MUUNGANO wa Jamii Tanzania (MJATA) hivi karibuni umewataka
machifu mkoani hapa kuheshimu taratibu na mipaka ya utawala wao ili kujenga
imani kwa jamii inayo wazunguka.
Hayo yalisemwa katika mkutano wa Machifu chini ya MJATA
uliofanyika Julai 5 mwaka huu huko Igawilo jijini Mbeya.
Chifu aliye jitambulisha kwenye mkutano huo kwa jina la
Julius Lyoto,alisema kuwa ili kujenga mahusiano mema na jamii machifu
wanatakiwa kubadilika na kujenga misingi ya ushirikiano , kuheshimu taratibu na
mipaka ya utawala.
Lyoto alitolea mfano wa machifu wa zamani akiwemo marehemu
Chifu Adam Sapi kwamba walikuwa na utamaduni wa kutembeleana na kujadili
maadili ya utamaduni,mila na desturi ili kuijenga jamii katika misingi hiyo.
Katika mkutano huo, mwenyekiti wa maadili ya Muungano wa
Jamii Tanzania ambaye pia alijitambulisha kuwa ni katibu wa machifu Wilaya ya
Mbarali,Ibrahim Mwalalila alisema kuwa kusudi la mkutano huo ni kujua kero za
wanachama wa MJATA.
Alisema kwamba,muungano huo umekuwa ukipoteza wanachama wake
kwa idadi kubwa na kuwepo mahudhurio finyu kwenye mikutano kinyume na
mahudhurio ya awali hali ambayo imesababisha viulizo kwa viongozi.
Chifu Rocket Mwanshinga alipata fursa ya kuzungumza na
kubainisha kero zinazo changia wanachama hao kujiondoa kwenye muungano huo kuwa
ni uongozi mbaya uliopo madarakani,kutohusishwa kwenye maamuzi ya chama hali
inayowafanya wajione wanaburuzwa.
Kero zingine alizo zitaja ni kutotekeleza ahadi za pesa ili
kuendesha shughuli za utunzaji wa mazingira na kuhifadhi misitu majukumu ambayo
ni miongoni mwa wajibu wa machifu hao.
Chifu Mwanshinga alisema kwamba , machifu pia wamekuwa
wakidhalilishwa na uongozi uliopo madarakani kwa kitendo cha kupita maofisini
kuomba misaada kwa visingizio kuwa ni agizo la machifu kitendo ambacho si cha
kweli.
‘Machifu sio omba omba,wala hatuna tabia hiyo lakini
tunashangazwa na tabia hiyo,mbaya zaidi hatusomewi hata hayo mapato badala yake
tunmasomewa matumizi huku tukiendelea kuchangishwa pesa’.Alisema
Baada ya mkutano huo mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa
kumpata mwenyekiti wa MJATA ,Shayo Masoko Soja ambaye alitajwa kwenye mkutano
kuwa anawaburuza machifu hao kwenye uongozi wake.
Muungano huo ulianzishwa na kusajiliwa mwaka 2009 ambao
ulianzishwa kwa kusudi la kupambana na kuzuia maovu katika jamii yakiwemo ya
upagaji wa nondo,mauaji ya maalbino na mengine mengi.
No comments:
Post a Comment