WASTAAFU wa serikali mkoani Mbeya hivi karibuni wamelalamika
juu ya ucheleweshwaji wa malipo yao ya pensheni ambayo kwa kawaida wanalipwa
kila baada ya miezi mitatu.
Mmoja wa wastaafu hao aliyejitambulisha kwa jina la Martin
Mwakalinga ,alisema kuwa kumekuwepo usumbufu wa kulipwa pensheni hizo tofauti
na agizo la serikali linaloelezea wastaafu hao walipwe pesa za miezi mitatu kwa
wakati mmoja.
Alisema kwamba,agizo hilo halijatekelezwa kwani kuna wakati
wanalipwa malipo ya miezi miwili kwa wakati mmoja badala ya miezi mitatu huku
akitolea mfano kuwa malipo ya mwezi julai 31 hadi Desemba mwaka jana hadi sasa
hawajalipwa.
Aidha ,Mwakalinga ambaye alikuwa mtumishi katika idara ya
Elimu na kustaafu mwaka 1996 alisema kuwa mbali ya tofauti hiyo pia malipo hayo
hayalipwi kwa mtililiko muafaka kitendo
ambacho kinawaweka katika wakati mgumu na kushindwa kuazima pesa mahali
kwingine kwaajili ya kujikimu.
‘Hatulipwi kwa wakati hali ambayo inatufanya tushindwe hata
kukopa kwa watu pesa kwani hatuna uhakika ni wakati gain tutalipwa pensheni
hizo,mfumo’Alisema na kuongeza kuwa mfumo uliopo umewaweka katika maisha ya
kubahatisha.
Aliendelea kuitupia lawama serikali kwamba,imewapa kisogo
kwa maelezo kuwa mnamo mwaka 2009 waliahidiwa kuongezewa malipo hayo ahadi
ambayo alisema hadi sasa bado haijatekelezwa.
Sambamba na hayo ,mstaafu huyo aliomba serikali iwafikirie
kwenye bajeti yake kuwaongezea wastaafu malipo hayo wapate robo tatu ya mshahara wa kima cha chini
kwa sasa ili kumudu maisha ya sasa ambayo alisema kuwa ni ghali kuliko miaka ya
nyuma.
‘Tunaiomba serikali itufikirie kwenye bajeti ili
kutupandishia malipo yetu kwa kuzingatia umuhimu wetu tulipokuwa tukilitumikia
Taifa letu,tumesahaulika hata kujikuta kama hatukuwa na thamani katika utendaji
wetu’.Alisema
No comments:
Post a Comment