Tuesday, January 10, 2012

MAABARA MPYA NA YA KISASA KUJENGWA MBALIZI

KANISA la Uinjilisti mkoani Mbeya limekusudia kuboresha huduma za Hospitali teule ya Wilaya ya Mbeya kwa  kujenga maabara ya kisasa  ambayo itagharimu zaidi ya shilingi milioni 25 za kitanzania,imefahamika.
Kwa mujibu wa  mshauri  na mkurugenzi wa maendeleo ya kanisa la Uinjilisti Tanzania, Mchungaji Markus Lehner,ujenzi  wa maabara hiyo tayari umeanza hospitalini hapo ambapo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 25 hadi kumalizika kwa ujenzi huo.
Alisema kuwa ,Kanisa hilo limeamua kuwatumikia wananchi katika huduma hiyo baada ya kupata msaada wa wafadhiri kutoka mataifa ya Ulaya ambao aliwata kwamba ni walezi wa kanisa na huduma zingine zinazo tolewa na kanisa hilo.
Mchungaji  Lehner alisema kwamba,huduma hiyo inatarajiwa kuanza kutolewa mara tu baada ya kukamilika kwa ujenzi  huo mwaka kesho ambapo idadi kubwa ya vifaa vya maabara tayari vimekwisha wasili na baadhi ya vifaa  kanisa limeahidiwa  kupatiwa   mapema mwezi Januari mwaka kesho.
Lehner alisema kuwa  kukamilika kwa maabara hiyo kutasaidia kuwepo kwa ufanisi mzuri na wagonjwa kupata huduma  nzuri zaidi za uchunguzi  wa afya na matibabu bora kasha kupunguza msongamano wa wagonjwa ambao wakati mwingine wamekuwa wakichelewa kupata matibabu kutokana na upungufu wa vifaa vya kitaalamu kwenye maabara iliyopo.
Aidha, alisema kwamba maabara hiyo itawawezesha wanafunzi wa chuo cha uguuzi hospitalini hapo kupata  maarifa ya kina ambayo yatawajengea uwezo mkubwa wa kuihudumia jamii baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Mchungaji huyo alisema kuwa  msimamo wa kanisa ni kumtumikia Mungu pamoja na watu wake na ndio maana limekuwa mstari wa mbele kuboresha mazingira ya Hospitali hiyo tangu miaka 12 iliyopita baada ya kanisa hilo kuweka mkono wake hospitalini hapo.
Awali katika mahafali ya chuo cha uuguzi Ifisi ,katika risara ya wahitimu mgeni rasmi ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Juliana Malange aliambiwa matatizo mbalimbali yanayokikabili chuo hicho kama vile ukosefu wa kompyuta na vitabu mbali ya kuwa Wilaya hiyo ina chuo hicho pekee.
Malange aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu na chuo hicho cha hospitali ya Ifisi na kudai kuwa pesa za ruzuku zinazotolewa na serikali zitaingizwa kwenye mpango huo ili kuendelea kukijengea chuo  uwezo mkubwa wa kutoa maarifa kwa wanachuo na kuwa mabalozi wazuri katika taifa na jamii watakayoitumikia.
Hospitali ya Ifisi imekuwa mkombozi  kwa wananchi kutoka sehemu mbalimbali ambapo imewapunguzia usumbufu na msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali  ya Rufaa  iliyokuwa tegemeo  kanda ya nyanda za juu kusini  na hospitali ya mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment