Tuesday, January 10, 2012

JESHI la polisi wilayani Mpanda limewafikisha mahakamani watu wawili kwa tuhuma za kufungisha ndoa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Rungwa katika mkoa mpya wa Katavi.
 
Waliofikishwa mahakamani ni  Salum Seif Esry (35)mkazi wa  Mpanda ambaye ni baba wa mwanafunzi na  Seif Khalid Abdallah (41) kaka wa mwanafunzi  wakazi wa madukani mjini Mpanda, ambapo wanatuhumiwa kumuoza binti wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Rungwa .
 
Akisoma mashtaka mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya  wilaya ya Mpanda, mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi Timoth Nyika alisema kuwa watuhumiwa hao walifanya kosa la kumuoza mwanafunzi  Jamila Salum (15) baada ya kupokea mahali ya shilingi milioni mbili kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Alifafanua kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo mnamo Novemba 13, 2011 katika msikiti wa Ibadh Jamatini Madukani mjini Mpanda kwa kufungisha  ndoa ya kiisalamu mwanafunzi huyo kwa mwanaume Ally Khalid Abdallah (40) 
 
 Baadae maharusi hao walifanyiwa sherehe katika ukumbi wa Chuo Kikuu huria cha mjini Mpanda.
 
Alisema wakiwa katika sherehe hizo jeshi la polisi lilifanikiwa kufika na kuzuia sherehe hiyo na kuwakamata watuhumiwa huku bwana harusi akiwa akiwa mtuhumiwa wa tatu hakufika ukumbini hapo.
 
Taarifa toka kwa ndugu wa Karibu wa bibi harusi zimedai kuwa awali bwana harusi nia yake ilikuwa ni kuwaoa ndugu wawili wa famuuuu wote wanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari ya Rungwa lakini huyo mwenzake alikataa kuolewa kwa madai kuwa yeye bado anataka kusoma.
 
Kwa upande wake kamanda wa jeshi la polisi mkoani Rukwa, Isuto Mantage alisema jana kuwa jeshi la polisi lilichukua hatua hizo baada ya kupata taarifa ya mkuu wa shule ya sekondari Rungwa, Emanuely Mwamwezi  kuwa mwanafunzi wake wa kidato cha kwanza Jamila Salum (15) amefunga ndoa katika msikiti wa Ibadh Jamatini mjini Mpanda na jioni atakuwa katika sherehe ya kuwpongeza maharusi katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria mjini Mpanda.
 
Alisema baada ya kufika katika ukumbi huo polisi waliwakuta wananchi waalikwa wakiwa wameshaanza sherehe wakimngonjea bwana harusi na hivyo kuzuia sherehe hizo na kuwakamata ndugu wa Bi Harusi mwanafunzi waliokuwamo ambao ni Baba wa mwanafunzi, Salum Seif Esry (35) na kaka wa mwananfunzi, Seif Khalid Abdallah (41).
 
Alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao ilibainika kuwa walikiri kumuoza mwanafunzi Jamila Salum baada ya kupokea mahari ya shilingi milioni mbili fedha taslimu kutoka kwa muoaji ambaye alikimbia baada ya kugundua kuwa jeshi la polisi limeingilia katika harusi yake.
 
Alisema mtuhumiwa ambaye ni muoaji Ally Khalid Abdallah (40) Raia wa Oman anatafutwa na jeshi la polisi aweze kufikishwa mahakamani ambapo watuhumiwa wawili wa kesi hiyo wamekana kosa ambapo wako nje kwa  dhamana hadi kesi hiyo yenye CC Na. 304/2011 itakapotajwa tena mahakamani hapo Desemba 5,2011.
 
Taarifa za shule ya sekondari Rungwa  kwa walimu wake zimedai kuwa maendeleo ya Jamila Salum yalikuwa mazuri sana kitaaluma kwani alikuwa na mahudhurio mazuri na katika mitihani alikuwa anashika nafasi katika kundi la kumi bora darasani kwake katika mitihani ya muhula uliopita.

No comments:

Post a Comment