Tuesday, January 10, 2012

WAHITIMU WAPATIWA VIFAA VYA KUAZIA MAISHA WAENDAKO

KANISA la Uinjilisti mkoani Mbeya hivi karibuni limewazawadia vifaa vya ufundi  wahitimu 34 wa chuo cha ufundi Mbalizi mkoani hapa.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa na makamu  mkuu wa chuo cha ufundi Mbalizi,Titto Nduka katika mahafali ya 51, alisema kila mwanafunzi alikabidhiwa vifaa vya zaidi ya sh.100,000 kwa wanachuo wahitimu 34 katika fani za ufundi wa magari na seremala.
Nduka alisema kwamba,kanisa hilo lilitoa vifaa hivyo kwa kusudi la kuwaandalia maisha ya kujitegemea mara tu baada ya kuhitimu mafunzo yao na kuanzisha karakana zao ambazo watazitumia  na kuweza kupanua wigo wa  ajira nchini.
Mkuu huyo alishauri vijana kujiunga na masomo ya ufundi ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayoizunguka jamii huku akisisitiza kwamba nchi nyingi zimepiga hatua  za kiteknolojia kupitia vyuo mbalimbali vya ufundi ambavyo alisema hapa nchini vijana wengi  hawajahamasika kujiunga na vyuo hivyo.
Nduka alisema kuwa,chuo chake kinakabiliwa na uhaba wa wanafunzi kitendo ambacho kinasababisha chuo hicho kujiendesha kiasara hata wakati mwingine chuo kukosa ufadhiri ambao unategemea mchango wa  chuo kumudu baadhi ya mahitaji badala ya kutegemea  misaada kutoka kwa wafadhiri.
Kufuatia hali hiyo Nduka alishauri serikali itoe mchango wake kwa jamii kwa madai kwamba jamii inapaswa kuelimishwa umuhimu wa  kujiunga na masomo hayo na kuweza kuvifufua vyuo ambavyo viliacha kutoa huduma  ya maarifa ya maisha kwenye jamii.
‘’Si lazima serikali itoe fungu la kuweza kuendesha vyuo vya ufundi bali tunahitaji kupata sapoti hata ya serikali kuhamasisha wananchi ili waweze kujua umuhimu wa kujiunga na vyuo vya ufundi ‘’,alisema na kuongeza kuwa kufanya hivyo serikali inaweza kuongeza vyanzo vyake vya mapato na kuinua uchumi wa taifa.
Alisema kanisa  nguvu ya wafadhiri ndiyo iliyowafikisha mahali walipo sasa japo kwa taabu ambapo alihofu kwamba wafadhiri nao wanaweza kugoma kutoa ufadhiri kwa sababu chuo hicho pamoja na matawi yake kinajiendesha kwa hasara huku baadhi ya matawi ya chuo hicho yakiwa yamefungwa  baada ya kukosa wanafunzi.
Kanisa la Uinjilisti Tanzania limekuwa mfadhiri mkubwa wa chuo hicho ndani ya kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment