Saturday, January 14, 2012

MWAKYOLILE AITAKA SERIKALI IWAADHIBU WACHUNGAJI WA KKKT

ASKOFU ISRAEL MWAKYOLILE AKIZUNGUMZA, KUSHOTO KWAKE NI MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO.
MGOGORO wa madehebu ya dini kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya limeingia sura mpya baada ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Konde kuruhusu Serikali kuchunguza wachungaji wake kama kweli wanajihusisha na biashara hiyo.
Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Konde Israel Mwakyolile hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa kuwa, si kweli kwamba kanisa hilo limewatimua wachungaji wawili kwa tuhuma za kujihusisha  na biashara hiyo haramu kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku nchini.
Alisema kuwa hajui  kama kanisa lake lina mchungaji yeyote anayejihusisha na biashara hiyo na hajawahi kumfukuza mchungaji wake kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya, na kusisitiza kwamba kama kunatuhuma za aina hiyo Serikali inaweza kuchunguza na hatua za kisheria zifuate kwa mchungaji atakaye bainika na tuhuma hizo. “Katika kanisa langu kwenye Dayosisi ya Konde, sijawahi kumfukuza ‘’Lakini mimi sio malaika wala sio Mungu, inawezekana wakawapo mimi siwajui, Serikali inao mkono mrefu ikihisi hivyo milango iko wazi inaweza kufanya uchunguzi na ikiwabaini washitakiwe kama raia wengine,” alisema Askofu Mwakyolile.
Askofu Mwakyolile  amesema kanisa  linakusudia kulishitaki mahakamani gazeti hilo (Jamboleo) kwa kuwa habari hiyo ambayo ilichapishwa Januari Mosi mwaka huu imewaumiza, imewajeruhi na imelidhalilisha kanisa lake.
Askofu huyo pia alitangaza kutomtambua Mchungaji William Mwamalanga ambaye gazeti hilo limemnukuu kwamba ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na haki za jamii, kitengo ambacho alisema hakipo kanisani kwake.
Mwakyolile alisema kwamba  kanisa lake halimjui mchunaji huyo na hivyo linakusudia kwenda mahakamani ili akathibitishe ukweli wa taarifa hiyo aliyoitoa gazetini.
Askofu Mwakyolile alisema kuwa kanisa lake likienda mahakamani litahitaji fidia ya fedha taslimu shilingi milioni 800 kwa uchafuliwa na habari hiyo.

No comments:

Post a Comment