Tuesday, January 10, 2012

BODABODA MBALIZI WAFUNGA MWAKA KWA KUTOA MSAADA

CHAMA cha waendesha  pikipiki katika Bonde la Mbalizi  wameufunga mwaka  kwa kuwatembelea wagonjwa waliolazwa na kuwapatia zawadi  kwenye hospitali ya Jeshi la Wananchi Tanzania na hospitali ya Ifisi zote za Mbalizi mkoani  Mbeya .
 
Akizungumza na JICHO LANGU BLOGU mjini Mbalizi wiki ya kwanza baada ya kuuanza mwaka mpya  mwenyekiti wa waendesha pikipiki au maarufu kwa jina la Boda boda,Maisha Mwakawanga alisema kwamba  waliwatembelea  twagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hizo  mnamo tarehe 31 mwaka jana na kuwapatia zawadi ambazo ni sabuni za kuogea na sabuni za kufulia kila mgonjwa. 

Mwenyekiti huyo alizitaja sababu zilizo wasukuma kutoa zawadi hizo kwa wagonjwa  kwamba ilikuwa ni sehemu ya kumshukuru mwenyezi mungu kuwafikisha hapo walipo wakiwa na vyombo vya moto barabarani lakini wakati huo hawakuona njia nyingine ya kuonyesha shukurani zao kwa muumba ambapo waliona bora wawakumbuke watu ambao waliupokea mwaka huo wakiwa  hospitalini kwaajili ya matibabu.

Alisema kuwa mbali ya wagonjwa hao kulazwa pia wanawaheshimu kama sehemu ya jamii nyingine vilevile ni wateja wao kwa upande wa usafiri huku wakizingatia kwamba kila mwanadamu anapitia matatizo mbalimbali yakiwamo hayo ya maradhi.

Mwakawanga alisema kuwa kabla ya kuamua kutoa zawadi hizo walipata ushauri kutoka kwa muunguzi mkuu wa hospitali ya Ifisi ambaye hakufahamika mara moja jina lake, muuguzi huyo aliwashauri kutoa zawadi za aina hiyo badala ya zawadi walizo kuwa wamefikiria kuzitoa awali kabla ya ushauri wa muuguzi huyo.

Alisema kuwa awali chama hicho kilipanga kupeleka zawadi kama  ambazo ni maji ya kunywa,biskuti kwaajili ya watoto na matunda matunda zawadi ambazo muuguzi wa Ifisi alisema kwa kitaalamu zinaweza kusababisha madhara kwa wagonjwa hivyo alipendekeza sabuni au pesa taslimu.

Mbali ya chama hicho kutoa zawadi hizo kwa wagonjwa pia waliweza kuwazawadia wagonjwa waliokutwa wakisubiri kupatiwa huduma za matibabu na zawadi zingine ziligawiwa kwa wauguzi wa hospitali hizo kama ishara ya upendo kwa wagonjwa wanao wahudumia .

Mwenyekiti huyo alisema ili kufanikisha zoezi hilo wanachama walichangishwa shilingi 2000 kila mmoja wao na baadhi yao waliguswa zaidi na kutoa kiasi kikubwa zaidi ya hicho kilichopangwa kwa kila mwanachama kutoka vikundi saba vya huduma ya Bodaboda kutoka bonde la Mbalizi.

Baadhi ya wagonjwa waliotembelewa na gazeti hili katika hospitali ya Ifisi waliliambia JICHO LANGU BLOGU kwamba walifarijika na kitendo na kusema kitendo hicho kilichofanywa na Bodaboda ni cha kiungwana na kinastahili kupongezwa.

Hata hivyo, Mwakawanga alisema kuwa chama cha kinamtazamo wa kuboresha huduma hiyo katika kuihudumia jamii katika shida na raha na hapo siku za usoni watawashirikisha na wenzao kutoka nje ya Mbalizi ambao baada ya kusikia tukio hilo nao walionekana kuguswa na kusikitika ni kwa nini hawakuhusishwa katika zoezi la kuuaga mwaka  kwa njia hiyo.

No comments:

Post a Comment