kupanua ukubwa wa Jiji pekee bali lililenga pia kupora vyanzo vya Mapato kwa maelezo kuwa eneo hilo la ekari 600 lililopo katika mlima Iwambi lina madini hivyo Jiji lilitaka kujipatia mapato kupitia eneo hilo ambalo ni eneo halali la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya

Habari za uchunguzi na zinazo thibitisha kuwa eneo hilo lina madini ,zimebaini kuwa kuna kampuni moja inayojihusisha na uchimbaji wa Madini imewaandikia Barua wakazi wa eneo hilo inayo wataka wahame makazi yao lakini wananchi wameweka mgomo kwani hawana taarifa za serikali sambamba na kufidiwa.

Hata hivyo,ofisi ya mkurugenzi wa Jiji haina taarifa za wanachi kutakiwa wahame maeneo yao kwa maelezo kuwa hakuna mtu au kampuni inayo miliki ardhi hiyo ambayo ni mali ya serikali.

No comments:

Post a Comment