- NI KATA MPYA
KATA mpya ya Nsalala katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vijijini imepata viongozi wake baada ya kufanyika uchaguzi uliosimamiwa na halmashauri ya Wilaya hiyo mapema mwezi Desemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kaimu afisa mtendaji wa kata hiyo ,John Mwanampazi uchaguzi huo ulishirikisha vyama vya kisiasa vya Chadema na CCM, Chadema kilifanikiwa kushinda viti vitatu katika nafasi ya vijiji na CCM kikiwa kimefanikiwa kuchukua nafasi moja ya kijiji.
Mwanampazi aliyataja maeneo waliyoshinda Chadema kuwa ni katika kijiji cha Tunduma Road ,Mshikamano na Mageuzi wakati chama cha Mapinduzi wakiambulia kijiji cha Mapinduzi.
Alwataja wagombea walioshinda katika nafasi za uenyekiti wa vijiji kuwa ni Atilio Lugusi ambaye sasa ni Mwenyekiti halali wa kijiji cha Tunduma Road ,Kissman Mwangomale amechukua nafasi ya kukiongoza kijiji cha Mshikamano na katika kijiji cha Mageuzi mwenyekiti wake ni Tubagha Mnyanya.
Kijiji cha Mapinduzi kinaongozwa na Nelson Mwakyusa lakini wakati huo,afisa mtendaji huyo alisema kuwa jumla ya vijiji vtano vinavyo unda kata ya Nsalala vilisimamisha wagombea katika nafasi hizo na wananchi kufanikiwa kutumia haki yao ya kuwachagua viongozi wao.
Hata hivyo mtendaji huyo alisema ni vjiji vnne pekee ambavyo viliweza kufanikisha zoezi hilo katika hali ya amani na usalama na kijiji cha tano kulitokea dosari kwenye kitongoji kimoja ambacho kililazimika kuahirisha zoezi la uchaguzi.
Alikitaja kijiji hicho kuwa ni Ndola ambako zoezi la uchaguzi litarudiwa kufuatia kuwepo kwa dosari za kanuni za uchaguzi kwenye kitongoji cha Tumaini ambacho uchaguzi uliahirishwa .
Mwanampazi alisema kwamba, katika kituo cha kupigia kura kwenye kitongoji cha Tumaini wasimamizi walitishiwa na wapiga kura hivyo hali iliyokuwepo ilitishia usalama na uvunjifu wa amani kwa mujibu wa kanuni ya uchaguzi (27) ambayo inasema kuwa kukiwa na jambo lolote la hatari uchaguzi unaweza kuahirishwa.
Mtendaji huyo alisema kuwa uchaguzi katika kijiji hicho utarudiwa mara tu baada ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo atakapotangaza kufanyika tena upya kwa uchaguzi ndani ya kijiji hicho lakini pia alithibitisha kuwa vijiji vinne vimepata viongozi halali kati ya vijiji vitano vinavyounda kata hiyo.
Alizitaja nafasi za vitongoji kuwa wagombea waligawana nafasi sawa kwa kila chama ambapo walipata viti tisa kila chama na kufikisha idadi ya jumla ya viti 18 vya vitongoji katika vijiji vine ambavyo vilifanya uchaguzi bila matatizo.
Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vijijini,Juliana Malange hazikufanikiwa ili kuzungumzia suala hilo kwa kina lakini habari za kuaminika ni kwamba kata hiyo bado haina watendaji wa vijiji na kata ambao wanaweza kuwa chachu katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika jamii husika.
No comments:
Post a Comment