ZAIDI ya shilingi bilioni 300 zitahitajika kwa ajili ya kujenga miradi ya maji katika vijiji 10 kwaajili ya watu wapatao 50,893 Wilayani Mbozi Mkoa Mbeya kufikia mwaka 2020.
Hayo yalisemwa na Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Mbozi Ackson Mwansyange wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji uliofanyika juzi katika kijiji cha Itumbula wilayani humo.
Mhandisi Mwansyange alisema utekelezaji wa Mradi huo unafanyika kupitia Programu ya Maji na usafi wa mazingira vijijini (RWSSP) ambapo kwa Mbozi Mashariki vijiji vya Ihanda, Halungu, Lungwa, Maninga na Utambalila vitanufaika na mradi huo.
Alivitaja vijiji vingine vitakavyonufaika na mradi huo kwa Mbzi Magharibi kuwa ni Namtambalala, Iyendwe, Mnyuzi, Chilulumo na Itumbuka na kuwa mchakato wa programu hiyo umeanza kwa kuchimba visima virefu (Boreholes) 10 katika vijiji hivyo ambavyovitakuwa vikisambaza maji kwa njia ya pampu za mashine ya diseli.
Alisema gharama itakayotumika kujimba visima hivyo ni sh.186,426,620 milioni ambapo katika bajeti ya mwaka 2011-2012 vijiji v3 kati ya 10 vinatazamiwa kujengwa mitandao ya maji ambavyo ni Itumbula, Namtambalala na Maninga ambapo gharama yake inakisiwa kuwa ni sh.931,903,119 na kuwanufaisha watu wapatao 15,308 hadi kufikia mwaka 2020.
Alisema Kijiji cha Itumbula ambacho Mkuu wa Mkoa wa Mbeya aliweka jiwe la Msingi kwa niaba ya vijiji vingine kupitia programu hiyo kimebahatika kupata maji ya kutosha kusambaza kwa wananchi wa kijiji hicho.
Alisema uchangiaji wa wananchi wa mradi huo ni asilimia 5 ya gharama ya mradi sawa na sh.16,636,301/95 ambapo hadi sasa wananchi wa kijiji hicho wamechangia kiasi cha sh.1,300,000 hali ambayo inahatarisha uendelevu wa mradi huo wa maji katika kijiji hicho.
No comments:
Post a Comment