Saturday, August 18, 2012

ASSANGE WA AUSTRALIA KUPELEKWA MAREKANI



Australia imethibitisha hii leo kuwa ina inajiandaa juu ya uwezekano wa kumpeleka Marekani raia wake Julian Assange. 
Matayarisho hayo yanafanywa na ubalozi wa nchi hiyo nchini Marekani ambao hata hivyo umesema kuwa ni mpango utakaotegeme mambo mengine kadhaa. Waziri wa Biashara wa Australia Craig Emerson amesema kuwa ubalozi huo mjini Washington unajiandaa na uwezekano wa kumsalimisha Assange mikononi mwa Marekani na kusema kuwa jambo hilo ni kitu cha kawaida kwenye masuala ya kidiplomasia. Katika mazungumzo yake na kituo cha televisheni cha ABC, Emerson amesema kuwa ubalozi huo unatimiza wajibu wake wa kuishauri serikali kama itaona kuna haja ya kumpeleka Assange nchini humo. Taarifa hiyo inafuatia kuenea kwa ripoti kuwa ubalozi wa Australia mjini Washington unahisi Marekani inamuwinda Assange.  Assange alipewa  hifadhi katika ubalozi wa Equador jijini London mnamo mwezi Juni ili kukwepa kusafirishwa kutoka Uingereza hadi Sweden kuhusiana na madai ya unyanyasaji kingono. Mawaziri wa Mambo ya Kigeni kutoka Shirikisho la Mataifa ya Amerika wanatarajiwa kukutana mjini Washington wiki ijayo kujadiliana kuhusu mgogoro huo wa kidiplomasia.

No comments:

Post a Comment